Klabu ya Simba imemzuia kiungo wao Said Ndemla kwenda kufanya majaribio kwenye klabu moja ya nchini Sweden iliyomuhitaji Ndemla kwa ajili ya kumfanyia majaribio.
Makamu wa Rais wa klabu hiyo Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amefafanua kwa nini Simba hawajamruhusu Ndemla kwenda nchini Sweden kufanya majaribio kwenye klabu inayomuhitaji.
“Sasa hivi Simba ipo kwenye mapambano ya ubingwa, kulingana na mahitaji Ndemla ni machezaji ambaye mwalimu atamuhitaji zaidi. Ukiangalia katika wiki mbili zilizopita ameweza kucheza karibu muda wote kwa maana hiyo kwa sasa hatupo kwenye kipindi cha usajili kwa hiyo endapo ataondoka kwa sasa hatuwezi kupata mbadala.”
“Mwalimu ameona ni jambo jema kama ataendelea kucheza na kama kutatokea mahitaji yoyote basi klabu itaweza kufanya mazungumzo ya awali na timu husika ili baada ya ligi kuisha aweze kuruhusiwa kwenda kufanya majaribio hayo.”
“Au kama kutakuwa na lolote hapa katikati kutoka kwenye benchi la ufundi basi tutaweza kufanya hivyo.”
Said Ndemla ni miongoni mwa wachezaji walioonesha uwezo mkubwa kwenye game ya Majimaji 0-3 Simba na kufanikiwa kufunga goli moja katika mchezo huo. Tangu kuanza kwa msimu huu, Ndemla amekuwa hapati nafasi ya kucheza mara nyingi kwenye kikosi cha kwanza cha Simba.