SIMON SSERUNKUMA AGOMA KUFUKUZWA SIMBA
Simon Sserunkuma (kushoto) akielekezwa jambo na kocha mkuu wa Simba, Goran Kopunovic
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Simon Sserunkuma alisajiliwa dirisha dogo na klabu ya Simba, lakini kiwango chake kimeshindwa kuwaridhisha mabosi wa Msimbazi.'
KIUNGO mshambuliaji wa Simba kutoka Uganda, Simon Sserunkuma, ameomba
kuendelea kuitumikia Simba kwa miezi sita zaidi licha ya klabu hiyo
kutangaza kumtema.
Simon Sserunkuma na Waganda wenzake, Dan Sserunkuma na Joseph Owino,
walitangazwa na klabu ya Simba juzi kwamba hawataendelea kuitumikia
klabu hiyo ya Msimbazi baada ya viwango vyao kutowakosha mabosi wao.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans
Poppe, ameuambia mtandao huu muda mfupi uliopita kuwa Simon ameomba
miezi sita wamuangalie zaidi na asiporidhisha katika kipindi hicho,
atakuwa tayari kuondoka.
"Ni kweli wachezaji wetu watatu kutoka Uganda tumeamua kuachana nao,
lakini mmoja ambaye ni Simon Sserunkuma ameomba tumpe miezi sita zaidi
ya kumwangalia," amesema Hanspope.
Kiongozi huyo amesema watavuka nje ya mipaka ya Tanzanua kusaka nyota
wengine wakali watakaoziba nafasi zilizoachwa na Waganda hao.