Uwanja wa CCM Kirumba wa mkoani Mwanza umeidhinishwa na CAF pamoja na FIFA kutumika kwa mechi za kimataifa baada ya kukidhi vigezo na viwango vya kimataifa.
Rais wa TFF Jamal Malinzi ametweet kuwapongeza wakazi wa jiji la Mwanza baada ya maofisa wa CAF na FIFA kuupitisha uwanja huo baada ya kumalizika kwa ukaguzi.

Yanga walikwama kuutumia uwanja huo kwa mechi yao ya kombe la shirikisho dhidi ya MC Alger kutokana na uwanja huo kutokidhi baadhi ya vigezo.
Kabla ya mechi hiyo, Yanga walituma maombi CAF wakitaka kubadili uwanja kutoka uwanja wa taifa kwenda CCM Kirumba lakini baada ya uwanja huo kukaguliwa afisa wa CAFalibaini kasoro kadhaa ambazo aliagiza zifanyiwe kazi kabla ya kuanza kutumiwa kwa mechi za kimataifa.
Baada ya marekebisho na ukarabati uliofanywa, sasa uwanja huo utatumika kwa mechi za kimataifa hivyo wakazi wa Mwanza huenda wakaanza kushuhudia michezo ya kimataifa kwa ngazi ya vilabu pamoja na ile ya timu za taifa.