Pamoja
na kwamba safari ya kiungo wa Azam, Farid Mussa kwenda Hispania katika
Klabu ya Tenerife kuonekana kukwama kutokana na kiungo huyo kukosa hati
ya kufanya kazi nchini humo, uongozi wa Azam FC umeweka wazi kwamba
hauna mpango naye licha ya kwamba hana timu ya kuichezea mpaka sasa.
Farid
ambaye aliuzwa na Azam kwenda Tenerife tangu mwanzoni mwa msimu huu wa
ligi ulipoanza mpaka sasa ameshindwa kuitumikia timu hiyo inayoshiriki
Ligi Daraja la Pili nchini humo kutokana na mabadiliko ambayo yamefanywa
ndani ya timu hiyo.
Msemaji
wa timu hiyo, Jaffar Idd amesema hawana mpango wa kumsajili Farid
kwenye kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo na kumfanya aendelee
kubaki hapa nchini kwani wao lengo lao ni kuona winga huyo anacheza soka
la kulipwa.
“Ingawa
tangu tuachane na Farid katika msimu uliopita na yeye kushindwa kucheza
soka kokote pale mpaka sasa lakini katu jambo hilo halitufanyi
tumsajili tena mchezaji huyo kwa muda huu kwa sababu tayari kila kitu
kimeshakamilika kule kwenye timu yake na kinachosubiriwa ni wao wenyewe
tu.
“Lengo
letu ni kuona ndoto yake ya kucheza nje ya nchi inatimia na hilo ndilo
tunalosimamia sisi na hata kama kwa muda huu ambapo hana timu yoyote ya
kuichezea katu sisi hatuwezi kumsajili na kumrudisha kundini.
“Hata
Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) sisi tumeshatoa na hapo utaona
lengo letu ni kutaka kuona anaondoka na kucheza huko kwa ajili ya
kufungua milango kwa wengine kucheza soka la kulipwa,” alisema Jaffar.
SOURCE: CHAMPIONI