WAKATI Bosi wa Chelsea Jose Mourinho akiisifia Timu yake kuwa ni kubwa na imara baada kuponea chupuchupu huko Paris walipotoka 1-1 na
Paris St-Germain katika Mechi ya Kwanza ya Raundi ya Mtoano ya Timu 16 ya UEFA CHAMPIONZ LIGI Jumanne Usiku, baadhi ya Wachambuzi huko England wamemponda Meneja huyo.
Licha ya kukiri Chelsea ilibahatika kupata Sare na PSG, Mourinho aliisifia na kuisema Timu yake ni kubwa na imara: “Kazi ngumu ni kuijenga Timu kubwa na imara na sisi ni Timu kubwa na imara. Lakini haya ni mambo yasiyotabirika ya Soka!”
Hata hivyo Wachambuzi wamempinga Mourinho kwa msimamo huo, na hasa Roy Keane, Nahodha wa zamani wa Manchester United, ambae alitamka: “Nadhani wanao uwezo wa kuwa Timu kubwa na imara. Ni wazi yeye ni Meneja mkubwa na bora lakini kuwa Timu kubwa na imara ni kutwaa Mataji. Kusema hilo sasa ni upuuzi!”
Jumanne Usiku, ndani ya Parc des Princes Jijini Paris, Chelsea walitangulia kwa Bao la Branislav Ivanovic lakini Edinson Cavani akaisawazishia PSG na kama si uhodari wa Kipa Thibaut Courtois basi PSG wangeondoka na lundo la Magoli.
Mourinho alizungumza: “Ukiona umahiri wa Kipa wetu basi utakiri tumebahatika kutofungwa!”
Lakini matokeo hayo ni bora kuliko Msimu uliopita kwenye Robo Fainali ya Mashindano haya haya walipokung’utwa 3-1 na PSG ndani ya Parc des Princes na Chelsea kushinda Mechi ya Pili huko Stamford Bridge 2-0 na Bao hilo la Pili kufungwa Dakika za mwishoni na Demba Ba na kuwapenyeza kwa Ubora wa Goli za Ugenini.
Mourinho amesema: “Hii ni nafasi kwetu. Ni wazi Mechi mbili sasa ni moja. Sasa kila kitu kitaamuliwa Stamford Bridge, si katika Mechi mbili!”
Chelsea na PSG zitarudiana hapo Jumatano Machi 11 na Mshindi kutinga Robo Fainali.
No comments:
Post a Comment