Friday, May 5, 2017

MKWAJU WA RASHFORD ULIOIBEBA MANCHESTER UNITED HUKO HISPANIA HUU HAPA


Marcus Rashford amefunga bao pekee wakati Man United ikishinda kwa bao 1-0 dhidi ya Celta Vigo katika mechi yake ya kwanza ya Kombe la Europa.

Bao hilo la dakika ya 67 limekuwa kivutio kikubwa kutokana na mkwaju wa adhabu mwanafunzi huyo wa sekondari alioupiga na kufunga.

TFF, WILDAID WASAINI MAKUBALIANO KUPIGA VITA UJANGILI





Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Taasisi ya kupigania uhai wa maisha ya wanyama wa mbugani ya Wildaid Alhamisi Mei 4, mwaka huu kwa pamoja wamesaini makubaliano ya vita dhidi ya ujangili.

Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam kati ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Mwakilishi wa taasisi hiyo, Lily Massa.

Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo, Rais wa TFF Jamal Malinzi alisema kwamba, “Hii ni sehemu nyingine ya TFF kujihusisha na shughuli za kijamii licha ya kuwa na majukumu ya kusimamia maendeleo ya mpira wa miguu katika kukuza na kuendesha mashindano.”

Malinzi amesema TFF inaendeleza utamaduni wa shughuli mbalimbali za jamii kwani hata kwa Rais wa Heshima wa TFF, Leodegar Tenga enzi za utawala wake akiwa kiongozi mkuu wa mpira wa miguu, alifanya hivyo katika kampeni za kupinga maambukizi mapya ya UKIMWI.

“Wengi mtakumbuka kuwa kulikuwa pia na vita vya kupigania afya za watoto na kupigania uhai wao pia kampeni za amani ambazo mpira wa miguu umetumika kuelimisha,” amesema.

Kwa hatua hii ya sasa, Rais Malinzi amesema kwamba TFF, inaingia makubaliano hayo na kuiteua timu ya taifa ya vijana Tanzania maarufu kama Serengeti Boys kusimama kidete kupinga uwindaji haramu wa wanyama mbugani kwa kuwa ni hazina kubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wa Mwakilishi wa WildAid, Lily Massa, alishukuru kuingia kwa makubalino hayo akisema kwamba ndoto zao za kupiga vita uwindaji haramu na ujangili, itafanikiwa.

“Tunashukuru kuingia programu hii na ninaamini Mungu atatusaidia,” amesema Massa ambaye taasisi yake iko karibu kila nchi yenye wanyama wa mbugani.


Katika hatua nyingine, Rais Malinzi aliitakia kila la kheri Serengeti Boys ambayo kwa sasa inajiandaa kuingia Gabon kwa ajili ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika. Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Mei 14, mwaka huu ambako Serengeti Boys ambayo iko Kundi B itakuwa Libreville - Mji Mkuu wa Gabon. Timu nyingine za Kundi B ni Mali, Niger na Angola.

ABDULRAHMAN MUSSA MCHEZAJI BORA WA VPL MWEZI APRILI






Mchezaji wa timu ya Ruvu Shooting FC, Abdulrahman Mussa amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa mwezi Aprili kwa msimu wa 2016/2017.

Abdulrahman  aliwashinda wachezaji Jafar Salum wa Mtibwa Sugar  FC na Zahoro Pazi wa Mbeya City.

Katika mwezi wa Aprili kulikuwa na raundi tatu na timu ya Ruvu Shooting ilicheza michezo miwili ambayo Abdulrahman alicheza dakika zote 180 na kufunga magoli manne(4) kati ya matano yaliyofungwa na timu yake na hivyo kuifanya timu yake kufikia nafasi ya tisa(9) kutoka nafasi ya kumi(10) katika msimamo wa Ligi ya Vodacom.

Abdulrahman alifunga Hat Trick (magoli matatu) katika mchezo wa Ruvu Shooting dhidi ya Majimaji uliofanyika katika uwanja wa mabatini Mlandizi.

Kwa kushinda tuzo hiyo, Abdulrahman Mussa  atazawadiwa  kitita cha sh. milioni moja (1,000,000/) kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom Tanzania.

Lebron Aendelea Kujimilikisha NBA, Amwacha Kareem Abdul Jabbar



Naam, kuna mchezaji mmoja pekee mpaka sasa ambaye amefunga  alama nyingi kwenye hatua za mtoano za NBA kuliko LeBron James mpaka kufikia Alfajiri ya leo Alhamis naye ni zimwi analolikimbiza Lebron James, neno alilonukuliwa kipindi akijaribu kumuelezea mchezaji bora wa muda wote wa NBA kwenye macho ya wengi, Michael Jordan.
James alimpita mchezaji nguli wa zamani wa klabu ya Los Angeles Lakers, Kareem Abdul-Jabbar (alama 5,762 ) na kukwea nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa hatua ya mtoano pale alipofunga alama yake ya 25 kwenye mchezo wa pili wa hatua ya nusu fainali ya kanda ya Mashariki kati ya Cleveland Cavaliers na Toronto Raptors.
James alipata mtupo wa pointi 3 katika dakika ya 8:41kwenye robo ya tatu na kuwafanya Cleveland kuongoza kwa alama 75-59 na yeye kufikisha alama 27. Alimaliza mchezo huo akiwa na alama 39 huku klabu yake ya Cavs’ ikiibuka na ushindi wa alama 125-103.

Michael Jordan anaongoza orodha ya wafungaji kwenye hatua ya mtoano ya NBA akiwa na alama 5,987. James anaweza kumpita iwapo Cavs watacheza michezo mingi zaidi kwenye hatua hii, wakiwa wanapigania kuingia fainali mara ya 3 mfululizo huku ikiwa mara ya 7 mfululizo kwa Lebron James.
Nyota huyo wa Cavs ameendelea kuwa na msimu bora hasa hatua ya mtoano hii akiwa na wastani wa alama 33.2, Rebound 9.8 na assist 8.0 huku katika hatua ya michezo ya ligi akiwa na wastani wa alama  26.4 , 8.6 rebounds, 8.7 assists, 0.6 blocks na kupokonya mipira mara 1.2 kwa mchezo.
“Najihisi nipo vyema,” alisema, “nimebarikiwa tu kuweza kufanya maamuzi mazuri ya mchezo wa leo kiasi cha kuisaidia timu yangu kushinda.”
James amefikia alama hizi kwenye hatua za mtoano ukiwa ni mchezo wake wa 205. Abdul-Jabbar alicheza michezo 237. Lakini hata hivyo James amecheza katika mfumo ambao unaruhusu kucheza michezo mingi kwenye hatua ya mtoano baada ya hatua ya kwanza ya mtoano kupanuliwa nao kuwa na michezo 7 ya mtoano mwaka 2003, msimu mmoja kabla hajaingia kwenye ligi.
James, akiwa na mwaka wake wa 14 kwenye ligi yupo katika nafasi ya 7 kwenye orodha ya wafungaji  bora wa muda wote wa NBA akiwa na alama 28,787. Abdul-Jabbar, ambaye alicheza misimu 18 ni wa kwanza akiwa na alama 38,387.
James alikuwa mchezaji wa nne pia kuweza kupata mitupo 300 ya pointi 3 na sasa anaungana na wachezaji kama Ray Allen (385), Reggie Miller (320) na Manu Ginobili (312).
James pia yupo katika nafasi ya tatu kwa wachezaji waliotoa assist nyingi kwenye hatua ya mtoano akiwa nyuma ya wachezaji Magic Johnson na John Stockton. Yupo pia katika nafasi ya tatu kwenye kupokonya mipira nyuma ya Scottie Pippen na Jordan.

Sababu ya Liuzio kuwekwa benchi na Omog




STRAIKA anayecheza kwa mkopo ndani ya kikosi cha Simba, Juma Liuzio ametoa sababu za kukosa namba ndani ya timu hiyo kwa siku za hivi karibuni.
Liuzio ambaye alijiunga na Simba kwa mkopo kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu akitokea Zesco ya Zambia amesema, mabadiliko ya mfumo wa Kocha wa timu hiyo Joseph Omog ndiyo unasababisha hayo yote.
“Mfumo wa Mwalimu umekuwa na tatizo kwangu ndiyo maana siku hizi anamuanzisha Fredrick Blagnon kwa lengo la kutumia mpira ya juu ambapo Blagnon ameonekana kuimudu vizuri kuliko mimi,” amesema Liuzio.
Aidha, mshambuliaji huyo amekuwa akiwaombea mbaya wapinzani wao (Yanga) katika mechi zao zilizosalia.
“Yanga wanaweza kupata sare katika mechi tatu ambazo ni Mbao FC, Kagera Sugar ,Mbeya City na pia wanaweza kufanya vibaya, lakini adui yako muombee njaa tu.”
Simba inaendelea na Mazoezi yake katika Uwanja wa chuo cha polisi Kurasini kujiaanda na mchezo wao mkali dhidi ya African Lyon Jumapili hii katika uwanja wa taifa.

Ahadi ya Kichuya kuelekea fainali ya FA



“TUTAWAPIGA TU,” hayo ni maneno ya Kiungo Mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya, ametamba kuifungia timu yake bao muhimu kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Azam Sports Federation dhidi ya Mbao FC.
Simba ilipata tiketi ya kuingia fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), baada ya kuichapa Azam bao 1-0, katika mchezo uliochezwa Jumamosi iliyopita kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kichuya amesema amejipanga kucheza kwa kujituma kwasababu hiyo ndiyo itakuwa shukrani yake pekee kwa timu yake na kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ili waweze kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
“Nitafurahi sana kama nitafunga bao na kuipa ubingwa wa FA timu yangu, kwa sababu tumekuwa na msimu mzuri lakini mwisho umeonekana mgumu kutokana kila timu ambayo tunapambana nayo inakuwa inatupania kusababisha kupata matokeo ambayo hayaturidhishi,” amesema Kichuya.
Amesema kwa sasa yupo fiti na kiwango chake kimezidi kupanda siku hadi siku hivyo anauhakika wa kupata nafasi kwenye kikosi kitakachoanza mchezo huo na yupo tayari kujitoa kwa ajili ya timu yake.
Kichuya amesema amecheza na Mbao mara mbili na amewajua vizuri mapungufu yao hivyo atahakikisha anayatumia kwa kuwafunga ili kuisaidia timu yake kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Amesema hakuna linaloshindikana ingawa Mbao ni timu ngumu na iliwasumbua kwenye mechi zote mbili walizocheza kabla ya mchezo huo wa fainali lakini wamejipanga kucheza kufa na kupona ili kutwaa taji hilo.
“Fainali hii ni muhimu sana kwetu na tutahakikisha tutawapa raha wapenzi wetu kwa kuchukua kombe hilo, hivyo nitapambana kuhakikisha timu yangu inashinda na kila mchezaji analijua hilo hivyo hatutafanya mzaha kila mmoja atacheza kwa kujituma akijua fika nini tunachotakiwa kufanya,” alisema
Kichuya mwenye mabao 10 kwenye ligi ya Vodacom, anatarajiwa kuibeba timu yake kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Mbao ambao umepangwa kupigwa Mei 28 kwenye uwanja Jamuhuri uliopo Mkoani Dodoma.

Mimi ni shabiki wa ‘kutupwa’ wa Arsenal’ – Pro. Lipumba


Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) taifa Mh. Prof. Ibrahim amesema yeye ni shabiki wa kutupwa wa Arsenal licha ya klabu hiyo ya England kutotwaa mataji makubwa kwa muda mrefu.
“Arsenal haifanyi vizuri, lakini ndio timu yangu ninayoipenda,” Prof. Lipumba amesema kwenye kipindi cha Clouds 360 cha Clouds TV leo Alhamisi Mei 4, 2017 wakati akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali yanayohusiana na chama chao (CUF).
Lipumba pia amesema yeye amewahi kucheza soka wakati akiwa mwanafunzi wa shule ya sekondari japo haikua kwa kiwango cha ushindani.
“Nimewahi kucheza mpira wakati nasoma sekondari, lakini sio katika ngazi ya ushindani,” amesema Pro. Lipumba.

Monday, May 1, 2017

Hii ndio furaha kubwa ya mashabiki wa Tottenham inayowakera sana Arsenal


Kipigo cha bao 2 kwa 0 toka kwa Tottenham kimezidi kuididimiza Arsenal katika msimamo wa Epl msimu huu na kuzidi kuondoa matumaini ya Arsenal kucheza Champions league msimu ujao.
Lakini Arsenal kutocheza Champions League sio habari chungu sana kwa kuwa tuliitarajia toka siku nyingi, habari chungu sana kwa Arsenal ni kumaliza ligi chini ya Tottenham Hostpur.
Klabu hizi ni pinzani sana kutokana na ujirani wao katika jiji la London lakini Tottenham hawajawahi kumaliza ligi juu ya Arsenal ndani ya miaka 22 iliyopita lakini msimu huu hilo linaonekana kutokea.
Mashabiki wa Tottenham wameanza kuwa kero kubwa kwa Arsenal nchini Uingereza na ndio maana haikuwa ajabu kwa wao kupigana kabla na baada ya mchezo wao.
Kocha Arsene Wenger anaelewa kuhusu mashabiki wa Arsenal wanavyojisikia kutokana na Tottenham kumaliza msimu juu yao, na Wenger anajua mashabiki wanaumia sana.
Baada ya mchezo kati yao Wenger alisema “niwapongeze kwa hilo la kumaliza juu yetu lakini sisi hatujaingia katika ligi kwa ajili ya hilo, sisi nia yetu ilikuwa kombe”
Wenger amesisitiza kwamba hata siku moja wao kama Arsenal hawawezi jifananisha na Tottenham bali wao huwa wanajilinganisha na pale walipotaka kuwa msimu huu.
Naye kocha wa Tottenham Hotspur Mauricio Pochettino ambaye mashabiki wa Tot walikuwa wakiimba nyimbo za kumsifu kwa kuimaliza Arsenal na kukaa juu yao amesema anafuraha kuwapa furaha mashabiki.
“Kuwa juu ya Arsenal kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 22 ni jambo la furaha kwa mashabiki zetu na hata sisi pia lakini nia yetu haswa ni kutaka ubingwa wa Epl msimu huu” alisema Pochettino.
Pochettino pia hakuishia hapo bali amelalamikia upangwaji wa ratiba ya ligi ya Epl akisema anadhani kwa ilipofikia ni vyema kama ingekuwa timu zinazofukuzia ubingwa zikawa zinacheza kwa wakati mmoja.

Mara ya mwisho Tottenham kumaliza ligi juu ya Arsenal raisi wetu alikuwa Mwinyi.


Tottenham msimu huu watamaliza msimu juu ya Arsenal kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1995, hembu tukumbuke matukio yaliyotokea tangia kipindi hicho.
1.Raisi wa Tanzania alikuwa Mzee Mwinyi. May 1995 ni mwaka ambao ulikuwa wa uchaguzi uliomuingiza raisi Mkapa madarakani, kipindi ambacho Tottenham anamaliza ligi juu ya Arsenal bado Tanzania tulikuwa tuko awamu ya pili ya uraisi hadi sasa tuko ya tano,mzee mwinyi aliondoka ikulu Novemba 1995.
2.Wenger alikuwa kocha wa Nagoya Grampus. Wakati Tottenham akimaliza juu ya Arsenal kocha wa Arsenal alikuwa Pat Rice, kipindi hicho Wenger alikuwa zake Japan akiifundisha klabu ya Nagoya Grampus.
3.Manchester United walikuwa na makombe 9 tu ya Epl. Wakati Arsenal walipomaliza chini ya Tottenham hata Manchester United ambao sasa wana makombe 20 walikuwa wana makombe 9 tu kwa kipindi hicho.
4.Wastani wa malipo ya wachezaji Epl ilikuwa ni £130,000 kwa mwaka.Kwa utafiti uliofanywa mwaka huo ambao Tot walimaliza juu ya Arsenal wastani wa malipo kwa wachezaji wa ligi kuu Uingereza ilikuwa £130,000 kwa mwaka lakini sasa tafiti zinaonesha wastani wa malipo wa wachezaji wa Epl kwa mwaka huu ni £2,438,275.
5.Rekodi ya usajili wa dunia ilikuwa £13.2m.Miaka ya 95 kuelekea 96 kipindi hicho Ronaldo De Lima alikuwa akishikilia rekodi ya mchezaji aliyesajiliwa kwa dau kubwa kwa kipindi hicho ambapo usajili wake uliigharimu Barcelona £13.2m,lakini sasa kuna Paul Pogba kanunuliwa kwa £89m ikiwa ni tofauti ya £76m.
6.Hector Bellerin alikuwa anajifunza kutambaa.Huwezi amini kuhusu mlinzi huyu wa pembeni wa Arsenal kwani wakati Tottenham wakimaliza juu ya Arsenal alikuwa mdogo sana na hakuwa hata na uwezo wa kutambaa, mwaka huo ligi iliisha mwezi May 1995 wakati Bellerin alizaliwa March mwaka huo.

Ushindi mwingine wa Serengeti Boys kimataifa




Timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imepata ushindi wa tatu mfululizo tangu iondoke nchini kwenda kuweka kambi maalum kwa ajili ya maandalizi kujiandaa na mashindano ya AFCON kwa vijana chini ya miaka 17 itakayoanza mwezi Mei 14, 2017.
Serengeti Boys wameifunga timu ya taifa ya vijana ya Cameroon kwa goli 1-0 lililofungwa na Ally Ng’anzi kipindi cha kwanza katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa.
Huu ni mchezo wa tatu Serengeti inashinda mfululizo, ilishinda mechi mbili za kirafiki dhidi ya Gabon zilizochezwa nchini Morocco ambako Serengeti ilikua imeweka kambi kabla ya kwenda Cameroon.
Baada ya kumaliza kambi nchini Cameroon itaondoka na kuelekea moja kwa moja Gabon ambako zitafanyika fainali za michuano hiyo ya vijana itakayoshirikisha mataifa nane.

Kakolanya amevunja ukimya kuhusu kusugua benchi Yanga


Na Zainabu Rajabu
LICHA ya kukosa nafasi ya uhakika ndani ya kikosi cha Yanga, mlinda mlango Beno Kakolanya amesema ataendelea kukomaa akiamini kwamba ipo siku atapata nafasi kama wenzake.
Kakolanya aliyejiunga na Yanga msimu huu akitokea Tanzania Prisons, amekuwa akipakta nafasi kwa nadra huku Deogratius Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’ wakicheza mara kwa mara.
Shaffihdauda.co.tz. ilizungumza na golikipa Beno Kakolanya ambaye amesema: “Nimekuwa nikicheza na kupata changamoto kwani kila kipa anaekuja wanasema hawezi pata namba lakini kwangu mimi nimepewa zaidi ya mechi nne na nimeonesha kiwango kizuri ila kupata nafasi katika kikosi cha kwanza ni maamuzi ya mwalimu.
“Siwezi kuporomoka kiwango changu kwani najiamini naweza kutokana na juhudi zangu ndiyo maana Yanga wakanisajili ila naamini Mungu yupo wakinipa nafasi tena nitaitumia vizuri,” amesema Kakolanya.
Aidha, Kakolanya amesema yaliyotokea jana ni mchezo wa mpira huku akimalizia na kusema bahati haikuwa yao kutinga fainali.
“Tumeshambulia sana ili kutafuta bao la kusawazisha lakini uimara wa kikosi cha Mbao ulionekana kuimarika vizuri nakuondoa mipira yote ya hatari langoni mwao.”
Yanga ambao walikuwa mabingwa watetezi wa kombe hilo la Azam Sport Federation (FA) jana wameambulia kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mbao FC.

MUNTARI ABAGULIWA ITALIA, MWAMUZI AMTWANGA KADI YA NJANO, YEYE AAMUA KUTOKA NJE MECHI IKIENDELEA





Kiungo Mghana Sulley Muntari amekutana na tabia chafu na mbovu zinazopaswa kulaaniwa za baadhi ya wazungu wajinga kuamua kumbagua, jana.


Hali hiyo imemkuta katika mechi ya Ligi Kuu Italia maarufu kama Serie A wakati akiichezea Pescara dhidi ya Cagliari ambayo mashabiki wake ndiyo walimbagua Muntari ambaye baadaye alilazimika kutoka nje.



Muntari alilazimika kutoka nje baada ya kumfuata mwamuzi na kumueleza kilichokuwa kinatokea ili asimamishe mchezo kama sheria zinavyoeleza, lakini mwamuzi aligoma na kumpa kadi ya njano.


Kitendo hicho kilimuudhi zaidi na Muntari aliyewahi kung’ara na AC Milan, akaamua kutoka nje na kuiacha timu yake ikiwa na wachezaji pungufu uwanjani.



Baada ya kuona hivyo, meneja wa uwanja huo aliamua kutangaza kupitia spike za uwanja akiwaonya mashabiki hao kuacha ujinga huo.

Hii si mara ya kwanza kwa mashabiki wa Cagliari kuonyesha ubaguzi wa wazi, waliwahi kufanya hivyo kwa Samuel Et'oo mwaka 2010 wakati akiichezea Inter Milan, mwamuzi alisimamisha mchezo.
01 May 2017

-------------------------------------------------------

-------------------------------------------------------
HABARI MPYAMPYAhttp://2.bp.blogspot.com/-mFnDPXvIysA/VOZH1z-2rpI/AAAAAAAAADs/shOR30FtkF4/s1600/anigif.gif