Taarifa kutoka nchini Ubelgiji zinasema kwamba, mchezaji wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga kwenye klabu ya TP Mazembe ya nchini Congo DR Mbwana Samatta muda wowote anaweza kujiunga na klabu ya Genk inayoshiriki ligi kuu nchini Ubelgiji (Belgian Pro League).
Kwa muda mrefu sana kulikuwa na harakati za Mbwana Samatta kujiunga na vilabu vya Ulaya, klabu ya Genk ya Ubelgiji kwa asilimia nyingi ipo kwenye dakika za mwisho kukamilisha deal la kumsajili Mbwana Samatta kutoka TP Mazembe.
Genk ipo nafasi ya sita (6) kwenye msimamo wa ligi kuu ya soka nchini Ubelgiji ikiwa imecheza michezo 20 na kufanikiwa kukusanya jumla ya pointi 28 hadi sasa.
Moise Katumbi ambaye alikuwa anaonekana kama kikwazo yupo Ubelgiji na jana alikuwa anafanya mazungumzo na timu ya Genk na kufikia makubaliano ambapo na yeye pia amekubali kumruhusu Mbwana Samatta.
Dirisha dogo la usajili kwa vilabu vya Ulaya litakapofunguliwa mwezi January Samatta atatua Belgium kujiunga na klabu hiyo.
Samatta amebakiza mkataba wa miezi minne pekee kuendelea kusalia kwenye klabu yake ya TP Mazembe ambayo msimu huu ameisaidia kutwaa kombe la klabu bingwa Afrika.