Friday, February 6, 2015

AGREY MORIS NA NYOSO WAFUNGIWA

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh0ZdxtW3H5O4L2BBdcDhqoFzeu7sM3YTnMdDUh5ZtA492HBatbDFY9T6bEdxTU31rQ_6mbVfOEJ4lyzRgmNpAeZi7v4YHweGRx29sln2dWa6WczzGfgl6_SkF9Zr3epgqpWJPK8dskEk5g/w93-h140-p/Nyosso+%25282%2529.JPG
Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewafungia kati ya mechi tatu na nane wachezaji Juma Nyosso wa Mbeya City na Aggrey Morris wa Azam kutokana na makosa ya kinidhamu waliyoyafanya wakiwa uwanjani. Nyoso ambaye alilalamikiwa na TFF kwa kumfanyia vitendo vya udhalilishaji mshambuliaji Elias Maguri wa Simba amefungiwa mechi nane za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).


 Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Ibara ya 57 na Ibara ya 11 (f) ya Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012. Akiwa mbele ya Kamati hiyo jana (Februari 5 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, Nyosso alikiri kufanya na kujutia kosa hilo, pia amemuomba radhi mchezaji Maguri kwa kitendo hicho. Akisoma uamuzi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wakili Jerome Msemwa alisema kitendo kilichofanywa na Nyosso ni kosa kubwa, kudhalilisha utu wa mtu, na ni mfano mbaya kwa watoto na jamii nzima ya mpira wa miguu.

 Naye Morris amefungiwa mechi tatu za VPL baada ya kutiwa hatiani kwa kumpiga mshambuliaji Emmanuel Okwi wakati timu hizo zilipopambana kwenye mechi ya ligi iliyochezwa Januari 25 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kabla ya kusoma uamuzi, Wakili Msemwa alisema mlalamikiwa Morris alikiri kugongana na Okwi, kwa maelezo kuwa aliingia kwenye 'reli' ndiyo ukatokea mgongano huo.

 Kamati baada ya kupitia malalamiko ya klabu ya Simba, ripoti za Brain CT scan kutoka Besta Diagnostic Centre na nyingine kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), taarifa za madaktari zilionyesha Okwi aligongwa kichwani akiwa anacheza mpira na kuzimia kwa dakika tano, pia mkanda wa video uliowasilishwa na TFF imeona kulikuwa na kugongana kati ya wachezaji hao.

 Hivyo, Kamati ikamtia hatiani Morris kwa kutumia Ibara ya 48(1)(d) ya Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012 kwa kumfungia mechi hizo tatu na kumpa onyo kali. Pia Kamati hiyo imemfungia miezi sita na kumpiga faini ya sh. 200,000 Meneja Vifaa (Kit Manager) wa timu ya Polisi Mara, Clement Kajeri kwa kuhamamisha vurugu na kuwapiga waamuzi kwenye mechi dhidi ya Mwadui iliyochezwa Uwanja wa Karume mjini Musoma. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 40(2) ya Ligi Daraja la Kwanza. Wachezaji watatu wa Friends Rangers; Mahmoud Othman, Khalid Twahil na John Alexander wamefungia miezi sita na faini ya sh. 500,000 kila mmoja kwa kumpiga mwamuzi kwenye mechi ya Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Majimaji. Licha ya wachezaji hao kuitikia mwito wa Kamati, wachezaji hao walizuiwa na viongozi wa kuingia ukumbini wakati malalamiko dhidi yao yalipoanza kusikilizwa.

 Hatua hiyo iliifanya Kamati ifanye uamuzi baada ya kuusikiliza upande wa walalamikaji pekee. Shauri dhidi ya mchezaji George Michael wa Ruvu Shooting kwa kumchezea ubabe Amisi Tambwe wa Yanga, Kamati imeliahirisha baada ya mlalamikiwa kupata udhuru uliosababisha asiwepo. Pia Kamati ya Nidhamu imeelekeza malalamiko ya timu ya Friends Rangers kupinga refa kuchezesha mechi yao dhidi ya Majimaji kwenye mvua kubwa, kutoa maamuzi yasiyo halali na kutokuwepo na ukweli kwenye ripoti ya Kamishna yakasikilizwe na Bodi ya Ligi kwa vile si masuala ya kinidhamu.

No comments:

Post a Comment

-------------------------------------------------------

-------------------------------------------------------
HABARI MPYAMPYAhttp://2.bp.blogspot.com/-mFnDPXvIysA/VOZH1z-2rpI/AAAAAAAAADs/shOR30FtkF4/s1600/anigif.gif