Monday, July 4, 2016

ANGBAN NAYE KUMBE SI SIRIAZ, SIKIA HII ALIVYOCHELEWA NDEGE



Kipa namba moja wa Simba, Vincent Angban raia wa Ivory Coast, alishindwa kutua nchini usiku wa kuamkia jana kutokana na kuchelewa ndege alipokuwa akitokea nchini kwao.
Angban alitarajia kutua akiambatana na mshambuliaji mpya wa timu hiyo raia wa Ivory Coast, Blagnon Goue Fredric alishindwa kufanya hivyo huku Fredric ambaye alikuwa akiitumikia Klabu ya African Sports ya Ivory Coast akiwasili peke yake juzi usiku kisha akitarajiwa kufanya mazungumzo ya usajili kumalizana na uongozi wa Simba, jana Jumapili.
Habari za kuamnika kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa kutokana na hali hiyo Angban anatarajia kutua nchini usiku wa kuamkia leo tayari kwa kuanza maandalizi yake kwa ajili ya msimu ujao.
“Mshambuliaji wetu mpya ambaye tunatarajia kumsajili hivi karibuni ambaye ni raia wa Ivory Coast tayari ameshatua na sasa yupo katika mazungumzo ya mwishomwisho na uongozi.
“Alikua aje na Angban ambaye alikwama kutokana na kuchelewa ndege, baada ya kuchelewa akaomba uongozi umuongezee fedha ile ambayo huwa inaongezwa inapotokea msafiri amechelewa ndege, uongozi ulikataa an ameongeza mwenyewe kwa kuwa ni uzembe wake,” kilisema chanzo kutoka Simba.

MAYANJA YUKO JIJINI DAR ES SALAAM NA HAYA NDIYO MANENO YAKE KUHUSIANA NA JOSEPH OMOG



Kocha Mganda, Jackson Mayanja aliyeelezwa kuwa mbioni kuachana na Simba kutokana na sababu mbalimbali, ametua jijini Dar, juzi usiku na kufunguka kuhusiana na kocha mkuu mpya wa timu hiyo, Joseph Omog.
Mayanja ambaye ametua nchini akitokea Uganda alikokwenda kwa ajili ya mapumziko mara baada ya kumalizika kwa ligi msimu uliopita, hivi karibuni kuliibuka taarifa zilizodai kuwa hayupo tayari kufanya kazi chini ya Omog lakini amekanusha hilo.
“Kama nikielewana na Simba nitafanya kazi tu chini ya Omog kwa kuwa nafahamu majukumu yangu kama kocha msaidizi,” alisema Mayanja.
Awali kulikuwa na taarifa kuwa Mayanja anaweza kutua katika timu yake ya zamani ya Kagera Sugar au Mwadui FC, ambapo yeye mwenyewe amekiri kufanya mazungumzo na klabu hizo kwa kuwa mkataba wake na Simba ulimalizika.
“Kweli Kagera na Mwadui wananihitaji, hata Kiyovu SC ya Rwanda pia lakini nipo Dar kwa kuwa nimetumiwa tiketi na Simba. Hivyo, nitawasikiliza Simba kwanza baada ya hapo ndiyo kitakachofuata,” alisema kocha huyo.
Taarifa za ndani ya Simba zinaeleza kuwa Mayanja alitarajiwa kukutana na Omog, jana kwa ajili ya mazungumzo.

Akiwa kocha wa muda wa Simba, Mayanja aliiongoza Simba katika mechi 16 za Ligi Kuu Bara na kushinda 11, sare moja na kupoteza nne dhidi ya Yanga, Mwadui, Toto African na JKT Ruvu.

KAZI IPO, YANGA WATAMBA WAKIMALIZANA NA TSHABALALA NDIYO MWISHO WA USAJILI WAO



Uongozi wa Klabu ya Yanga umesema bado upo katika harakati za kuhakikisha unamnasa beki wa kushoto wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kwa kuwa ndiyo chaguo lao.

Tshabalala ambaye msimu ujao atatambulika kama Zimbwe Jr, alitua Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Kagera Sugar ambapo kwa sasa amekuwa lulu ndani ya timu hiyo kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa.
Mmoja wa mabosi wa Yanga amesema kuwa wapo katika harakati za kuhakikisha wanamnasa beki huyo kwa ajili ya kuleta changamoto kwa Mwinyi Haji na Oscar Joshua kutokana na viwango vyao kuonekana kupwaya.
Bosi huyo alisema kwa upande wao nafasi iliyobaki katika usajili wa msimu huu ni beki wa kushoto na kiungo mmoja ambao wataweza kuwasaidia katika ligi na mashindano ya kimataifa.
“Tunataka beki wa kushoto na chaguo letu ni Tshabalala wa Simba, huyo ndiyo atakuwa mtu sahihi wa kuweza kutoa changamoto kwa (Oscar) Joshua na (Haji) Mwinyi.
“Unajua tatizo halipo kwa mchezaji kwa sababu tumeshakutana naye zaidi ya mara nne na ameonyesha kukubali isipokuwa Simba ndiyo wanaonekana kuwa ni wagumu kwa kuwa bado wanamkataba naye wa mwaka mmoja,” alisema bosi huyo.
Alipotafutwa  Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Murro alisema kuwa kwa sasa hawezi kuliongelea suala hilo kwa kuwa bado halijafika mezani kwake.

Ikumbukwe kuwa, hivi karibuni uongozi wa Simba uliwahi kusema hauna mpango wa kumuuza mchezaji huyo kutokana na kuwa ni msaada mkubwa ndani ya timu hiyo.

SOURCE: CHAMPIONI

KICHUYA ANA UHAKIKA KABISA, ATATUA SIMBA MAANA NDIYO ANAPOPATAKA



Kiungo myumbulikaji wa Mtibwa Sugar, Shiza Kichuya anayewaniwa na Simba amefunguka kuwa vimesalia vitu vichache kwa ajili ya kuvaa uzi mwekundu msimu ujao kwa ajili ya kuitumikia Simba.
Kichuya, mchezaji anayesifika kwa mashuti, nguvu na uwezo wa kumiliki mpira, alianza kuhusishwa kuhamia Simba mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara, hivi karibuni amefunguka kuwa kwa upande wake tayari ameshamaliza kila kitu na kilichobaki sasa ni uongozi wa Mtibwa kumalizana na Simba.
Aidha, alisema kwamba kwa kuwa bado yupo kwenye mkataba na Mtibwa, kila kitu sasa kimehamia kwa Mkurugenzi wa Mtibwa, Jamal Bayser na yeye ndiye anayefanya mazungumzo ya mwisho na mabosi wa Simba kabla ya kupewa taarifa ya maafikiano ya kumwaga saini.
“Siwezi kulizungumzia kwa undani hili suala lakini niseme tu kwamba kwa upande wangu nishamaliza kila kitu na nimepewa taarifa tu kwamba hata kwa upande wa viongozi wa Mtibwa na Simba nao wamefikia pazuri, kwa hiyo nasubiri taarifa ya mwisho.
“Kimsingi ieleweke kwamba mpira ni ajira yangu na kokote nafanya kazi, kama nitafanikiwa kutua Simba itakuwa safi pia maana popote nitakapokwenda nitapiga mzigo kama kawaida,” alisema Kichuya anayetajwa kuwa moja ya wachezaji walioonyesha kiwango cha juu msimu uliopita.
Kichuya anakumbukwa pia kwa kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi katika Ligi Kuu Bara kwa mwezi Machi katika msimu uliopita ambapo uwezo wake ulimwezesha pia kuitwa katika timu ya taifa kwa mara ya kwanza chini ya Kocha wa Taifa Stars, Charles Mkwasa kwa ajili ya mechi dhidi ya Chad iliyofanyika Machi 23, 2016, jijini N'Djamena.
Kuhusiana na hilo, Bayser alisema: “Tunasikia Simba wanamtaka lakini sisi pia tumepanga kumbakisha kikosini kwetu lakini akikataa hatutakuwa na namna, tutamuacha aende kwani hayo yatakuwa maamuzi yake mwenyewe.”

-------------------------------------------------------

-------------------------------------------------------
HABARI MPYAMPYAhttp://2.bp.blogspot.com/-mFnDPXvIysA/VOZH1z-2rpI/AAAAAAAAADs/shOR30FtkF4/s1600/anigif.gif