Friday, March 13, 2015

MAKAPU:PLUIJIN AMEFANYA CHAGUO SAHIHI YANGA


MAKAPU (KUSHOTO) AKIPAMBANA NA AJIBU WA SIMBA....

MAKOCHA wanaweza kuwa ndiyo binadamu wanaoongoza kwa kulaumiwa kuliko wengi wote katika mchezo wa soka, ikiwezekana hata michezo mingine.

Mara nyingi, kocha anapoisaidia timu kupata mafanikio, kawaida huonekana ni mafanikio ya wengi, ikifeli, lawama zinaangukia kwake, hakuwa makini au hafai.
Tumeona hayo yakimuangukia Arsene Wenger wa Arsenal na makocha wengine wengi na hasa jambo la kujali vijana ambavyo limekuwa ni kama msumari kwa makocha wengi.
Jumapili iliyopita kulikuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara uliosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, kwa kuwa unawakutanisha watani wa jadi, Simba na Yanga.
Simba waiibuka na ushindi wa bao safi la Emmanuel Okwi, bao ambalo unaweza kuliweka katika historia ya moja ya mabao bora yaliyowahi kufungwa katika ligi hiyo.
Baada ya mechi hiyo, kama ilivyo ada kunakuwa na lawama nyingi na kawaida, mashabiki na hata viongozi wa timu hizo mbili kongwe, mara nyingi hawakubali kufungwa kimpira, badala yake kila mmoja huangusha lawama kivyake.
Moja ya lawama zilizoangushwa ni Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm kumtumia kiungo kinda Said Juma ‘Makapu’ ambaye alicheza katika kiungo cha ukabaji. Wengi walilalama kwamba Mholanzi huyo vipi aliamua kumchezesha kiungo huyo kinda katika mechi kubwa kama hiyo ya watani.
Wengi wanaona Makapu kwa kuwa ni kinda, basi alikuwa tatizo katika kikosi cha Yanga siku hiyo na wako waliopendekeza huenda Salum Telela angecheza siku hiyo.
Wako wanaoamini bora Yanga ingemchezesha Telela namba mbili na mkongwe Mbuyu Twite angerudi katikati kuendesha nafasi hiyo ya ukabaji kama ambavyo amekuwa akifanya mara kadhaa.
Hakuna aliyeiona kazi ya Makapu siku hiyo, wala hakuna anayeona jambo kubwa la msingi alilolifanya Pluijm kwa mchezaji huyo, kwa Yanga na Tanzania kwa jumla.
Makapu anayevaa namba 22 alikuwa kati ya wachezaji bora kabisa katika mechi hiyo, nitaeleza sababu kadhaa.
Moja:
Yanga haikuwa na tatizo katika kiungo cha ukabaji kwa kuwa alikuwa na nguvu na ukabaji wake ni ule wa kukera.
Ndiyo maana utaona kosakosa nyingi zilikuwa upande wa lango la Simba na Yanga wakashindwa kuzitumia lakini ulinzi wa Yanga ukiongozwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akisaidiana na Makapu na Yondani ulikuwa bora hadi walipofanya kosa lililozaa bao.
Hata ungemuweka mchezaji mkongwe, kosa walilofanya Yanga, bado lingeweza kuwa tatizo, ndiyo maana mpira wa mwisho wakati Okwi anafunga, aliupiga mbele ya Twite, lazima uamini yeyote anaweza kukosea.
Mbili:
Hakukuwa na mipira mingi ya juu iliyokuwa na madhara katika ukiachana na ule mpira aliopiga Elius Maguri mbele ya Cannavaro ambaye tayari alishaumia. Hii ilitokana na ubora wa mipira ya juu kuongezeka upande wa Yanga kwa kuwa Makapu ni kati ya wachezaji warefu na wanaopiga vichwa.
Tatu:
Makapu ana nguvu, ana uwezo wa kupiga miguu yote. Alikuwa na tatizo kidogo la nafasi, wakati upi mwafaka wa kuwa wapi na afanye nini. lakini hilo lilitokana na uzoefu alionao. Ili abadilike, ni lazima acheze, hiyo haina ujanja.
Kumlaumu Pluijm, pia ni sawa na zile lawama za msimu mmoja na nusu tu uliopita pale mashabiki walipomlaumu Kocha Ernie Brandts pale alipoanza kumuamini Telela aliyeonekana hafai na sasa wengi wanalia achezeshwe.
Kwa Pluijm, ana kila sababu ya kuendelea kumuamini Makapu, kinda mwenye kila sababu ya kucheza namba sita kwa kuwa ana sifa nyingi kwa asilimia 75 sasa. Anachotakiwa ni kuaminiwa na kupewa nafasi zaidi. Watu hujifunza zaidi hujifunza kwa vitendo, hivyo Makapu hawezi kujifunza akiwa benchi.
Kama Makapu ataendelea kupewa nafasi zaidi, basi ndiye shujaa na tegemeo wa Yanga hapo baadaye kama ambavyo Simba waliwaamini akina Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’ na Said Ndemla na leo, ndiyo tegemeo la kikosi chao.
Acha wengine waone Plujm anakosea, lakini Makapu kucheza namba sita na sifa alizonazo ni chaguo sahihi kabisa, tena katika wakati mwafaka.

No comments:

Post a Comment

-------------------------------------------------------

-------------------------------------------------------
HABARI MPYAMPYAhttp://2.bp.blogspot.com/-mFnDPXvIysA/VOZH1z-2rpI/AAAAAAAAADs/shOR30FtkF4/s1600/anigif.gif