Chile imeifunga Colombia kwa bao 2-0 kwenye mchezo wa nusu fainali ya Copa America Centenario na itakutana na Argentina kwenye mchezo wa fainali kwenye uwanja wa MetLife mchezo wa fainali unaozikutanisha timu hizo baada ya mwaka mmoja.
Magoli ya mapema ya Charles Aranguiz na Jose Fuenzalida yaliipa La Roja uongozi wa game hiyo mapema , licha ya Colombia kutengeneza nafasi za kutosha, hawakuweza kubadili matokeo hayo.
Chile na Argentina zimekuwa ni bora kwenye mashindano kwa muda mrefu na zinastahili kupambana kuwania ndoo ya Copa America kwenye mchezo wa fainali siku ya Jumapili.
Ni nafasi kwa Argentina kulipa kisasi baada ya kupoteza mchezo wa fainali ya michuano hiyo mbele ya Chile waliokuwa wenyeji wa mashindano mwaka uliopita.
Chile watakuwa na faida ya urejeo wa kiungo wao Vidal huku Diaz akitarajiwa kuwepo kwenye kikosi baada ya kuwa majeruhi huku kikosi kizima kikiwa kwenye form nzuri.
Argentina ndiyo wanapewa nafasi kubwa kwasababu ya walishaichapa Chile bao 2-1 kwenye hatua ya makundi. Argentina walicheza mchezo huo bila ya uwepo wa nyota wao Lionel Messi aliyekuwa akiuguza maumivu ya mbavu.
Wakiwa bila ya Ezequiel Lavezzi ambaye anauguza majeraha ya kiwiko, kikosi cha Tata Martino bado kina nyota wengine wengi ambao wanaweza kuziba nafasi hiyo.
Argentina watakuwa kwenye presha kubwa ukilinganisha na Chile. La Albiceleste haijafanikiwa kutwaa taji hilo tangu ilipolinyakua kwa mara ya mwisho mwaka 1993. Baada ya kupoteza fainali mbili hivi karibuni ile ya Kombe la Dunia pamoja na Copa America, watakuwa wanataka kurekebisha makosa.
Messi bado ameendelea kukumbwa na jinamizi la kushindwa kutwaa mataji akiwa na timu yake ya taifa, Jumapili itakuwa ni nafasi yake nyingine ya kukamilisha ndoto zake za muda mrefu.