MSIMU
uliopita, kikosi cha Ndanda FC kilinusurika kuteremka daraja hadi la
kwanza “kimkandamkanda” kwa kuwa mambo yalikuwa mabaya kupita kiasi.
Licha
ya kuwa kati ya timu zinazoonekana zinakwenda kuteremka daraja. Ndanda
FC ndiyo ilikuwa timu ambayo imepoteza mwelekeo zaidi baada ya uongozi
wake kuonekana umepotea njia.
Kibaya
zaidi, wachezaji wake wengi nao walionekana wamepotea na wamekata tamaa
na hata kufikia kulalamika kwenye vyombo vya habari.
Baadhi
ya mambo waliyolalamika ni kukosa hata fedha kwa ajili ya mlo. Yaani
walikuwa kambini na walikuwa wakishinda njaa, kitu ambacho ni kibaya
zaidi cha mwisho unapozungumzia kundi la wanadamu.
Mnaweza
kukosa jambo jingine lakini si chakula ambayo ni huduma namba moja kwa
mwanadamu. Lakini wachezaji hao walisema nafuu yao ilikuwa ni mlo mmoja
kwa siku, jambo ambalo si zuri hata kulisikia na sikuwahi kusikia
kiongozi wa Ndanda FC akilikanusha.
Waliokuwa
wakilalamika ni kati ya wachezaji wakongwe kabisa wa Ndanda FC na hata
watu wa benchi la ufundi. Hili halikuwa jambo zuri lakini hongera kwao
kwa kuwa walijitutumua na mwisho Ndanda FC ikabaki Ligi Kuu Bara.
Baada
ya hapo, nilitegemea kuona wanajipanga. Ingawa jambo hilo halikufanyika
mapema sana kwa kuwa inaonyesha hata usajili wa Ndanda FC haukuwa ule
unaoonyesha kuna mabadiliko makubwa.
Huenda
uongozi haukuwa na fedha na mipango haikuwa bora kuhakikisha fedha
nyingi zinapatikana. Lakini baada ya dirisha la usajili kufungwa,
nimeona kuna Kampuni Motsun Group Ltd kupitia ya bidhaa yake ya mabati
ya Kiboko imejitokeza kuidhamini Ndanda FC.
Ndanda
FC wamepata udhamini wa mwaka mmoja kuitangaza Kiboko. Hawakusema kiasi
gani lakini tayari wameongeza kitu mfukoni mwao ambacho kitawasaidia
kuwa tofauti na awali.
Lakini
lazima ukumbuke kuwa Ndanda FC wanaingiza fedha kupitia wadhamini wa
Ligi Kuu Bara, Vodacom pia Azam TV ambazo zinaweza zisiwe nyingi sana
lakini zinasaidia gharama kadhaa za uendeshaji tofauti na zamani.
Msimu
uliopita pia walipokea fedha kutoka Vodacom na Azam TV lakini
wakashindwa kusimama na kufanya vizuri. Ujio wa Kiboko ni jambo jingine
bora wanalopaswa kulitumia kama chachu ya mabadiliko.
Ninaamini
Kiboko wangeweza kutodhamini katika soka na kwenda kwingine
kujitangaza. Uamuzi wao kuingia kwenye soka lazima wapate faida na
mafanikio yao na ikiwezekana wanaongeza mkataba ni kuona Ndanda FC
inafanya vizuri.
Ndanda
FC wasifurahie fedha tu wanazopata, badala yake wanapaswa kujua kwamba
wadhamini wao pia kuna jambo wanategemea kutoka kwao na wakifurahia
zaidi basi wataweza kuendelea na udhamini na ikiwezekana kuongeza zaidi,
hili ninaamini linaweza kutokea.
Lakini
anayeweza kulifanya litokee, ni Ndanda wenyewe ukianza na viongozi na
wachezaji pia. Wanaposaidia lazima wajue wana deni la kumtangaza
mdhamini wakiwa na mafanikio na ikiwezekana suala la nidhamu linapaswa
kuwa juu zaidi ukilinganisha na msimu uliopita.
Kesho
kama Ndanda FC itateremka daraja, maana yake watakuwa pia wamemshusha
mdhamini wao kwa maana ya kwamba hatakuwa na nafasi ya kuongeza mkataba
tena. Lakini wakifanya vema na ikiwezekana kufikia angalau ule uwezo
waliouonyesha Mbao FC ya Mwanza msimu uliopita, huenda hata wadhamini
wenye donge nono wanaweza kujitokeza zaidi.
Ndanda
FC mna deni kubwa la kuonyesha tofauti kwa kuwa mwanadamu bora ni yule
anayejifunza kupitia makosa yake. Kama msimu unaoanza wiki chache zijazo
utaendelea kuwa wa shida kwenu, basi lawama zibaki kwenu na mtaonyesha
ni watu wa kubahatisha mambo.
Fanyeni
vizuri ili muwe sehemu ya kuwashawishi wadhamini wengine kwamba hata
timu ndogo zinaweza kudhaminiwa na kuwatangaza vizuri wadhamini.