“TUTAWAPIGA TU,” hayo ni maneno ya Kiungo Mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya, ametamba kuifungia timu yake bao muhimu kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Azam Sports Federation dhidi ya Mbao FC.
Simba ilipata tiketi ya kuingia fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), baada ya kuichapa Azam bao 1-0, katika mchezo uliochezwa Jumamosi iliyopita kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kichuya amesema amejipanga kucheza kwa kujituma kwasababu hiyo ndiyo itakuwa shukrani yake pekee kwa timu yake na kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ili waweze kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
“Nitafurahi sana kama nitafunga bao na kuipa ubingwa wa FA timu yangu, kwa sababu tumekuwa na msimu mzuri lakini mwisho umeonekana mgumu kutokana kila timu ambayo tunapambana nayo inakuwa inatupania kusababisha kupata matokeo ambayo hayaturidhishi,” amesema Kichuya.
Amesema kwa sasa yupo fiti na kiwango chake kimezidi kupanda siku hadi siku hivyo anauhakika wa kupata nafasi kwenye kikosi kitakachoanza mchezo huo na yupo tayari kujitoa kwa ajili ya timu yake.
Kichuya amesema amecheza na Mbao mara mbili na amewajua vizuri mapungufu yao hivyo atahakikisha anayatumia kwa kuwafunga ili kuisaidia timu yake kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Amesema hakuna linaloshindikana ingawa Mbao ni timu ngumu na iliwasumbua kwenye mechi zote mbili walizocheza kabla ya mchezo huo wa fainali lakini wamejipanga kucheza kufa na kupona ili kutwaa taji hilo.
“Fainali hii ni muhimu sana kwetu na tutahakikisha tutawapa raha wapenzi wetu kwa kuchukua kombe hilo, hivyo nitapambana kuhakikisha timu yangu inashinda na kila mchezaji analijua hilo hivyo hatutafanya mzaha kila mmoja atacheza kwa kujituma akijua fika nini tunachotakiwa kufanya,” alisema
Kichuya mwenye mabao 10 kwenye ligi ya Vodacom, anatarajiwa kuibeba timu yake kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Mbao ambao umepangwa kupigwa Mei 28 kwenye uwanja Jamuhuri uliopo Mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment