Habari na mtandao wa AzamFC:
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuwa
mwenyeji wa michuano maalumu ya kimataifa ya timu nne itakayofanyika
mwanzoni mwa mwakani.
Michuano hiyo ni ile waliyoenda kushiriki jijini Ndola Zambia hivi
karibuni na kutwaa ubingwa, ambapo imeanzishwa kwa muungano wa klabu
tatu, Azam FC, TP Mazembe na Zesco United.
Akizungumza hivi karibuni na mtandao wa www.azamfc.co.tz mara baada
ya kikosi hicho kurejea kutoka Zambia, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC,
Saad Kawemba, alisema mwakani ni zamu yao kuandaa michuano hiyo na hivi
sasa wanajipanga kuweza kuwaalika marafiki zao hao pamoja na kuangalia
namna gani watakavyocheza nao hapa nyumbani.
“Tulialikwa kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo ilipofanyika
Kongo katika mji wa Lubumbashi, ambapo tulikubaliana kimaandishi kwamba
tutengeneze umoja huu, ambao ni umoja wa vilabu vitatu TP Mazembe, Zesco
United na sisi Azam FC.
“Na mwaka huu tumepata nafasi hiyo tena kwa kualikwa, ambapo tumeweza
kuwa mabingwa na mwaka jana TP Mazembe walikuwa mabingwa na akaenda
kuchukua ubingwa wa Afrika (Ligi ya Mabingwa Afrika), kwa hiyo Azam FC
mwaka huu tumechukua ubingwa tunategemea kupata matokeo mazuri katika
mashindano ya CAF kwa sababu mechi nzuri na tumejiandaa,” alisema.
Kawemba alisema kuwa lengo kubwa la kuunda umoja huo ni kuweza kuzipa
nafasi timu zinazoshiriki michuano ya CAF kuweza kufanya mazoezi kwa
pamoja, huku akisisitiza kuwa michuano ya umoja huo ni mikubwa na sio
kama wengi wanavyodhania.
“Ingawa watu wanaona kuwa hayana tija, lakini kwetu tunaamini ya kuwa
yanatija na yametupa nafasi hiyo ya kujijenga, kila mtu aliona
tulivyocheza mwaka jana dhidi ya El Merreikh baada ya kutoka Lubumbashi
na mwaka huu tunaamini kabisa mechi ya Bidvest Wits itakuwa tofauti na
tulikuwa tukisema hivyo pia hata hao wanaotubeza sasa hivi walikuwa
wakituuliza Azam mnajiandaa kwa namna gani kwenye michuano ya Kimataifa,
kwa hiyo haya ndio majibu na huwa hatuzungumzi bali tunafanya kwa
vitendo,” alisema.
Aliongeza kuwa; “Na sio kama tunabeza mtu yoyote, hatuwezi kujiandaa
kucheza dhidi ya Bidvest kwa kucheza na klabu ya hapa nyumbani, hakuna
klabu yoyote inayoweza kutupa mazoezi hapa, kwa hiyo tumeenda kufanya
mazoezi huko kwa ajili ya Bidvest na timu zinazokuja na kwa hapa
nyumbani tumerudi, tumefanya mazoezi ya juu kidogo na tunaamini
hakutakuwa na tatizo lolote.”
Bosi huyo aliwaondoa hofu mashabiki wa Azam FC kwa kuwaambia kuwa
wamekuja kuendeleza pale walipoishia na hawana wasiwasi kwa
yanayoendelea hivi sasa Tanzania katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara (VPL).
“Tunaangalia michezo yetu iliyoko mbele yetu na tuna uhakika
tutafanya vizuri na tutakaa katika nafasi ambayo tunastahili kukaa na
kila mtu anajua nafasi hiyo ni ipi,” alimalizia Kawemba.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB hivi sasa inashika nafasi ya
tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa imejisanyia jumla ya pointi 42 sawa na
Simba inayokamata nafasi ya pili na Yanga inayoshika usukani kwa pointi
43.
Lakini matajiri hao wa Azam Complex wana mechi mbili mkononi,
zinazoweza kuwaweka juu kileleni kwa tofauti ya pointi tano kwa
atakayemfuatia kama wakizishinda zote, jambo la kuvutia zaidi mpaka sasa
ndio timu pekee kwenye ligi ambayo haijapoteza mchezo wowote.