Na Ram Mbegeze
Kamati ya maadili na sheria ya FIFA imetuma maombi ya kutaka aliyekuwa msaidizi wa Mohamed bin Hammam afungiwe kifungo cha maisha kujihusisha na soka kutokana na uchunguzi wa rushwa kwenye soka unaomhusu.
Kamati hiyo ya maadili ya FIFA imesema hayo jana Jumatano kuwa uchunguzi wake kwa Najeeb Chirakal “ulilenga malipo yaliyofanywa kwa watendaji kadhaa wa soka duniani.”
Pia ilipendekeza kuwa majaji wa maadili na sheria wa FIFA kuweka sheria mpya ya kifungo cha maisha kwa kesi zote zinazohusu hongo na rushwa, ahadi za zawadi, migongano ya kimaslahi na kushindwa kwa maafisa kutoa ushirikiano kwa wachunguzi.
Chirakal aliishi sana nchini Qatar na alikuwa mfanyakazi wa Bin Hammam, moja ya watendaji wenye nguvu waliowahi kuwepo ndani ya FIFA na Rais wa chama cha soka cha bara la Asia ambaye alipewa kifungo cha maisha na FIFA mwaka 2012.
Bado haijawekwa wazi ni lini kamati ya majaji ya FIFA itakutana kutoa maamuzi ya kesi hii lakini mara nyingi huchukua wiki kadhaa.
Chirakal aligundulika hapo nyuma kupitia machapisho ya jarida la Uingereza,The Sunday Times na ripoti ya Pricewaterhouse Coopers kuhusiana na taarifa za kifedha za chama cha soka cha bara la Asia ikiwa ni ya mahusiano ya watendaji wa bara la Afrika na Asia kuhitaji fedha kutoka kwa Bin Hammam.
Mwezi Oktoba 2012, Chirakal alisimamishwa kupisha uchunguzi na mahakama ya maadili ya FIFA kutokana na kushindwa kutoa ushirikiano kuhusiana na sakata la Bin Hammam.
Akiwa kama msaidizi wa Bin Hammam aliombwa kutoa taarifa rasmi na nyaraka lakini akashindwa kufanya hivyo.
Kamati ya maadili ya FIFA ilimwondoa Bin Hammam kwa mara ya pili mwezi Desemba 2012 kutokana na usimamizi mbovu wa kifedha wa chama cha soka Asia (AFC), ambayo ilitoka katika taarifa iliyovujishwa ya ukaguzi wa mahesabu iliyofanywa na shirika la uhasibu linalofahamika kama PwC.
Ripoti hiyo ilimhusisha Chirakal na washirika wengine wa Rais huyo waliokuwa kwenye mlolongo wa kujihusisha na viongozi wa vyama vya soka barani kama Amadou Diallo, waliokuwa wakiomba fedha kutoka kwa Bin Hammam, ambaye alikuwa anatumia utajiri wake binafsi kuhonga. Diallo alihusishwa na kashfa ya mwaka 2011 kutokana na kupata fedha zisizo halali katika kampeni iliyofanikiwa ya Qatar kupata uenyeji wa kombe la dunia mwaka 2022.
Bin Hammam alifungiwa mara ya kwanza na FIFA mwaka 2011 kutokana na malipo yasiyokuwa halali kwa wapiga kura kutoka Caribbean wakati anagombea urais wa FIFA dhidi ya Sepp Blatter. Kifungo hicho cha maisha kilifutwa na mahakama ya masuala ya kimichezo.
No comments:
Post a Comment