Saturday, June 25, 2016

KATIBU MPYA WA SIMBA AMEAHIDI MAMBO MAKUU MAWILI KWA MASHABIKI



img_9676.jpg
Patrick Kahemele amesaini mkata wa miaka miwili kuitumikia Simba kama Katibu Mkuu wa klabu hiyo baada ya mabingwa hao wa zamani kukaa kwa muda mfefu bila kuwa na mtendaji mkuu wa shughuli za klabu yao.
Kahemele ameahidi mambo makuu mawili katika uongozi wake wa miaka miwili ndani ya Simba. Jambo la kubwa na kwanza ni kuifanya Simba ijitegemee na kuacha kutegemea mifuko ya watu wachache lakini huu ukiwa ni mpango wa muda mrefu. Jambo la pili ni kuisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara ilioukosa kwa misimu minne sasa.
“Simba ni timu kubwa, imekuwa na hamu ya mafanikio ndani ya uwanja na nje ya uwanja. Tukizungumza nje ya uwanja, klabu inahitaji kujitegemea na naamini wana Simba wana mawazo mengi, kikubwa ni kukaa na kushirikiana tuweke mawazo yetu pamoja na kuona ni jinsi gani tunaweza tukaikwamua klabu ya Simba kutoka kutegemea mifuko ya watu wachache hadi kuwa klabu inayojitegemea na kusimama yenyewe,” amesema Kahemele ambaye ataanza majukumu yake ya kazi Julai 1 mwaka huu.
“Hiyo ni mipango ya muda mrefu katika kipindi cha miaka miwili ningependa nifanikishe hilo ambalo hata nikiondoka mimi pamoja na viongozi wenzangu tunakuwa tumefanya kitiu flani. Lakini la msingi kabisa ni kuhakikisha msimu ujao lazima ubingwa uende Msimbazi kwasababu Simba ni timu ambayo imezoea kushinda vikombe lakini kazi hiyo inaanzia kwenye usajili, lazima tuwe na timu nzuri, benchi la ufundi zuri, timu ipate kambi na huduma nzuri na vyote hivyo vikiwekwa pamoja hakuna linaloshindikana.”
Anatoa neno kuhusu mashabiki wa ‘mnyama’
“Mashabiki wa Simba ni wastaarabu sana, sijawahi kuona mashabiki wa Simba wakitia presha, mashabiki wa Simba wakikupa shida ujue umewakosea lakini kama hujawakosea hawana shida kabisa.”

KESSY ATACHEZA DHIDI YA MAZEMBE? TFF IMETOA UFAFANUZI


Kessy-Algeria
Shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia msemaji wake, Alfred Lucas limesema kuwa, linashughulikia sakata la uhamisho wa mchezaji Hassan Kessy Ramadhani kutoka Simba kwenda Yanga ili aweze kucheza kwenye mchezo wa kimataifa kati ya Yanga dhidi ya TP Mazembe unaotarajiwa kuchezwa siku ya Jumanne June 28 kwenye uwanja wa taifa.
“Tayari Yanga wameshaandika barua imekuja TFF wakiomba suala la Kessy liweze kumalizwa haraka ili waweze kumtumia kwenye mchezo wao wa Jumanne dhidi ya TP Mazembe,”amesema Alfred Lucas afisa habari wa shirikisho la soka Tanzania.
“Niwahakikishie mashabiki wa Yanga kwamba TFF weekend yote hii kwa maana ya leo Jumamosi na Jumapili tutalifanyia kazi hilo na tayari mawasiliano yameshafanyika ili Yanga waanze kumtumia mchezaji huyu mara baada ya mkataba wake kuisha.”
“Lakini kama kuna kikwazo chochote tunajaribu kufikiria ili Yanaga wawe huru kusiwe na dosari yeyote kwenye michuano hii halafu sababu ikawa ni kuwakosa wachezaji wake wote iliyowasajili kwa ajili ya michuano hiyo.”
“Naamini kwa uungwana waliokuwa nao Simba kama kuna kikwazo watakiondoa ili mchezaji huyo aendelee kipaji chake na maisha mengine yaendelee.”
Kessy hakuruhusiwa kucheza kwenye mchezo wa kimataifa kati ya Yanga dhidi ya MO Bejaia kwasababu kibali chake kutoka Simba kwenda Yanga kilikuwa hakijathibishwa.

PAUL SCHOLES ASAINI MKATABA KUCHEZA SOKA INDIA


Scholes

Mchezaji wa zamani wa Manchester United na England Paul Scholes amesaini mkataba wa miaka mitatu kucheza kwenye ligi ya Premier Futsal nchini India. Mchezaji huyu wa Man United amatajwa kuwa mmoja wa nyota watakaocheza ligi hiyo pamoja na Deco.
Huu utakuwa msimu wa kwanza wa ligi hii mpya ambayo itahusisha kuchezwa kwa aina ya mchezo wa mpira wenye sheria tofauti .
Mchezo huu unachezwa na wachezaji watano pekee kwa kila timu pia utumia mpira mdogo zaidi, unaodunda zaidi na unachezwa ndani na si uwanjani kama ilivyozoeleka.
“Futsal ni mchezo unaofurahisha, na umetoa mchango mkubwa sana katika kukuza vipaji vya wachezaji wakubwa zaidi kuwahi kutokea,” alisema Scholes.
“Premier Futsal ni njia nzuri sana ya kutambulisha mchezo wa mpira India, na nasubiri kwa hamu sana kupata nafasi ya kuwasilimia mashabiki wote nchini India ambao najua ni kati ya mashabiki bora zaidi duniani.”
Mchezaji wa zamani wa Barcelona Deco na wachezaji mbalimbali wengine wa mchezo wa Futsal wameshasaini mkataba kucheza ligi hii na waandaji wa ligi hii wameahidi kwamba majina mengine makubwa lukuki yatajiunga na ligi hii hivi punde.
“Tangu tuzindue ligi yetu tulisema kwamba tunatia jitihada kuleta vipaji mbalimbali nchini India na kama inavyonekana kweli tunatimiza ahadi yetu.”
Scholes 41, alifanikiwa kushinda ubingwa wa Ligi mara 11 na klabu ya Manchester United pamoja na ligi ya mabingwa 2 akiwa klabu ya Manchester United kabla ya kustaafu mwaka 2013.
Raisi wa Ligi hii ni Luis Figo mchezaji wa zamani wa Real Madrid na Barcelona.

OSCAR JOSHUA ARUDISHA MATUMAINI, AANZA KUJIFUA UTURUKI




Yanga itakuwa dimbani Jumanne ijayo kuwavaa TP Mazembe katika mechi ya Kundi A ya Kombe la Shirikisho Afrika linaloandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) dhidi ya TP Mazembe, hofu kubwa ya timu hiyo ni beki ya kushoto.

Wachezaji wawili wanaocheza nafasi hiyo, Haji Mwinyi na Oscar Joshua wote wapo katika hatari ya kuikosa mechi hiyo, hivyo Yanga ipo katika wakati mgumu wa nani acheze nafasi hiyo.

Mwinyi yeye ana kadi nyekundu aliyoonyeshwa katika mchezo uliopita wa michuano hiyo dhidi ya MO Bejaia ya Algeria wakati Joshua ana maumivu ya nyama za paja, pia aliyapata katika mchezo huo.

Habari njema kwa Yanga ni kwamba, Joshua tayari ameanza mazoezi mepesi kambini huko mjini Antalya, Uturuki ambako timu hiyo imejichimbia kujiandaa na mechi dhidi ya TP Mazembe.

Kutoka Uturuki, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema: “Joshua anaendelea vizuri na tayari ameanza mazoezi mepesi kwa ajili ya kujiandaa na mechi na Mazembe.

“Bado sijajua hatma yake kama atacheza au hatocheza mechi na Mazembe, hivyo kila kitu kitajulikana ikiwa imebaki siku moja kabla ya mchezo wao baada ya daktari wetu Edward Bavo kutoa ripoti yake.”

Joshua alipata majeraha hayo usiku wa Jumapili iliyopita dakika ya 32 katika mchezo dhidi ya MO Bejaia mjini Bejaia, Algeria ambapo ilibidi atolewe na nafasi yake kuchukuliwa na Mwinyi. Katika mchezo huo, Yanga ilifungwa bao 1-0.

JEMBE LIMEREJEA UWANJANI, NI JUMA ABDUL, APIGA DAKIKA ZA FULL GAME MAZOEZINI


JUMA ABDUL
Yanga huenda ikashusha pumzi kidogo katika nafasi ya beki ya kulia kwani Juma Abdul ameanza mazoezi ya nguvu na jana Ijumaa asubuhi alicheza dakika 90 uwanjani.

Abdul aliumia kifundo cha mguu katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA dhidi ya Azam FC hivi karibuni ambapo Yanga ilishinda mabao 3-1, siku alipoumia nafasi yake ilichukuliwa na Mbuyu Twite.

Alitibiwa na kupata nafuu lakini akajitonesha katika mchezo wa Taifa Stars na Misri wa kufuzu Kombe la Afrika 2017 na tangu hapo hakuonekana uwanjani, ambapo alikuwa akiuguza jeraha hilo.

Baada ya kufanya mazoezi ya ufukweni kwa wiki nzima, jana Abdul alifanya mazoezi ya uwanjani kwenye Uwanja wa Garden uliopo Vijana, Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo alitumia dakika 90.

SALEHJEMBE ilimshuhudia Abdul akianza na zoezi la kukimbia akizunguka uwanja mara 20 kabla ya kucheza uwanjani.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Abdul alisema: “Nipo fiti kabisa na ninaweza kucheza mechi na TP Mazembe, wiki nzima nilikuwa na programu ya mazoezi ya stamina katika Ufukwe wa Coco.

“Leo (jana) ndiyo nimeanza kucheza uwanjani na nimetoka freshi kabisa na sina shaka hata nikipewa mechi ya Mazembe.”

Wakati wenzake wakiwa kambini Antalya, Uturuki, beki huyo alikuwa chini ya uangalizi wa Daktari Haroun Ally.

Yanga itacheza na TP Mazembe, Jumanne ijayo mchezo wa Kundi A wa Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 

SIMBA YAANZA TENA HARAKATI ZA KUMSAJILI MAVUGO, ATATUA NCHINI SOOOOON...



Wakati wowote kuanzia sasa Simba itamleta nchini straika Laudit Mavugo baada ya kumaliza mkataba wake kuitumikia Vital’O ya Burundi baada ya awali dili hilo kushindikana.

Tangu mwaka jana, Simba ilikuwa ikimuwania Mavugo raia wa Burundi kila kipindi cha usajili kinapofika lakini mambo huaribika na ikabidi isubiri hadi straika huyo alipomaliza mkataba wake.

Mmoja wa mabosi wa Kamati ya Usajili ya Simba ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema Mavugo atatua wakati wowote kuanzia sasa na tayari alisaini mkataba wa miaka miwili tangu msimu uliopita.

Alisema mkataba huo uliigharimu Simba Sh milioni 36, lakini awali walibanwa na mambo ya mkataba wa straika huyo na timu yake hivyo kungoja hadi amalize mkataba.

“Mavugo atawasili nchini wakati wowote kuanzia sasa kwa kuwa ni mchezaji wetu na alisaini mkataba wa miaka miwili ya kuitumikia Simba na fedha zilizotumika kwenye usajili wake ni Sh milioni 36.

“Kwa sasa mkataba wake umekwisha kule katika timu yake aliyokuwa akiichezea, hivyo yupo huru na ni uhakika atatua kuja kuichezea Simba msimu ujao,” alisema bosi huyo. 

Mavugo ana uwezo mkubwa wa kuzifumania nyavu na Simba inaamini atakuwa mkombozi wao msimu ujao na kuzima ngebe za wapinzani wao.

SOURCE: CHAMPIONI

-------------------------------------------------------

-------------------------------------------------------
HABARI MPYAMPYAhttp://2.bp.blogspot.com/-mFnDPXvIysA/VOZH1z-2rpI/AAAAAAAAADs/shOR30FtkF4/s1600/anigif.gif