Sasa
ni siku chache tu baada ya Yanga kufanikiwa kumsajili, Obrey Chirwa
raia wa Zambia, mpachika mabao wa timu hiyo, raia wa Burundi, Amissi
Tambwe, amedai kuwa hana wasiwasi na ujio wa nyota huyo kikosini hapo.
Yanga imemleta Chirwa kutoka FC Platinum ya Zimbabwe ili kuimarisha safu yake ya ushambuliaji.
Tambwe
ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita baada ya kupiga
mabao 21, amesema anajiamini na ana uhakika wa kubakia katika kikosi
cha kwanza cha Yanga endapo kocha mkuu wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van
Der Pluijm atapenda.
“Sina
wasiwasi na nafasi yangu kwani najiamini na Mungu akipenda nitaendelea
kuwa kikosi cha kwanza na nitazidi kufanya vizuri kama ilivyokuwa msimu
uliopita.
“Naongea
hivyo kwa sababu najiamini na ninajua nini ninachokifanya, kwa hiyo
sihofii mchezaji yeyote ila nawapongeza Yanga kwa usajili wa Chirwa
kwani tunachotaka sisi ni mafanikio, hivyo nitashirikiana naye kwa kila
jambo kama nilivyokuwa nikishirikiana na (Donald) Ngoma,” alisema
Tambwe.