Kumekuwa
na taarifa za upotoshaji kuhusu uratibu na ushiriki wa klabu za
Tanzania katika mashindano ya kimataifa hususani ushiriki wa Young
Africans SC katika mashindano ya Kombe la Shirikisho kwa msimu wa
2015/2016.
Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), limekuwa likitoa kila aina ya msaasa
uliowezekana kuisaidia klabu za Young Africans na Azam ambazo
ziliwakilisha nchi katika mashindanmo ya kimataifa. Kwa upande wa Young
Africans awali walishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na upande wa Azam
ilishiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Mtakumbuka,
Azam FC ilitolewa na Esperance ya Tunisia katika michuano hiyo na kwa
upande wa Young Africans iliposhindwa kufuzu kwa hatua ya Nane Bora ya
Ligi ya Mabingwa Afrika, ikashushwa na kucheza na Esperanca Sagrada ya
Angola na kuitoa hivyo kufuzu kwa hatua ya Nane Bora ya Kombe la
Shirikisho au kwa lugha nyingine, hatua ya Makundi. TFF ikaendelea
kuisaidia Young Africans kuhakikisha inashiriki vema katika mashindano
hayo.
Sasa,
Aprili 21, 2016 Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilitoa waraka kwa timu
zilizokuwa zinacheza kuwania kuingia hatua ya Makundi (Ligi ya Mabingwa
Afrika na Kombe la Shirikisho) kupeleka majina ya maofisa
watakaohudhuria warsha ya namna ya kuratibu mechi hizo kuelekea fainali.
Kadhalika walitakiwa kupeleka vivuli (photocopies) vya hati zao za
kusafiria.
Maofisa
walihitajika ni meneja wa timu, daktari wa timu na ofisa habari wa
timu. Taarifa hiyo ilikuja kabla ya Young Africans kucheza na Esperanca
ya Angola. TFF iliwaataarifu Young Africans kwa kuwataka kutuma nyaraka
hizo kati ya Aprili 26 na Aprili 28, 2016.
Lengo
la warsha ilikuwa ni kujadili maswala ya uratibu, ufundi, udhamini na
kanuni za mashindano. CAF ilijitolea kugharamia usafiri, malazi na
gharama zote kwa watu watatu kutoka Young Africans SC.
Taarifa
hizi na hata ukumbusho (reminders) zilipelekwa kwa baruapepe, simu na
hata kuonana ana kwa ana kwa Katibu Mkuu wa Young Africans, Ofisa Habari
na Viongozi wengine wa klabu.
Maofisa
wa TFF kwa nyakati tofauti tofauti waliwasihi Young Africans na pia
kuwakumbusha kutuma majina CAF na vivuli vya hati hati ya kusafiria,
lakini kwa sababu wanazoweza kuzielezea wenyewe kwa nini hawakupeleka
majina.
Mei
22, 2016 ikiwa ni siku mbili kabla ya warsha kuanza hapo Mei 24, 2016,
Kaimu Katibu Mkuu wa Young Africans, Bwana Baraka Deusdedit alituma
majina CAF yakiwa hayana vivuli yaani photocopies vya hati ya kusafiria.
Siku
moja kabla ya washiriki kuanza kuwasili Cairo, Misri, Kaimu Katibu Mkuu
wa Young Africans alituma nyaraka kama zilivyotakiwa na wakatumiwa
tiketi tatu (3) na CAF. Pamoja na tiketi kuletwa Young Africans bado
watu hao hawakusafiri wakidai klabu haijatoa ruhusa.
Maofisa
wa TFF wamekuwa wakifanya kazi mpaka muda wa ziada wakiwa na Kaimu
Katibu Mkuu wa Young Africans, Baraka Deusdedit ili timu iweze kushiriki
vema pamoja na upungufu wa kiutawala ndani ya sekretarieti yake
yanayojidhihirisha wazi.
Masuala yote yanayolalamikiwa na Ofisa Habari wa Young Africans, yaliyotolewa kwa timu zote kwenye semina ya Cairo, Misri.
TFF
itaendelea kuvitembelea kusaidia klabu kujenga weledi kupitia mradi wa
leseni za klabu na vilevile kuratibu ushiriki wa mashindano mbalimbali.
Hata
hivyo, TFF haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa maofisa wa klabu
wanaochafua jina la shirikisho ili kuficha madhaifu yao ya kiutawala
(Administrative inefficiencies).