Thursday, July 7, 2016

HATIMAYE UFARANSA YATUA FAINALI EURO 2016, USO KWA USO NA URENO


France fans
Wenyeji Ufaransa wamefanikiwa kufuzu kucheza hatua ya fainali ya Euro 2016 kwa ushindi wao wa kwanza dhidi ya Ujerumani kwenye michuano mikubwa tangu mwaka 1958.
Antoine Griezmann, ndiye mfungaji anayeongoza kwa magoli hadi sasa na ndiye aliyeamua mchezo huo kwa kufunga bao katika kila kipindi na kuipeleka Ufaransa kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Ureno utakaochezwa Jumapili kwenye uwanja wa Stade de France.
Griezmann alianza kufunga mkwaju wa penati kipindi cha kwanza baada ya referee Nicola Rizzoli raia wa Italy kumtuhumun Bastian Schweinsteiger kuunawa mpira wakati akiwania mpira wa juu dhidi ya Patrice Evra.
Ufaransa iliweza kumudu presha ya Ujerumani kabla ya Griezmann kupachika bao la ushindi zikiwa zimesalia dakika 18 mpira kumalizika alipopiga mkwaju akiwa karibu na goli la Ujerumani kufuatia golikipa Manuel Neuer kuokoa krosi ya Paul Pogba.
Joshua Kimmich aligongesha mwamba kwa upande wa Ujerumani huku golikipa wa Ufaransa Hugo Lloris akiokoa mchomo wa hatari kuwanyima goli washindi hao wa kombe la dunia.
Rekodi zilizowekwa baada ya mchezo huo
  • Ufaransa ni nchi ya kwanza kufika fainali ya Euro ikiwa nchi mwenyeji wa mashindano (mara ya kwanza ilikuwa 1984)
  • Ufaransa wamefunga Ujerumani kwenye michuano mikubwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1958. Ni mchezo wao wa kwanza pia kutoruhusu goli dhidi ya Ujerumani.
  • Ujerumani wamepoteza nusu fainali yao ya nne kati ya sita kwenye michuano mikubwa (2006, 2010, 2012, 2016).
  • Bastian Schweinsteiger amecheza mchezo wake wa 38 kwenye michuano mikubwa, michezo mingi zaidi ya mchezaji yeyote kwenye historia ya Kombe la Dunia na michuano ya Ulaya.
  • Michel Platini bado anashikilia rekodi ya magoli mengi zaidi kwenye msimu mmoja wa michuano ya Euro (magoli 9 Euro 1984) magoli matatu zaidi ya Antoine Griezmann aliyefunga magoli 6 hadi sasa Euro 2016

Wednesday, July 6, 2016

NUSU FAINALI YA KWANZA EURO 2016: URENO VS WALES NI VITA YA RONALDO NA BALE

Bale-Ronaldo
Nusu fainali ya kwanza ya michuano ya Euro inapigwa leo, kati ya Ureno na Wales, mchezo utakaofanyika katika dimba la Stade des Lumières lililopo jijini Lyon majira ya saa nne za usiku.
Huu ni mchezo ambao unabeba hisia kubwa kutokana na kukutana kwa mafahari wawili wa Real Madrid Gareth Bale na Cristiano Ronaldo.
Taarifa kutoka kila timu
Kiungo wa Wales Aaron Ramsey na mlinzi Ben Davies wote hawatakuwepo kutokana na kutumikia adhabu ya kuwa na kadi mbili za njano.
Nafasi ya Ramsey inaweza kuzibwa na Jonny Williams, Andy King au Dave Edwards.
James Collins anaweza kuziba nafasi ya Davies au vinginevyo, Jazz Richards anaweza kuanza kama beki wa kulia huku Chris Gunter akihamishiwa katikati kucheza kama beki wa kati.
Ureno watakuwa wakifuatilia kwa karibu maendeleo ya beki wao Pepe, ambaye alifanya jana alifanya mazoezi peke yake kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya paja.
William Carvalho hatakuwepo kwenye mchezo wa leo, hivyo Danilo anatarajiwa kujaza pengo hilo kwenye nafasi ya kiungo wa kati kwa upande wa Ureno.
Beki wa kushoto Raphael Guerreiro na kiungo Andre Gomes ambao walikosa mchezo wa robo fainali dhidi ya Poland kufuatia kusumbuliwa na maumivu ya misuli, wanarejea leo baada ya kupona.
Kocha wa Ureno Fernando Santos amesema kwamba endapo atakuwa hana uhakika na afya ya Pepe basi hatamchezesha beki huyo.
“Kwa upande wa Pepe, pengine utakuwa unajitekenya na kucheka mwenyewe kitandani kwasababu sitaweza kujibu swali hilo,” alisema.
“Kama Pepe anakuwa fiti kwa asilimia 100, nitafikiria juu ya hilo na pengine anaweza kuanza mchezo wa leo. kama haitawezekana pia hakuna tatizo. Wachezaji wote wanapaswa kuwa fiti kwa asilimia 100 kwa ajili ya mchezo huu.”
Uchambuzi wa mchezo.
Hili ni pambano la kihistoria kwa upande wa Wales, ambao wanaenda kwa mara ya kwanza wanacheza mchezo mkubwa wa kimashindano katika jiji la Lyon.
Ureno kwa upande wao kuna tofauti kidogo, wana uzoefu mkubwa wa kucheza kwenye hatua hii. Hii ni mara ya saba kwa ‘Wamakonde’ hao wa kizungu kufika hatua hii kwenye michuano ya Kombe la Dunia na Michuano ya Ulaya, lakini mara moja tu wakifanikiwa kuvuka hatua hio na kutinga fainali. Walifanya hivyo kwenye Euro ya mwaka 2004.
Mpaka sasa Ureno hawajashinda mchezo wowote ndani ya dakika 90 kwenye michuano ya mwaka huu. Lakini nguvu yao ya kuamua matokeo ilionekana kwenye mchezo dhidi ya Croatia na Poland, na leo watakuwa na kazi nyingine nzito dhidi ya wabishi wa Wales.
Santos ana imani kwamba timu yake itapata matokeo chanya leo.
“Sina wasiwasi wowote juu ya mchezo wa leo, Ninachoangalia kwa sasa ni kufika fainali na kubeba kombe tu,” amesema.
“Napenda kucheza soka la kuvutia? Ndio, ni kweli. Lakini kuna tofauti kati ya kucheza soka la kuvutia na kurudi nyumbani, au kucheza soka bovu na kuendelea kubaki hapa, ningependa kucheza soka bovu na kuendelea kubaki hapa.”
Tofauti na wapinzani wao, Wale wamekuwa kwenye kiwango bora kabisa kwenye michuano hii hasa kwenye mchezo waliopata ushindi mnono dhidi ya Belgium. Lakini bado wanaamini kuna mengi zaidi ya hapo yanakuja pengine ikibidi kufika fainali na kuchukua kombe na kuweka rekodi mpya.
“Ni dhahiri tumevuka malengo ya watu wengi,” amesema Gareth Bale.
“Lakini siku zote tuliamini tungefanya hivi, kama unakumbuka walichofanya mwaka 2004 na Denmark mwaka 1992, sasa kwanini sisi tushindwe kufanya hivyo?”
Mfanikio ya Wale yamewachanganya na wachezaji wenyewe. Kiungo Joe Ledley alipaswa kufunga ndoa Jumamosi lakini aliamua kuahirisha.
“Nilikuwa na iamni kubwa kwamba tungeweza kufanya kitu kwenye michuano hii, na ndiyo maana nikapanga mapumziko yangu yaanze tarehe 11 July, siku moja baada ya fainali, mimi sipo kama wengine!”Bale alimaliza.
Takwimu za mechi walizokutana
  • Kabla ya mchezo wa leo, timu hizi zimekutana mara tatu tu na haikuwa kwenye michezo ya mashindano
  • Kati ya michezo hiy, Ureno wameshinda mara mbili na Wales kushinda mara moja.
  • Mara ya mwisho kukutana ndani ya miaka 65 iliyopita, ilikuwa ni kwenye mchezo wa kirafiki mwaka 2000 na Ureno kushinda magoli 3-0.
Ureno
  • Ureno wamepoteza nusu fainali sita kwenye michuano ya Kombe la Dunia na Euro na kushinda moja tu dhidi ya Uholanzi kwa mabao 2-1 mwaka 2004, kwenye Euro iliyofanyika nchini mwao na Ronaldo alifunga goli kwenye mchezo huo.
  • Hii ni mara ya tano kwa Ureno kufika hatua ya nusu fainali kwenye Michuano ya Euro.
  • Mechi sita za mwisho kwa Ureno kwenye Michuano ya Ulaya iliisha kwa sare baada ya dakika 90. Mitano ni kwenye Euro ya mwaka huu na mmoja wa nusu fainali dhidi ya Uhispania kwenye Euro ya mwaka 2012 ambapo walipoteza kwa penati. Mchezo huo uliisha kwa suluhu.
  • Ureno hawajafungwa kwenye michezo 12 ya mashindano chini ya kocha Fernando Santos (ushindi mara nane, sare mara nne), ushindi katika michezo yote nane ukiwa ni kwa tofauti ya goli moja-moja. Mchezo wao dhidi ya Poland unahesabiwa kama sare.
  • Cristiano Ronaldo amefunga magoli 2 tu katika michezo 13 ya mtoano kwenye michuano ya kimataifa. Amebakisha goli moja tu kufikia rekodi ya ufungaji bora wa muda wote ya magoli tisa inayoshikiliwa na Michel Platini kwenye michuano hii.
  • Nani amehusika kwenye magoli matatu kati ya sita ya Ureno kwenye Michuano ya Euro mwaka huu, amefunga magoli mawili na kutoa pasi moja ya goli.
  • Ureno wameshinda changamoto za mikwaju ya penati kwenye mechi tatu kati ya nne kwenye michuano mbalimbali. Hakuna timu iliyowahi kushinda mara mbili mfululizo changamoto za mikwaju ya penati katika historia ya mashindano haya.
Wales
  • Wales wamefunga magoli 10 kwenye michuano ya Euro mwaka huu. Timu pekee ya Uingereza kufunga zaidi yao ilikuwa ni England ambao walifunga magoli 11 kwenye Kombe la Dunia mwaka 1966.
  • Ni ufaransa pekee ndio wenye safu bora ya ushambuliaji zaidi ya Wales kwenye michuano hii. Wamefunga magoli 11.
  • Wales ndio timu ya kwanza kufika hatia ya nusu fainali ya Michuano ya Ulaya ikiwa kama timu iliyoshiriki kwa mara ya kwanza tangu kwa mara ya mwisho walivyofanya Sweden mwaka 1992
  • Hii ni mara ya kwanza kwa Wales kufika hatua ya nusu fainali katika michuano iliyoandaliwa na ama Uefa au Fifa kwa level yoyote iwe wanaume au wanawake.
  • Hal Robson-Kanu amefunga magoli mawili kutokana na mashuti matatu yaliyolenga lango kwenye michuano ya mwaka huu.
  • Aaron Ramsey, ambaye anakosa mchezo wa leo kutokana na kutumikia adhabu yake ya kadi mbili za njano, amefunga au kutoa pasi ya goli kwenye magoli nane ya mwisho kufungwa na Wale (ukiondoa goli la kujifunga)
  • Gareth Bale amepiga mashuti 14 yaliyolenga lango kwenye michuano ya mwaka huu, zaidi ya mchezaji yeyote kwenye michuano hii.

Monday, July 4, 2016

ANGBAN NAYE KUMBE SI SIRIAZ, SIKIA HII ALIVYOCHELEWA NDEGE



Kipa namba moja wa Simba, Vincent Angban raia wa Ivory Coast, alishindwa kutua nchini usiku wa kuamkia jana kutokana na kuchelewa ndege alipokuwa akitokea nchini kwao.
Angban alitarajia kutua akiambatana na mshambuliaji mpya wa timu hiyo raia wa Ivory Coast, Blagnon Goue Fredric alishindwa kufanya hivyo huku Fredric ambaye alikuwa akiitumikia Klabu ya African Sports ya Ivory Coast akiwasili peke yake juzi usiku kisha akitarajiwa kufanya mazungumzo ya usajili kumalizana na uongozi wa Simba, jana Jumapili.
Habari za kuamnika kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa kutokana na hali hiyo Angban anatarajia kutua nchini usiku wa kuamkia leo tayari kwa kuanza maandalizi yake kwa ajili ya msimu ujao.
“Mshambuliaji wetu mpya ambaye tunatarajia kumsajili hivi karibuni ambaye ni raia wa Ivory Coast tayari ameshatua na sasa yupo katika mazungumzo ya mwishomwisho na uongozi.
“Alikua aje na Angban ambaye alikwama kutokana na kuchelewa ndege, baada ya kuchelewa akaomba uongozi umuongezee fedha ile ambayo huwa inaongezwa inapotokea msafiri amechelewa ndege, uongozi ulikataa an ameongeza mwenyewe kwa kuwa ni uzembe wake,” kilisema chanzo kutoka Simba.

MAYANJA YUKO JIJINI DAR ES SALAAM NA HAYA NDIYO MANENO YAKE KUHUSIANA NA JOSEPH OMOG



Kocha Mganda, Jackson Mayanja aliyeelezwa kuwa mbioni kuachana na Simba kutokana na sababu mbalimbali, ametua jijini Dar, juzi usiku na kufunguka kuhusiana na kocha mkuu mpya wa timu hiyo, Joseph Omog.
Mayanja ambaye ametua nchini akitokea Uganda alikokwenda kwa ajili ya mapumziko mara baada ya kumalizika kwa ligi msimu uliopita, hivi karibuni kuliibuka taarifa zilizodai kuwa hayupo tayari kufanya kazi chini ya Omog lakini amekanusha hilo.
“Kama nikielewana na Simba nitafanya kazi tu chini ya Omog kwa kuwa nafahamu majukumu yangu kama kocha msaidizi,” alisema Mayanja.
Awali kulikuwa na taarifa kuwa Mayanja anaweza kutua katika timu yake ya zamani ya Kagera Sugar au Mwadui FC, ambapo yeye mwenyewe amekiri kufanya mazungumzo na klabu hizo kwa kuwa mkataba wake na Simba ulimalizika.
“Kweli Kagera na Mwadui wananihitaji, hata Kiyovu SC ya Rwanda pia lakini nipo Dar kwa kuwa nimetumiwa tiketi na Simba. Hivyo, nitawasikiliza Simba kwanza baada ya hapo ndiyo kitakachofuata,” alisema kocha huyo.
Taarifa za ndani ya Simba zinaeleza kuwa Mayanja alitarajiwa kukutana na Omog, jana kwa ajili ya mazungumzo.

Akiwa kocha wa muda wa Simba, Mayanja aliiongoza Simba katika mechi 16 za Ligi Kuu Bara na kushinda 11, sare moja na kupoteza nne dhidi ya Yanga, Mwadui, Toto African na JKT Ruvu.

KAZI IPO, YANGA WATAMBA WAKIMALIZANA NA TSHABALALA NDIYO MWISHO WA USAJILI WAO



Uongozi wa Klabu ya Yanga umesema bado upo katika harakati za kuhakikisha unamnasa beki wa kushoto wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kwa kuwa ndiyo chaguo lao.

Tshabalala ambaye msimu ujao atatambulika kama Zimbwe Jr, alitua Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Kagera Sugar ambapo kwa sasa amekuwa lulu ndani ya timu hiyo kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa.
Mmoja wa mabosi wa Yanga amesema kuwa wapo katika harakati za kuhakikisha wanamnasa beki huyo kwa ajili ya kuleta changamoto kwa Mwinyi Haji na Oscar Joshua kutokana na viwango vyao kuonekana kupwaya.
Bosi huyo alisema kwa upande wao nafasi iliyobaki katika usajili wa msimu huu ni beki wa kushoto na kiungo mmoja ambao wataweza kuwasaidia katika ligi na mashindano ya kimataifa.
“Tunataka beki wa kushoto na chaguo letu ni Tshabalala wa Simba, huyo ndiyo atakuwa mtu sahihi wa kuweza kutoa changamoto kwa (Oscar) Joshua na (Haji) Mwinyi.
“Unajua tatizo halipo kwa mchezaji kwa sababu tumeshakutana naye zaidi ya mara nne na ameonyesha kukubali isipokuwa Simba ndiyo wanaonekana kuwa ni wagumu kwa kuwa bado wanamkataba naye wa mwaka mmoja,” alisema bosi huyo.
Alipotafutwa  Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Murro alisema kuwa kwa sasa hawezi kuliongelea suala hilo kwa kuwa bado halijafika mezani kwake.

Ikumbukwe kuwa, hivi karibuni uongozi wa Simba uliwahi kusema hauna mpango wa kumuuza mchezaji huyo kutokana na kuwa ni msaada mkubwa ndani ya timu hiyo.

SOURCE: CHAMPIONI

KICHUYA ANA UHAKIKA KABISA, ATATUA SIMBA MAANA NDIYO ANAPOPATAKA



Kiungo myumbulikaji wa Mtibwa Sugar, Shiza Kichuya anayewaniwa na Simba amefunguka kuwa vimesalia vitu vichache kwa ajili ya kuvaa uzi mwekundu msimu ujao kwa ajili ya kuitumikia Simba.
Kichuya, mchezaji anayesifika kwa mashuti, nguvu na uwezo wa kumiliki mpira, alianza kuhusishwa kuhamia Simba mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara, hivi karibuni amefunguka kuwa kwa upande wake tayari ameshamaliza kila kitu na kilichobaki sasa ni uongozi wa Mtibwa kumalizana na Simba.
Aidha, alisema kwamba kwa kuwa bado yupo kwenye mkataba na Mtibwa, kila kitu sasa kimehamia kwa Mkurugenzi wa Mtibwa, Jamal Bayser na yeye ndiye anayefanya mazungumzo ya mwisho na mabosi wa Simba kabla ya kupewa taarifa ya maafikiano ya kumwaga saini.
“Siwezi kulizungumzia kwa undani hili suala lakini niseme tu kwamba kwa upande wangu nishamaliza kila kitu na nimepewa taarifa tu kwamba hata kwa upande wa viongozi wa Mtibwa na Simba nao wamefikia pazuri, kwa hiyo nasubiri taarifa ya mwisho.
“Kimsingi ieleweke kwamba mpira ni ajira yangu na kokote nafanya kazi, kama nitafanikiwa kutua Simba itakuwa safi pia maana popote nitakapokwenda nitapiga mzigo kama kawaida,” alisema Kichuya anayetajwa kuwa moja ya wachezaji walioonyesha kiwango cha juu msimu uliopita.
Kichuya anakumbukwa pia kwa kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi katika Ligi Kuu Bara kwa mwezi Machi katika msimu uliopita ambapo uwezo wake ulimwezesha pia kuitwa katika timu ya taifa kwa mara ya kwanza chini ya Kocha wa Taifa Stars, Charles Mkwasa kwa ajili ya mechi dhidi ya Chad iliyofanyika Machi 23, 2016, jijini N'Djamena.
Kuhusiana na hilo, Bayser alisema: “Tunasikia Simba wanamtaka lakini sisi pia tumepanga kumbakisha kikosini kwetu lakini akikataa hatutakuwa na namna, tutamuacha aende kwani hayo yatakuwa maamuzi yake mwenyewe.”

Saturday, July 2, 2016

NEYMAR AONGOZA KWA MSHAHARA MBELE YA MESSI, RONALDO



Neymar wa Barcelona ndiye anachukua mshahara mkubwa zaidi kwa mwaka mmoja. Nafuatiwa na Messi na hivyo kuifanya Barcelona kuwa inalipa mshahara mkubwa zaidi ikifuatiwa na Madrid.


Tano bora inaonekana kutawaliwa na Barcelona na Madrid zikiwa na wachezaji wawili kila moja. Maana yake timu za Hispania ndiyo zinalipa vizuri zaidi hasa kwa wachezaji wake nyota zaidi.

10 BORA HII HAPA:
Neymar:  euro milioni 56
Messi:  euro milioni 50
Cristiano: euro milion 47.5
Ibrahimovic:  euro milioni 26.7
Bale:  euro milioni 21.4
Rooney:  euro milioni 16.9
Luis Suarez:  euro milioni 16
Iniesta:  euro milioni 16
Hazard:  euro milioni 16
Aguero:  euro milioni 15.1

HII NI KWA MUJIBU WA GAZETI NAMBA MOJA LA MICHEZO LA HISPANIA LA MARCA

ILIKUWA BONGE LA GAME; UJERUMANI YATINGA NUSU FAINALI KWA PENALTI 6-5, LAKINI ITALIA SI MCHEZO



Germany: Neuer, Howedes, Boateng, Hummels, Hector, Kimmich, Khedira, Kroos, Ozil, Muller, Gomez. 
Subs: Leno, Mustafi, Schweinsteiger, Schurrle, Podolski, Draxler, Can, Weigl, Tah, Gotze, Sane, ter Stegen.
Goal: Ozil 65 
Italy: Buffon, Barzagli, Bonucci, Chiellini, Florenzi, Sturaro, Parolo, Giaccherini, De Sciglio, Pelle, Eder. 
Subs: Sirigu, Darmian, Ogbonna, Candreva, Zaza, Immobile, De Rossi, Insigne, Bernardeschi, El Shaarawy, Marchetti.
Goal: Bonucci 78 
Referee: Viktor Kassai (Hungary)













Friday, July 1, 2016

ISHU YA KWENDA TP MAZEMBE, MAHADHI ASEMA KAMA VIPI POA TU



Kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga, Juma Mahadhi amefunguka kuwa yupo tayari kujiunga na TP Mazembe iwapo watampa ofa ya maana huku akisisitiza anajipanga kuisaidia timu yake katika michezo iliyobaki kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mahadhi  aliyejiunga na Yanga akitokea Coastal Union ya Tanga, alionyesha uwezo mkubwa katika mchezo dhidi ya TP Mazembe, Jumanne ya wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar ambapo alidumu kwa dakika 65 kabla ya kubanwa na misuli iliyosababisha atolewe na nafasi yake kuchukuliwa na Geoffrey Mwashiuya.

Mahadhi alisema kwa sasa anajipanga upya kwa ajili ya kuisadia timu yake katika michezo iliyobakia ya michuano hiyo ambayo ni ya pili kwa ukubwa upande wa ngazi ya klabu Afrika hivyo hataki kuipoteza nafasi hiyo.

“Ishu kubwa ilikuwa ni misuli ilinikamata na kusababisha nishindwe kuendela na mchezo japo awali nilikuwa nacheza kwa hofu sana, nikiogopa kuharibu lakini kadiri muda ulivyozidi kwenda nikawa naona kumbe naweza kufanya kitu kwa ajili ya timu yangu ila bahati mbaya ndiyo hivyo sikuweza kuendelea na mchezo ambao kwetu ulikuwa na umuhimu sana.

“Lakini naamini nitakuwa sawa mapema tu Mungu akipenda kwa sababu malengo yangu nimeyaweka katika michezo iliyosalia.


“Kama Mazembe watakuwa kweli wananihitaji basi nitakuwa tayari kwenda kujiunga nao iwapo wataleta ofa ambayo itakuwa na maslahi mazuri maana mimi ni mchezaji na kazi yangi ni mpira sasa fursa ikitokea lazima niitumie,” alisema Mahadhi. 

SOURCE: CHAMPIONI

SERENGETI BOYS SAAFI, WAKO TAYARI KWA AJILI YA KAZI YA SHELISHELI



Kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys tayari kipo mjini Victoria nchini Shelisheli kuwavaa wenyeji katika mechi ya kuwania kucheza michuano ya Afrika.

Katika mechi ya kwanza, Serengeti Boys waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 jijini Dar es Salaam na sasa wanatakiwa kupata sare ya aina yoyote au ushindi ikiwezekana.

Kocha Mkuu, Bakari Shime alisema amewaambia wachezaji wake kusahau ushindi uliopita na sasa nguvu na katika mechi ya wikiendi hii.




OHOOO! GOR MAHIA WAINGIA MZIGONI NA SIMBA KUMUWANIA MAVUGO



Baada ya Klabu ya Simba kutangaza kutaka kumsajili straika Mrundi, Laudit Mavugo, mabingwa mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia, nao wameingia kati wakiitaka saini ya straika huyo.

Simba ambayo msimu uliopita ilimkosa Mavugo dakika za mwisho, tayari imeanza mchakato wa kumnasa straika huyo huku ikitajwa Wekundu hao wa Msimbazi wameweka mezani kitita cha dola 50,000 (zaidi ya Sh milioni 100).

Mtandao wa Soka25east.com wa Kenya, umeripoti kuwa, Gor Mahia maarufu kwa jina la K’Ogalo, ipo kwenye mikakati ya kumnasa Mavugo ambaye tayari ametangaza kuondoka Vital’O ya Burundi.

Hata hivyo, Rais wa Vital’O, Benjamin Bikorimana amesema bado anaamini Mavugo ataendelea kuwepo klabuni hapo na kuipigania timu yake kuzidi kupata mafanikio.

Wakati huohuo, Mavugo amenukuliwa akisema: “Nataka kuondoka hapa Burundi na kwenda kucheza soka la kulipwa kwani hiyo ndiyo ndoto yangu.”

Mavugo ambaye aliwahi kuzichezea timu za Kiyovu, AS Kigali na Police FC, huu ni msimu wake wa pili ndani ya Vital’O huku akiwa amefunga jumla ya mabao 60 kwa kipindi chote hicho.


Upande wa Simba kumekuwa na taarifa kuwa kuna uwezekano wa Mavugo kutua nchini muda wowote kuanzia leo kwa kuwa wamefikia pazuri katika mazungumzo yao.

OMOG ALIVYOTUA NCHINI USIKU NA LEO ANASAINI MKATABA WA KUINOA SIMBA


Kocha Joseph Omog tayari ametua nchini kwa ajili ya kumalizana na uongozi wa klabu ya Simba.

Omog raia wa Camerooon amewasili saa 9 alfajiri akitokea kwao Cameroon tayari kumalizana na Simba leo.


Omog aliyeipa ubingwa Azam FC mwaka 2014, anatarajia kuanza kuinoa Simba rasmi ndani ya siku tatu ikiwa ni baada ya kuingia mkataba leo.

Kocha Jackson Mayanja raia wa Uganda ambaye alikuwa na kikosi msimu uliopita, atakuwa msaidizi wake.

UGAIDI WACHANGIA YANGA KUAMUA KUBADILI KAMBI YA UTURUKI



Tukio la shambulio la kigaidi kwenye Uwanja wa Ndege wa Ataturk mjini Istanbul, Uturuki limebadili mipango ya Yanga kwenda kuweka kambi nchini huko kubadilika na badala yake inajipanga kwenda Pemba.

Yanga ilikuwa Antalya, Uturuki ilipoweka kambi kujiandaa na michezo yake miwili ya Kombe la Shirikisho, ikaahidi kurejea Uturuki baada ya mechi dhidi ya TP Mazembe, Jumanne ya wiki hii lakini sasa imebadili uamuzi.

"Timu itaondoka kesho (leo) kuelekea Pemba kwa ajili ya kambi ya muda kujiandaa na mechi na Medeama ambayo ni muhimu kwetu kupata ushindi ili hesabu ziende sawa.

"Sisi tulichopanga ni kushinda michezo yote iliyobaki ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupoteza michezo miwili dhidi ya MO Bejaia na Medeama.

"Maamuzi hayo ya kambi ya Pemba yametokana na tukio kubwa la kigaidi lililofanywa huko Uturuki, hivyo kiusalama tumeona ni vema tukabaki nchini," alisema mtoa taarifa wetu.


Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro kuzungumzia hilo alisema: "Kambi yetu tutaitangaza wakati wowote wapi tutakapokwenda, hivyo subirieni kwanza tutawajulisha.”

-------------------------------------------------------

-------------------------------------------------------
HABARI MPYAMPYAhttp://2.bp.blogspot.com/-mFnDPXvIysA/VOZH1z-2rpI/AAAAAAAAADs/shOR30FtkF4/s1600/anigif.gif