Friday, May 5, 2017
TFF, WILDAID WASAINI MAKUBALIANO KUPIGA VITA UJANGILI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Taasisi ya kupigania uhai wa maisha
ya wanyama wa mbugani ya Wildaid Alhamisi Mei 4, mwaka huu kwa pamoja
wamesaini makubaliano ya vita dhidi ya ujangili.
Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam kati ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Mwakilishi wa taasisi hiyo, Lily Massa.
Akizungumza
kabla ya kusaini makubaliano hayo, Rais wa TFF Jamal Malinzi alisema
kwamba, “Hii ni sehemu nyingine ya TFF kujihusisha na shughuli za
kijamii licha ya kuwa na majukumu ya kusimamia maendeleo ya mpira wa
miguu katika kukuza na kuendesha mashindano.”
Malinzi
amesema TFF inaendeleza utamaduni wa shughuli mbalimbali za jamii kwani
hata kwa Rais wa Heshima wa TFF, Leodegar Tenga enzi za utawala wake
akiwa kiongozi mkuu wa mpira wa miguu, alifanya hivyo katika kampeni za
kupinga maambukizi mapya ya UKIMWI.
“Wengi
mtakumbuka kuwa kulikuwa pia na vita vya kupigania afya za watoto na
kupigania uhai wao pia kampeni za amani ambazo mpira wa miguu umetumika
kuelimisha,” amesema.
Kwa
hatua hii ya sasa, Rais Malinzi amesema kwamba TFF, inaingia
makubaliano hayo na kuiteua timu ya taifa ya vijana Tanzania maarufu
kama Serengeti Boys kusimama kidete kupinga uwindaji haramu wa wanyama
mbugani kwa kuwa ni hazina kubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa
upande wa Mwakilishi wa WildAid, Lily Massa, alishukuru kuingia kwa
makubalino hayo akisema kwamba ndoto zao za kupiga vita uwindaji haramu
na ujangili, itafanikiwa.
“Tunashukuru
kuingia programu hii na ninaamini Mungu atatusaidia,” amesema Massa
ambaye taasisi yake iko karibu kila nchi yenye wanyama wa mbugani.
Katika
hatua nyingine, Rais Malinzi aliitakia kila la kheri Serengeti Boys
ambayo kwa sasa inajiandaa kuingia Gabon kwa ajili ya fainali za Kombe
la Mataifa ya Afrika. Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Mei 14, mwaka huu
ambako Serengeti Boys ambayo iko Kundi B itakuwa Libreville - Mji Mkuu
wa Gabon. Timu nyingine za Kundi B ni Mali, Niger na Angola.
ABDULRAHMAN MUSSA MCHEZAJI BORA WA VPL MWEZI APRILI
Mchezaji
wa timu ya Ruvu Shooting FC, Abdulrahman Mussa amechaguliwa kuwa
mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa mwezi Aprili kwa msimu wa
2016/2017.
Abdulrahman aliwashinda wachezaji Jafar Salum wa Mtibwa Sugar FC na Zahoro Pazi wa Mbeya City.
Katika
mwezi wa Aprili kulikuwa na raundi tatu na timu ya Ruvu Shooting
ilicheza michezo miwili ambayo Abdulrahman alicheza dakika zote 180 na
kufunga magoli manne(4) kati ya matano yaliyofungwa na timu yake na
hivyo kuifanya timu yake kufikia nafasi ya tisa(9) kutoka nafasi ya
kumi(10) katika msimamo wa Ligi ya Vodacom.
Abdulrahman
alifunga Hat Trick (magoli matatu) katika mchezo wa Ruvu Shooting dhidi
ya Majimaji uliofanyika katika uwanja wa mabatini Mlandizi.
Kwa kushinda tuzo hiyo, Abdulrahman Mussa atazawadiwa kitita cha sh. milioni moja (1,000,000/) kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom Tanzania.
Lebron Aendelea Kujimilikisha NBA, Amwacha Kareem Abdul Jabbar
Naam, kuna mchezaji mmoja pekee mpaka sasa ambaye amefunga alama nyingi kwenye hatua za mtoano za NBA kuliko LeBron James mpaka kufikia Alfajiri ya leo Alhamis naye ni zimwi analolikimbiza Lebron James, neno alilonukuliwa kipindi akijaribu kumuelezea mchezaji bora wa muda wote wa NBA kwenye macho ya wengi, Michael Jordan.
James alimpita mchezaji nguli wa zamani wa klabu ya Los Angeles Lakers, Kareem Abdul-Jabbar (alama 5,762 ) na kukwea nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa hatua ya mtoano pale alipofunga alama yake ya 25 kwenye mchezo wa pili wa hatua ya nusu fainali ya kanda ya Mashariki kati ya Cleveland Cavaliers na Toronto Raptors.
James alipata mtupo wa pointi 3 katika dakika ya 8:41kwenye robo ya tatu na kuwafanya Cleveland kuongoza kwa alama 75-59 na yeye kufikisha alama 27. Alimaliza mchezo huo akiwa na alama 39 huku klabu yake ya Cavs’ ikiibuka na ushindi wa alama 125-103.
Michael Jordan anaongoza orodha ya wafungaji kwenye hatua ya mtoano ya NBA akiwa na alama 5,987. James anaweza kumpita iwapo Cavs watacheza michezo mingi zaidi kwenye hatua hii, wakiwa wanapigania kuingia fainali mara ya 3 mfululizo huku ikiwa mara ya 7 mfululizo kwa Lebron James.
Nyota huyo wa Cavs ameendelea kuwa na msimu bora hasa hatua ya mtoano hii akiwa na wastani wa alama 33.2, Rebound 9.8 na assist 8.0 huku katika hatua ya michezo ya ligi akiwa na wastani wa alama 26.4 , 8.6 rebounds, 8.7 assists, 0.6 blocks na kupokonya mipira mara 1.2 kwa mchezo.
“Najihisi nipo vyema,” alisema, “nimebarikiwa tu kuweza kufanya maamuzi mazuri ya mchezo wa leo kiasi cha kuisaidia timu yangu kushinda.”
James amefikia alama hizi kwenye hatua za mtoano ukiwa ni mchezo wake wa 205. Abdul-Jabbar alicheza michezo 237. Lakini hata hivyo James amecheza katika mfumo ambao unaruhusu kucheza michezo mingi kwenye hatua ya mtoano baada ya hatua ya kwanza ya mtoano kupanuliwa nao kuwa na michezo 7 ya mtoano mwaka 2003, msimu mmoja kabla hajaingia kwenye ligi.
James, akiwa na mwaka wake wa 14 kwenye ligi yupo katika nafasi ya 7 kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa NBA akiwa na alama 28,787. Abdul-Jabbar, ambaye alicheza misimu 18 ni wa kwanza akiwa na alama 38,387.
James alikuwa mchezaji wa nne pia kuweza kupata mitupo 300 ya pointi 3 na sasa anaungana na wachezaji kama Ray Allen (385), Reggie Miller (320) na Manu Ginobili (312).
James pia yupo katika nafasi ya tatu kwa wachezaji waliotoa assist nyingi kwenye hatua ya mtoano akiwa nyuma ya wachezaji Magic Johnson na John Stockton. Yupo pia katika nafasi ya tatu kwenye kupokonya mipira nyuma ya Scottie Pippen na Jordan.
Sababu ya Liuzio kuwekwa benchi na Omog
STRAIKA anayecheza kwa mkopo ndani ya kikosi cha Simba, Juma Liuzio ametoa sababu za kukosa namba ndani ya timu hiyo kwa siku za hivi karibuni.
Liuzio ambaye alijiunga na Simba kwa mkopo kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu akitokea Zesco ya Zambia amesema, mabadiliko ya mfumo wa Kocha wa timu hiyo Joseph Omog ndiyo unasababisha hayo yote.
“Mfumo wa Mwalimu umekuwa na tatizo kwangu ndiyo maana siku hizi anamuanzisha Fredrick Blagnon kwa lengo la kutumia mpira ya juu ambapo Blagnon ameonekana kuimudu vizuri kuliko mimi,” amesema Liuzio.
Aidha, mshambuliaji huyo amekuwa akiwaombea mbaya wapinzani wao (Yanga) katika mechi zao zilizosalia.
“Yanga wanaweza kupata sare katika mechi tatu ambazo ni Mbao FC, Kagera Sugar ,Mbeya City na pia wanaweza kufanya vibaya, lakini adui yako muombee njaa tu.”
Simba inaendelea na Mazoezi yake katika Uwanja wa chuo cha polisi Kurasini kujiaanda na mchezo wao mkali dhidi ya African Lyon Jumapili hii katika uwanja wa taifa.
Ahadi ya Kichuya kuelekea fainali ya FA
“TUTAWAPIGA TU,” hayo ni maneno ya Kiungo Mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya, ametamba kuifungia timu yake bao muhimu kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Azam Sports Federation dhidi ya Mbao FC.
Simba ilipata tiketi ya kuingia fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), baada ya kuichapa Azam bao 1-0, katika mchezo uliochezwa Jumamosi iliyopita kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kichuya amesema amejipanga kucheza kwa kujituma kwasababu hiyo ndiyo itakuwa shukrani yake pekee kwa timu yake na kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ili waweze kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
“Nitafurahi sana kama nitafunga bao na kuipa ubingwa wa FA timu yangu, kwa sababu tumekuwa na msimu mzuri lakini mwisho umeonekana mgumu kutokana kila timu ambayo tunapambana nayo inakuwa inatupania kusababisha kupata matokeo ambayo hayaturidhishi,” amesema Kichuya.
Amesema kwa sasa yupo fiti na kiwango chake kimezidi kupanda siku hadi siku hivyo anauhakika wa kupata nafasi kwenye kikosi kitakachoanza mchezo huo na yupo tayari kujitoa kwa ajili ya timu yake.
Kichuya amesema amecheza na Mbao mara mbili na amewajua vizuri mapungufu yao hivyo atahakikisha anayatumia kwa kuwafunga ili kuisaidia timu yake kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Amesema hakuna linaloshindikana ingawa Mbao ni timu ngumu na iliwasumbua kwenye mechi zote mbili walizocheza kabla ya mchezo huo wa fainali lakini wamejipanga kucheza kufa na kupona ili kutwaa taji hilo.
“Fainali hii ni muhimu sana kwetu na tutahakikisha tutawapa raha wapenzi wetu kwa kuchukua kombe hilo, hivyo nitapambana kuhakikisha timu yangu inashinda na kila mchezaji analijua hilo hivyo hatutafanya mzaha kila mmoja atacheza kwa kujituma akijua fika nini tunachotakiwa kufanya,” alisema
Kichuya mwenye mabao 10 kwenye ligi ya Vodacom, anatarajiwa kuibeba timu yake kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Mbao ambao umepangwa kupigwa Mei 28 kwenye uwanja Jamuhuri uliopo Mkoani Dodoma.
Mimi ni shabiki wa ‘kutupwa’ wa Arsenal’ – Pro. Lipumba
“Arsenal haifanyi vizuri, lakini ndio timu yangu ninayoipenda,” Prof. Lipumba amesema kwenye kipindi cha Clouds 360 cha Clouds TV leo Alhamisi Mei 4, 2017 wakati akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali yanayohusiana na chama chao (CUF).
Lipumba pia amesema yeye amewahi kucheza soka wakati akiwa mwanafunzi wa shule ya sekondari japo haikua kwa kiwango cha ushindani.
“Nimewahi kucheza mpira wakati nasoma sekondari, lakini sio katika ngazi ya ushindani,” amesema Pro. Lipumba.
Subscribe to:
Posts (Atom)