Sunday, June 26, 2016

ALEXIS SANCHEZ MWANASOKA BORA WA COPA AMERICA



Mshambuliaji nyota wa Arsenal, Alexis Sanchez ametangazwa kuwa mwanasoka bora wa michuano ya Copa America.


Sanchez ambaye ameiwezesha timu yake ya taifa ya Chile kubeba kombe hilo kwa mara nyingine tena, amewapiku nyota wengine wengi wakiwemo Lionel Messi, Angel Di Maria na wengine wengi.

MAGURI ASAINI OMAN MIAKA MITATU, SASA NI MCHEZAJI WA DHOFAR SC


Aliyekuwa mshambuliaji nyota wa Stand United, Elias Maguri amesaini mkataba wa miaka mitatu wa kuitumikia Dhofar SC ya nchini Oman.
Maguri ambaye alionyesha kiwango cha juu msimu uliopita kabla hajaanza kutoelewana na uongozi wa benchi la ufundi la timu hiyo, alisaini mkataba huo jana.
Klabu hiyo ndiyo wawakilishi wa Oman katika michuano ya Bara la Asia, hivyo hii itampa Maguri nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa zaidi.

Awali alikuwa akiwindwa na timu kadhaa ikiwemo Simba ya jijini Dar es Salaam lakini alishindwa kujiunga nazo na kutimkia nchini Oman.
Kabla ya kwenda kwenye timu hiyo, Maguri ambaye alitoka Simba kabla ya kujiunga na Stand aliwahi kufanya majaribio kwenye timu ya TP Mazembe na kusema kuwa amefanikiwa kufuzu, ingawa klabu yake ilimgomea  kwa kuwa hakufuata utaratibu wakati wa kwenda kwenye majaribio hayo.

Msimu uliopita mshambuliaji wa huyo wa Taifa Stars, aliifungia timu yake mabao 15 na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Amissi Tambwe (21), na Donald Ngoma (17).

SIMBA YAMUWEKEA OMOG NAFASI YA KUFANYA USAJILI




Pamoja na kuendelea na usajili, klabu ya Simba imeweka nafasi kwa ajili ya kocha wake mpya ambaye kwa asilimia 95 atakuwa Joseph Omog.

Omog raia wa Cameroon aliyewahi kuipa ubingwa Azam FC, amekubaliana na Simba kila kitu na inaonekana ndiye atakuwa kocha mpya wa Simba kwa kuwa kocha Mghana, Tetteh anaonekana kutokuwa tayari kujiunga na Msimbazi.

“Unajua kocha anapokuja, lazima naye atakuwa na mawazo yake kuhusiana na suala la usajili.

“Pamoja na kufanya usajili, lakini kocha naye atawekewa nafasi kwa wachezaji wa kigeni pamoja na wale wa ndani,” kilieleza chanzo.

“Hii maana yake pamoja na usajili huo ambao ulifanywa na kamati ya ufundi na usajili, mwalimu naye anakuwa na nafasi ya kusajili pia.”


Simba inatarajia kuanza mazoezi rasmi kesho au keshokutwa kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya.

SERENGETI BOYS YAANZA VIZURI KUWANIA AFRIKA, YAITWANGA SHELISHELI MABAO 3-0




 Timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys imeanza vema katika kuwania nafasi ya kushiriki michuano ya Afrika ya vijana chini ya miaka 17 baada ya kuitwanga Shelisheli kwa mabao 3-0.

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Segengeti Boys ingeweza kupata mabao mengi zaidi kama washambuliaji wake wangekuwa makini.

Hata hivyo, walipoteza nafasi nyingi sana na baadaye walionekana kuridhika na ushindi huo.



ATUPELE WA 'KIJANI' AICHA NDANDA FC, ATUA KATIKA KIKOSI CHA WANAJESHI



Mshambuliaji Atupele Green amejiunga na JKT Ruvu kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu.

Green ambaye alikuwa anakipiga Ndanda FC msimu uliopita, msimu ujao ataonekana akiwa na JKT iliyorejea Ligi Kuu Bara.

Tayari kila kitu kimekwenda safi baada ya Green au wa Kijani kumalizana na timu hiyo ya jeshi.




TFF YATOA ONYO, YASEMA YANGA ITAONDOLEWA MASHINDANONI NA CAF


RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI NA RAIS WA CAF, ISSA HAYATOU WAKIWA PAMOJA
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limepokea taarifa juu ya mpango na kauli za baadhi ya viongozi wa Young Africans SC kushawishi mashabiki wao kufanya vurugu dhidi ya warushaji matangazo ya televisheni ya moja kwa moja wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho la Afrika ngazi ya Makundi kati ya Young Africans ya Tanzania na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) utakaofanyika Juni 28, 2016 saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Dar es Salaam.
TFF ikiwa msimamizi mkuu wa mpira wa miguu Tanzania, inawajibika na mara moja inachukua nafasi hii kuwatahadharisha baadhi ya viongozi wa Young Africans, wanachama na mashabiki wao kutofanya hivyo kwani itakuwa ni kinyume na  kanuni za mashindano na mikataba ya udhamini katika hatua hii.
Ikumbukwe kwamba CAF inamiliki asilimia mia moja ya haki za habari na masoko katika ngazi hii ya makundi na jaribio lolote la kukwamisha matangazo ya biashara au utengenezaji na urushaji wa matangazo ya televisheni au ukwamishaji wa shughuli zingine kama hizo kwa CAF au wakala aliyeteuliwa na CAF kutaigharimu klabu mwenyeji si kwa kutozwa faini tu lakini pia uwezekano wa kuondolewa mashindanoni.
Pia TFF inatoa tahadhari hiyo ikiwamo ile ya utamaduni wa kukaa uwanjani ili kuepusha aina yoyote ya vurugu kwenye michezo yake hususani hii ya hatua ya makundi. TFF inafahamu kuwa tayari viongozi wa Young Africans walikwisha kusoma nyaraka na taarifa mbalimbali kuhusu kanuni na masuala ya udhamini kwa timu zinazofuzu hatua ya Nane Bora.Wapenzi wa Yanga wanaombwa kufika kwa wingi na kuishangilia kwa nguvu  timu yao ikiwa ni njia ya kuitia hamasa.Hata hivyo shamrashamra hizo zifanyike kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu za Mpira wa Miguu na sheria za nchi.
Vitendo vya kuashiria vurugu na kufanya vurugu vikithibitishwa katika taarifa ya Mwamuzi, Janny Sikazwe wa Zambia; Kamishna wa mchezo, Celestin Ntangungira wa Rwanda na Mratibu Mkuu Maalumu kutoka Msumbiji, Sidio Jose Mugadza, hatua zake zitachukuliwa dhidi yake ikiwamo KUONDOLEWA KWENYE MASHINDANO. Vilevile vitendo vya kutishia amani,kudhuru mwili au kuharibu mali vitachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za kijinai.
Katika mchezo huo wa kimataifa Na. 107, Mwamuzi Sikazwe atasaidiwa na Jarson Emiliano dos Santos kutoka Angola atayekuwa kwenye mstari wa kulia (line 1) na Berhe O’Michael wa Eritrea atayekuwa upande wa kushoto (line 2) huku Wellington Kaoma wa Zambia akiwa ni mwamuzi wa akiba.
Wakati huohuo, kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini kinatarajia kukaa siku ya Jumamosi tarehe 2 Julai 2016. Taarifa zaidi itatolewa karibuni.

-------------------------------------------------------

-------------------------------------------------------
HABARI MPYAMPYAhttp://2.bp.blogspot.com/-mFnDPXvIysA/VOZH1z-2rpI/AAAAAAAAADs/shOR30FtkF4/s1600/anigif.gif