Utawala wa Barca katika Copa del Rey: Enrique na Messi wanaiwinda rekodi iliyodumu miaka 64

FC Barcelona wanatengeneza rekodi katika kila msimu wa Copa Del Rey. Baada ya kuwaondoa Atletico Madrid katika nusu fainali jana usiku, timu hii sasa imefika hatua ya fainali ya michuano hiyo kwa mara ya 4 mfululizo na mara ya 38 katika historia.
Luis Enrique sasa amefanikiwa kuiingiza Barca mara 3 katika misimu yake mitatu aliyokaa Camp Nou – rekodi ambayo Fernando Daucik pekee ndio alifanikiwa kabla na kikosi cha Barca kutoka 1951 mpaka 1953. Kocha huyu Mslovenia, akiwa na timu iliyoongozwa na nahodha Kubala, alishinda makombe yote matatu katika fainali za Copa Del Rey na sasa miaka 64 baadae Luis Enrique ana nafasi ya kuifikia rekodi hiyo ya vikombe hivyo na timu inayoongozwa na LaPurga Messi.
Barca wamefikia hatua hii ya fainali mara 7 katika misimu 9 iliyopita na ndio timu iliyoshinda kikombe hiki mara nyingi zaidi katika historia – mara 28. 
Pep Guardiola alifika fainali ya Copa mara 3 na kushinda mara mbili, wakati Tata Martino alifika mara 1.
Barcelona sasa anamsubiri mshindi wa nusu fainali ya leo kati ya Alaves vs Celta Vigo ili kucheza nae fainali ya michuano hii.