Mapambano katika vita sikuzote ni kuhakikisha tusitegemee katika
kuamini kuwa, adui hata kuja upande wetu lakini tumsome na kujifunza
kumpokea pale anapowasili.
Usiwaze kuwa hatokushambulia kwanza lakini unahakikisha kuwa unakuwa
kwenye nafasi ambayo inakufanya kuwa salama dhidi yake huku unajipanga
kumdhuru inavyotakiwa, hii ndiyo namna ambayo akili ya ushindi
inavyotakiwa kuwa siku zote, hivyo ndivyo ambavyo Simba humuwinda Nyati
siku zote na kila mla nyama hushika kisu kwa namna hiyo.
Hakuna asiyekuwa na tamaa na mchezo kati ya Manchester United dhidi
ya Arsenal, hakuna jicho ambalo mboni yake haitofurahi kushuhudia uso
mkavu wa Mourinho dhidi ya taswira ya huruma ya Arsenal Wenger
zikitazamana katika nyasi ambazo ni wazi zitaumia kwa dakika 90 na zile
za nyongeza ambazo muuaji wake ni Andre Marriner.
Kila roho itakuwa na hatima yake, kila majigambo yatapata mbabe wake
na hakuna namna nyingine zaidi ya kuamini kuwa kila hasira itabidi
ikinzane na furaha nyingine japo jambo zuri ambalo linaufanya huu mchezo
kuwa wa kuvutia pengine ukaweza kuuita Pizza ni chuki iliyopo baina ya
makocha hawa wawili. Hawakubaliani, hawafuatiliani, na wala
hawahitajiani katika pembe ya kila mmoja, wote wanaamini ni Faru ingawa
mwingine anayeitwa Mourinho pembe yake imemdhuru zaidi Wenger.
Silaha hazishushwi na mageuzi yanayoweza kufanyika siku hii,
Manchester United bado hawana muunganiko kikosini mwao huku Arsenal
wakiwa katika Kitonga na gari yao yani wanateremka tu.
Ozil macho yake yamekuwa makubwa zaidi na sasa anaziona nyavu kwa
ufasaha kuliko alivyokuwa akiona miili ya wenzie ili awapigie pazi za
mwisho, lakini pia Sanchez yupo katika kiwango chake cha Bugatti kiwango
ghali kabisa katika maisha yake ya soka kwa sasa amekomaa, anawahusisha
wengine mchezoni na anafanya kila anayemzunguka aonekane Daudi
anayeweka kumuangusha Goliati yeyote anayekuja mbele yake.
Hii ndiyo silaha yao kwa sasa yani ubora wa watu hawa wawili ndio
unaamua matokeo ya Arsenal kwa kiasi kikubwa huku kisimani wakiachiwa
Granit Xhaka na Francis Coquelin wafate maji.
Mourinho siku zote kuhusu Wenger katika mechi za kimashindano amekuwa
ni nyumba ya Kobe, kila jiwe lilipokuja upande wa kichwa chake
halikumpata kwasababu ilikuwa rahisi kwake kurejesha kichwa ndani huku
akiwa na sumu ya koboko. Kila alipong’ata Wenger alimuua na hakuna namna
ambayo Wenger angeweza kufanya lakini hakuna wakati mzuri ambao pengine
Wenger alikuwa akiuombea kama huu, ule wakati ambao adui hana mikono
huku akitakiwa kukumaliza kwa bunduki.
Manchester United kwa sasa ‘maji kujaa’ lakini nyakati nyingi inakuwa
‘maji kupwa’, Mourinho hajapata muunganiko ambao ulizoeleka hapo kabla
kwenye vilabu vingine alivyopita, pamoja na kuwa kuna nyakati wachezaji
kama Pogba wanakuwa na nyongeza ya kile ambacho wengi wanategemea
kukiona kutoka kwao bado Mourinho taa za gari lake zimezima au mwanga
wake umefifia na hata lile kurunzi alilolinunua ili wakati amezidiwa
limulike halijaweza kuwa fiti huku pia likionekana kutoingia kwenye
mfumo linaitwa Henrikh Mkhitaryan.
Huu pia unaweza kuwa wakati mbaya zaidi kwa Arsenal Wenger kwasababu
kwa namna Manchester United walivyokutana na ugumu katika mechi kubwa,
silaha ya Mourinho inaweza kuwa kujihami na kuwazuia Arsenal ambao
wanatiririka wasiweze kucheza kwa uhuru.
Mourinho ni ngumu kwake kuweka kichwa mahali ambapo nyumba ya Wenger
inaweza kukua hivyo kutaka kufanya pambano liwe refu na wakati ambao
vijana wa Arsenal wanakuwa wameishiwa nguvu au kuondoka kwa wingi ili
wakashambulie aweze kutumia mwanya huo kuwaumiza.
Mamba kamwe hang’oki meno kwasababu uhai wake hutegemea hapo, hivyo
akiwa mpole haina maana kuwa unatakiwa kuweka kiganja kwenye mdomo wake,
hii ndiyo inatakiwa kuwa akili ya Wenger wakati huu.
Pamoja na kuwa Mourinho anaweza kuwa kwenye wakati mgumu bado anabaki
kuwa moja ya makocha wa kiwango cha Dunia na uzoefu wake unaweza
kuwaumiza Arsenal wakati wowote kama hawatokuwa makini na nafasi
wanazozitengeneza na kama Mustafi na Koscielny hawatakuwa makini muda
wote jambo ambalo halijawa tabia yao msimu huu.
Hakuna asiyetamani pilau siku za siku kuu, sembuse hili ambalo
kachumbari katengeneza muhindi? Pilipili yake kila mmoja itamfaa utamu
wake kila mmoja ataufurahia na wapo ambao wanatamani hata mwiko uwe wao
waamue pishi litavyotoka hao wanaitwa Manchester City, Liverpool na
Chelsea. Adui mwombee njaa lakini hawa wanawaombea arosto ili hata dawa
watakazo zihitaji ziendelee kuwalevya.
Unapotamani kuua kwa upanga, kumbuka shoka anaweza kuwanayo jirani,
umakini tu ndio utaamua mchezo huu ingawa hakuna siri sufuria lipo kwa
Mourinho na mwiko anao Wenger mwenyewe wakati huu, ujanja wake tu namna
ya kuivisha, kisipoiva shauri yake.