Nyanda wa Yanga, Ali Mustapha ‘Barthez’,
amejipalia makaa na sasa kuna uwezekano mkubwa akasugua benchi katika michezo
iliyobaki ya Ligi Kuu Bara na nafasi yake ikarudishwa kwa Deogratius Munishi ‘Dida’.
Barthez amekuwa katika wakati mgumu mara baada
ya kufungwa bao na Mganda, Emmanuel Okwi katika mechi dhidi ya Simba, Jumapili
iliyopita katika mechi ya Ligi Kuu Bara jambo ambalo limechangia kumvuruga.
Imeelezwa kuwa hatua hiyo ya kuwa na uwezekano
wa kuwekwa benchi imetokana na mambo mawili; moja ni kuhofia kumuweka tena
langoni kwenye mechi inayofuata akiwa na msongo wa mawazo kutokana na lawama
anazopokea, lakini kingine ni kumuacha benchi ajifunze kwanza na kujiweka fiti
upya.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Yanga
kimelipenyezea Championi Ijumaa kuwa, hata katika mechi
inayofuata ya Yanga dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe itakayopigwa keshokutwa
Jumapili, kipa atakayelinda lango la timu hiyo ni Dida.
Hata hivyo, imefafanuliwa zaidi kuwa, kurudi
kwake dimbani Barthez, kutategemea na kiwango cha Dida atakachoonyesha.
“Kiukweli Barthez amekalia kuti kavu na nafasi
yake imechukuliwa na Dida, yaani yule anaweza kucheza kama Dida ataharibu
atakaporejea langoni. Vinginevyo itakuwa ndiyo basi tena.
“Bao alilofungwa na Okwi imeonekana naye
alichangia kwa kiasi fulani kutokana na kutokuwa makini,” kilisema chanzo.
Kabla ya mechi hiyo, Barthez alisimama langoni
katika michezo tisa mfululizo na kufungwa mabao mawili, lakini bao la Okwi
ndilo limeonekana nuksi kwake.
No comments:
Post a Comment