Desemba imefika na hali ya mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Uingereza inazidi kuwa mbaya. Baada ya kucheza mechi 16, wamepoteza 9 na mpaka sasa wana pointi 15 tu – presha ya kumtimua kocha Jose Mourinho inazidi kupanda.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari leo mchana manejimenti ya timu inayoundwa na — Bruce Buck, Marina Granovskaia, Eugene Tenenbaum and Michael Emenalo — watakutana pamoja na Mmiliki Roman Abramovich kuamua hatma ya Mourinho.
Roman Abramovich itampasa aingie mfukoni na kumlipa Jose Mourinho kiasi kisichopungua £40million ikiwa menejimenti itaamua kumfukuza kazi leo Jumatano.
Wakati mreno huyo aliporejea katika klabu mwaka 2013, bodi ya menejimenti ilipiga kura 3-2 ili kumrudisha. Leo inaweza kuwa tofauti.
Kulipa fidia ya mkataba wa wake wa miaka minne unaomfanya alipwe £250,000 kwa wiki ni moja ya sababu kuu nyuma ya kusita kwa Chelsea kumtimua kazi Mourinho muda mfupi baada ya kusaini mkataba mpya.
Mourinho alikubali kuongeza mkataba mpya mwishoni mwa msimu uliopita lakini klabu ilisubiri mpaka mwezi August kabla ya kusaini mkataba mpya rasmi.
Baada ya kushinda ubingwa vizuri sana, Chelsea waliamini alikuwa kocha bora zaidi duniani na wakakubali kumuongezea mkataba wa miaka minne bila kukubaliana kuweka kipengele cha makubaliano endapo wakiamua kumtimua kazi. Sasa hivi endapo Abramovich atataka mreno aondoke itabidi amlipe fidia ya £40m – hii itakuwa mara ya pili Mourinho kulipwa fidia baada ya kufukuzwa na Chelsea.