Nusu fainali ya kwanza ya michuano ya Euro inapigwa leo, kati ya Ureno na Wales, mchezo utakaofanyika katika dimba la Stade des Lumières lililopo jijini Lyon majira ya saa nne za usiku.
Huu ni mchezo ambao unabeba hisia kubwa kutokana na kukutana kwa mafahari wawili wa Real Madrid Gareth Bale na Cristiano Ronaldo.
Taarifa kutoka kila timu
Kiungo wa Wales Aaron Ramsey na mlinzi Ben Davies wote hawatakuwepo kutokana na kutumikia adhabu ya kuwa na kadi mbili za njano.
Nafasi ya Ramsey inaweza kuzibwa na Jonny Williams, Andy King au Dave Edwards.
James Collins anaweza kuziba nafasi ya Davies au vinginevyo, Jazz Richards anaweza kuanza kama beki wa kulia huku Chris Gunter akihamishiwa katikati kucheza kama beki wa kati.
Ureno watakuwa wakifuatilia kwa karibu maendeleo ya beki wao Pepe, ambaye alifanya jana alifanya mazoezi peke yake kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya paja.
William Carvalho hatakuwepo kwenye mchezo wa leo, hivyo Danilo anatarajiwa kujaza pengo hilo kwenye nafasi ya kiungo wa kati kwa upande wa Ureno.
Beki wa kushoto Raphael Guerreiro na kiungo Andre Gomes ambao walikosa mchezo wa robo fainali dhidi ya Poland kufuatia kusumbuliwa na maumivu ya misuli, wanarejea leo baada ya kupona.
Kocha wa Ureno Fernando Santos amesema kwamba endapo atakuwa hana uhakika na afya ya Pepe basi hatamchezesha beki huyo.
“Kwa upande wa Pepe, pengine utakuwa unajitekenya na kucheka mwenyewe kitandani kwasababu sitaweza kujibu swali hilo,” alisema.
“Kama Pepe anakuwa fiti kwa asilimia 100, nitafikiria juu ya hilo na pengine anaweza kuanza mchezo wa leo. kama haitawezekana pia hakuna tatizo. Wachezaji wote wanapaswa kuwa fiti kwa asilimia 100 kwa ajili ya mchezo huu.”
Uchambuzi wa mchezo.
Hili ni pambano la kihistoria kwa upande wa Wales, ambao wanaenda kwa mara ya kwanza wanacheza mchezo mkubwa wa kimashindano katika jiji la Lyon.
Ureno kwa upande wao kuna tofauti kidogo, wana uzoefu mkubwa wa kucheza kwenye hatua hii. Hii ni mara ya saba kwa ‘Wamakonde’ hao wa kizungu kufika hatua hii kwenye michuano ya Kombe la Dunia na Michuano ya Ulaya, lakini mara moja tu wakifanikiwa kuvuka hatua hio na kutinga fainali. Walifanya hivyo kwenye Euro ya mwaka 2004.
Mpaka sasa Ureno hawajashinda mchezo wowote ndani ya dakika 90 kwenye michuano ya mwaka huu. Lakini nguvu yao ya kuamua matokeo ilionekana kwenye mchezo dhidi ya Croatia na Poland, na leo watakuwa na kazi nyingine nzito dhidi ya wabishi wa Wales.
Santos ana imani kwamba timu yake itapata matokeo chanya leo.
“Sina wasiwasi wowote juu ya mchezo wa leo, Ninachoangalia kwa sasa ni kufika fainali na kubeba kombe tu,” amesema.
“Napenda kucheza soka la kuvutia? Ndio, ni kweli. Lakini kuna tofauti kati ya kucheza soka la kuvutia na kurudi nyumbani, au kucheza soka bovu na kuendelea kubaki hapa, ningependa kucheza soka bovu na kuendelea kubaki hapa.”
Tofauti na wapinzani wao, Wale wamekuwa kwenye kiwango bora kabisa kwenye michuano hii hasa kwenye mchezo waliopata ushindi mnono dhidi ya Belgium. Lakini bado wanaamini kuna mengi zaidi ya hapo yanakuja pengine ikibidi kufika fainali na kuchukua kombe na kuweka rekodi mpya.
“Ni dhahiri tumevuka malengo ya watu wengi,” amesema Gareth Bale.
“Lakini siku zote tuliamini tungefanya hivi, kama unakumbuka walichofanya mwaka 2004 na Denmark mwaka 1992, sasa kwanini sisi tushindwe kufanya hivyo?”
Mfanikio ya Wale yamewachanganya na wachezaji wenyewe. Kiungo Joe Ledley alipaswa kufunga ndoa Jumamosi lakini aliamua kuahirisha.
“Nilikuwa na iamni kubwa kwamba tungeweza kufanya kitu kwenye michuano hii, na ndiyo maana nikapanga mapumziko yangu yaanze tarehe 11 July, siku moja baada ya fainali, mimi sipo kama wengine!”Bale alimaliza.
Takwimu za mechi walizokutana
- Kabla ya mchezo wa leo, timu hizi zimekutana mara tatu tu na haikuwa kwenye michezo ya mashindano
- Kati ya michezo hiy, Ureno wameshinda mara mbili na Wales kushinda mara moja.
- Mara ya mwisho kukutana ndani ya miaka 65 iliyopita, ilikuwa ni kwenye mchezo wa kirafiki mwaka 2000 na Ureno kushinda magoli 3-0.
- Ureno wamepoteza nusu fainali sita kwenye michuano ya Kombe la Dunia na Euro na kushinda moja tu dhidi ya Uholanzi kwa mabao 2-1 mwaka 2004, kwenye Euro iliyofanyika nchini mwao na Ronaldo alifunga goli kwenye mchezo huo.
- Hii ni mara ya tano kwa Ureno kufika hatua ya nusu fainali kwenye Michuano ya Euro.
- Mechi sita za mwisho kwa Ureno kwenye Michuano ya Ulaya iliisha kwa sare baada ya dakika 90. Mitano ni kwenye Euro ya mwaka huu na mmoja wa nusu fainali dhidi ya Uhispania kwenye Euro ya mwaka 2012 ambapo walipoteza kwa penati. Mchezo huo uliisha kwa suluhu.
- Ureno hawajafungwa kwenye michezo 12 ya mashindano chini ya kocha Fernando Santos (ushindi mara nane, sare mara nne), ushindi katika michezo yote nane ukiwa ni kwa tofauti ya goli moja-moja. Mchezo wao dhidi ya Poland unahesabiwa kama sare.
- Cristiano Ronaldo amefunga magoli 2 tu katika michezo 13 ya mtoano kwenye michuano ya kimataifa. Amebakisha goli moja tu kufikia rekodi ya ufungaji bora wa muda wote ya magoli tisa inayoshikiliwa na Michel Platini kwenye michuano hii.
- Nani amehusika kwenye magoli matatu kati ya sita ya Ureno kwenye Michuano ya Euro mwaka huu, amefunga magoli mawili na kutoa pasi moja ya goli.
- Ureno wameshinda changamoto za mikwaju ya penati kwenye mechi tatu kati ya nne kwenye michuano mbalimbali. Hakuna timu iliyowahi kushinda mara mbili mfululizo changamoto za mikwaju ya penati katika historia ya mashindano haya.
- Wales wamefunga magoli 10 kwenye michuano ya Euro mwaka huu. Timu pekee ya Uingereza kufunga zaidi yao ilikuwa ni England ambao walifunga magoli 11 kwenye Kombe la Dunia mwaka 1966.
- Ni ufaransa pekee ndio wenye safu bora ya ushambuliaji zaidi ya Wales kwenye michuano hii. Wamefunga magoli 11.
- Wales ndio timu ya kwanza kufika hatia ya nusu fainali ya Michuano ya Ulaya ikiwa kama timu iliyoshiriki kwa mara ya kwanza tangu kwa mara ya mwisho walivyofanya Sweden mwaka 1992
- Hii ni mara ya kwanza kwa Wales kufika hatua ya nusu fainali katika michuano iliyoandaliwa na ama Uefa au Fifa kwa level yoyote iwe wanaume au wanawake.
- Hal Robson-Kanu amefunga magoli mawili kutokana na mashuti matatu yaliyolenga lango kwenye michuano ya mwaka huu.
- Aaron Ramsey, ambaye anakosa mchezo wa leo kutokana na kutumikia adhabu yake ya kadi mbili za njano, amefunga au kutoa pasi ya goli kwenye magoli nane ya mwisho kufungwa na Wale (ukiondoa goli la kujifunga)
- Gareth Bale amepiga mashuti 14 yaliyolenga lango kwenye michuano ya mwaka huu, zaidi ya mchezaji yeyote kwenye michuano hii.