Beki
wa Yanga, Vincent Bossou, ametamka hadharani licha ya kukubali kipigo
cha mabai 2-1 kutoka kwa Mbeya City lakini hatamsahau mwamuzi wa kati wa
mchezo huo, Rajab Mrope kutokana na maamuzi yake kuwa tata.
Yanga
ilipata kipigo hicho kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya katika
mchezo wa Ligi Kuu Bara, juzi, ambapo beki huyo raia wa Togo anasema
hajawahi kuona maamuzi kadhaa yaliyofanywa na refa huyo.
“Tumefungwa
na tunakubali matokeo lakini sitasahau alichokifanya refa, alikuwa na
makosa mengi na maamuzi tata kibao ambayo yametugharimu kwa kiasi
kikubwa.
“Sidhani
kama marefa wa namna hii wataweza kulikomboa soka la Tanzania ambalo
linataka kupiga hatua kutoka hapa lilipo kwa sababu hawajiamini na hata
kuchezesha kwenyewe inakuwa shida na hata kusimamia maamuzi yao,”
alisema Bossou.
Katika
mchezo huo, mwamuzi alikubali bao la pili la Mbeya City lakini baada ya
kuzongwa na wachezaji wa Yanga waliodai haikuwa sahihi kwa kuwa faulo
iliyopigwa ilitekelezwa bila ruhusa ya mwamuzi, refa huyo akaamuru faulo
irudiwe, Mbeya City nao wakamzonga wakilalamika, akabadili maamuzi tena
na kukubali kuwa ni bao na mpira uwekwe kati.
No comments:
Post a Comment