Na Saleh Ally
UWANJA
unaotumiwa na Mouloudia Olympique de Bejaia au Mo Bejaia unajulikana
kwa jina la Unite Maghrebine, uko katika Mji wa Bejaia.
Kutoka
mji mkuu wa Algeria uliotwao Algiers hadi Bejaia ni umbali wa Kilomita
228, umbali wa saa 3:30 kwa gari kwa mwendo chini ya sheria za nchi ya
Algeria.
Usiku
wa kuamkia keshokutwa, Yanga watakuwa uwanjani tayari kuwavaa wenyeji
wao Bejaia katika mechi yao ya kwanza ya kihistoria ambayo kamwe haiwezi
kuwa rahisi kama ambavyo mashabiki wanaifikiria.
Tunaiita
mechi ya Kihistoria kwa kuwa gumzo lilikuwa ni Yanga kufuzu katika
michuano hiyo lakini sasa ni kuanza kushiriki rasmi na kucheza kwa mara
ya kwanza.
Kinachotakiwa
kikubwa ni Yanga kuanza kucheza michuano hiyo na kufanya vizuri. Mechi
ya kwanza inaweza kuwa dira nzuri ya mwendo wa Yanga kwa ajili ya
kujenga hali ya kujiamini katika mechi nyingi zinazofuatia.
Ukiangalia
kishabiki, unaweza kuona Yanga wana kazi rahisi sana kwa kuwa Bejaia
ambayo imeanzishwa mwaka 1954 ni changa hata kwao ambao walianzisha
klabu yao mwaka 1935. Lakini ukweli unaonyesha hivi, Bejaia wana kiu
kali ya maendeleo na litakuwa kosa kubwa kuanza kuwachukulia kwa udogo
au wenye kasi ndogo kama Bajaj unapolinganisha na gari lenye mwendo kasi
kama Range Rover Vogue.
Kubali
kwamba, Mo Bejaia wanataka kufanya vema zaidi na lazima watataka
kuimaliza Yanga hasa nyumbani. Ndiyo maana licha ya kuwepo kwa timu
kubwa na maarufu za Algeria kama USM Alger, JS Kabylie na ES Setif
lakini wao wanaendelea kuwa wawakilishi wa nchini hiyo katika michuano
ya Kombe la Shirikisho.
Kitakwimu
inaonekana Bejaia ni timu yenye mwendo wa saizi ya kati lakini makini
kwenye ulinzi na haifungi mabao mengi sana lakini wastani wake wa
ushindi uko juu.
Katika
michuano ya kimataifa, hili Yanga wanapaswa kulitazama zaidi.
Inaonekana haijapoteza mechi nyumbani na ilifanikiwa kupata ushindi
zaidi ya mara mbili ambao unakwenda kuanzia mabao mawili hadi matatu,
ikiwa nyumbani imekuwa ikiruhusu mabao machache sana.
Kibaya zaidi, inaonekana ni timu ngumu kuruhusu mabao ikiwa nyumbani, jambo ambalo Yanga watatakiwa kulifanyia kazi sana.
Takwimu
zinaonyesha timu hiyo, ilikwenda vizuri kwenye Ligi Kuu ya Algeria
ingawa ikakwama katika nafasi ya sita. Lakini pointi kati ya aliye
nafasi ya pili na nafasi ya sita ni mbili au tatu tu, jambo ambalo
linaonyesha pia ligi ya nchi hiyo ilikuwa na ushindani wa juu kabisa.
Takwimu
za uchezaji, zinaibeba sana Mo Bejaia licha ya ligi ya ushindani wa juu
wa nyumbani kwao. Ukiangalia, ni nadra sana kucheza mechi mbili bila ya
kushinda.
Takwimu
zinasema imeweza kucheza mechi tatu bila ya kupoteza na ikacheza mechi
tano mfululizo bila ya kupata sare, maana yake ni timu inayochipukia
lakini hatari sana.
Yanga
hawatatakiwa kuibeza kwa kuwa kufikia hatua hiyo moja ya timu
ilizozitoa kwenye Kombe la Shirikisho ni Club African ambayo ndiyo timu
yenye mashabiki wengi zaidi nchini Tunisia ikifuatiwa na Esperance
halafu Etoile du Sahel.
Ukiachana
na hivyo, ndani kuna wachezaji ambao iwe isiwe, Yanga inapaswa kuwa
makini nao kwa kuwa rekodi zao kiufungaji katika mechi za nyumbani na
hizo za kimataifa wamethibitisha ni watu hatari sana.
Mfano
Mohammed Waliou Ndoye raia wa Senegal ambaye anavaa namba jezi 19, huyu
ni mtu hatari. Katika mechi nne kafunga mabao matatu, hizi ni zile za
Ligi Kuu Algeria lakini zile za kimataifa, mechi nne kafunga mabao
mawili. Ninaamini Yanga wamejiandaa zaidi yake kwa kuwa ni mwepesi na
hatari kwenye kupiga mashuti.
Bado
wana kiungo Zahir Zerdab anayevaa namba 22 mwenye uraia wa Ufaransa pia
Faouz Yahaya mwenye namba 10 mgongoni, ni watu hatari ambao rekodi za
ufungaji za mabao mawili katika kila mechi nne zinawabeba.
Kitu
kingine kizuri kwa Waarabu hao ni kwamba ina wigo mpana wa wafungaji.
Niliowataja kama watashindwa kufunga bao kuna akina Soumaila Sidibe raia
wa Mali, Ismail Belkacemi ambao wamekuwa mara kwa mara wanapatikana
katika listi ya wafungaji.
Kingine
wanachopaswa kukumbuka Yanga ni kwamba sehemu ya ulinzi, Mo Bejaia
wanaonekana kuwa imara sana. Ni timu yenye mashambulizi machache lakini
mazito, lakini haitaki kabisa kufungwa.
Lazima
tumwamini Pluijm na wachezaji wa Yanga, lakini lazima tuwakumbushe kama
namna hii. Tuwaamini wamejiandaa vizuri lakini umakini ndani ya dakika
90 unapaswa kuwa juu zaidi ya mechi zote walizocheza.
Ugenini kuna ugumu wake, lakini umakini wa juu au zaidi kama ule katika mechi dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola, unahitajika.
TAKWIMU ZA MO BEJAIA:
Cheza mechi bila kupoteza: 1
Kucheza mechi bila kushinda: 1
Kucheza mechi bila kupoteza: 3
Sare za mfululizo katika mechi tano: 1
Kushinda mechi za nyumbani mfululizo: 1
Kucheza nyumbani bila kupoteza mfululizo: 8
Mechi za nyumbani mfululizo bila ya sare: 1
Mechi mfululizo za ugenini bila kushinda: 5
Kucheza ugenini mfululizo bila kupoteza: 2
Ushindi mkubwa 5-1
Kipigo kikubwa 0-2
Wastani wa mabao kwa mechi 2.05