RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI NA RAIS WA CAF, ISSA HAYATOU WAKIWA PAMOJA |
Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), limepokea taarifa juu ya mpango na kauli za
baadhi ya viongozi wa Young Africans SC kushawishi mashabiki wao kufanya
vurugu dhidi ya warushaji matangazo ya televisheni ya moja kwa moja
wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho la Afrika ngazi ya Makundi kati
ya Young Africans ya Tanzania na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC) utakaofanyika Juni 28, 2016 saa 10.00 jioni kwenye Uwanja
wa Dar es Salaam.
TFF
ikiwa msimamizi mkuu wa mpira wa miguu Tanzania, inawajibika na mara
moja inachukua nafasi hii kuwatahadharisha baadhi ya viongozi wa Young
Africans, wanachama na mashabiki wao kutofanya hivyo kwani itakuwa ni
kinyume na kanuni za mashindano na mikataba ya udhamini katika hatua
hii.
Ikumbukwe
kwamba CAF inamiliki asilimia mia moja ya haki za habari na masoko
katika ngazi hii ya makundi na jaribio lolote la kukwamisha matangazo ya
biashara au utengenezaji na urushaji wa matangazo ya televisheni au
ukwamishaji wa shughuli zingine kama hizo kwa CAF au wakala aliyeteuliwa
na CAF kutaigharimu klabu mwenyeji si kwa kutozwa faini tu lakini pia
uwezekano wa kuondolewa mashindanoni.
Pia
TFF inatoa tahadhari hiyo ikiwamo ile ya utamaduni wa kukaa uwanjani
ili kuepusha aina yoyote ya vurugu kwenye michezo yake hususani hii ya
hatua ya makundi. TFF inafahamu kuwa tayari viongozi wa Young Africans
walikwisha kusoma nyaraka na taarifa mbalimbali kuhusu kanuni na masuala
ya udhamini kwa timu zinazofuzu hatua ya Nane Bora.Wapenzi wa Yanga
wanaombwa kufika kwa wingi na kuishangilia kwa nguvu timu yao ikiwa ni
njia ya kuitia hamasa.Hata hivyo shamrashamra hizo zifanyike kwa kufuata
sheria,kanuni na taratibu za Mpira wa Miguu na sheria za nchi.
Vitendo
vya kuashiria vurugu na kufanya vurugu vikithibitishwa katika taarifa
ya Mwamuzi, Janny Sikazwe wa Zambia; Kamishna wa mchezo, Celestin
Ntangungira wa Rwanda na Mratibu Mkuu Maalumu kutoka Msumbiji, Sidio
Jose Mugadza, hatua zake zitachukuliwa dhidi yake ikiwamo KUONDOLEWA KWENYE MASHINDANO. Vilevile vitendo vya kutishia amani,kudhuru mwili au kuharibu mali vitachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za kijinai.
Katika
mchezo huo wa kimataifa Na. 107, Mwamuzi Sikazwe atasaidiwa na Jarson
Emiliano dos Santos kutoka Angola atayekuwa kwenye mstari wa kulia (line
1) na Berhe O’Michael wa Eritrea atayekuwa upande wa kushoto (line 2)
huku Wellington Kaoma wa Zambia akiwa ni mwamuzi wa akiba.
Wakati huohuo, kikao
cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini
kinatarajia kukaa siku ya Jumamosi tarehe 2 Julai 2016. Taarifa zaidi
itatolewa karibuni.
No comments:
Post a Comment