Saturday, December 5, 2015

Sababu za Messi kupewa Tuzo ya Mshambuliaji Bora La Liga na Kwanini Naamini Neymar na CR7 hawastahili kuwemo Top 3 Ballon D’Or

Sababu za Messi kupewa Tuzo ya Mshambuliaji Bora La Liga na Kwanini Naamini Neymar na CR7 hawastahili kuwemo Top 3 Ballon D’Or

kama tunavyojua wiki hii kulitolewa tuzo mbalimbali za Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ kwa msimu uliopita. Mojawapo ni ile ya mshambuliaji bora wa msimu ambayo ilichukuliwa na staa wa Barcelona, Lionel Messi. 
Kati ya tuzo zilizotolewa, kipa bora, beki bora na kocha bora na nyinginezo, lakini kidogo hii ya Messi imezua mjadala wa aina yake.
Wapo wanaoamini ilimfaa mpinzani wake wa karibu, Cristiano Ronaldo wa Real Madrid, wakiegemea katika hoja ya kutwaa tuzo ya ufungaji ambapo alimzidi Messi. Ni kweli, Ronaldo alifanya kweli katika ishu ya kucheka na nyavu, kwani alimaliza msimu akiwa na hat trick nane, dhidi ya tano za Messi.
  Ni dhahiri unapozungumzia sekta ya ufungaji bora, Ronaldo ama CR7 kama anavyofahamika, alistahili kuchukua tuzo hiyo, lakini kuna kitu kinachowachanganya wengi. Unapozungumzia mfungaji bora na mshambualiji bora ni vitu viwili, ingawa wote wanaweza kuwa na jukumu la kufunga.
Mshambuliaji bora ni aina ya mchezaji anayetegemea mfumo wa timu na mfumo wa kocha na ili afunge lazima awe kwenye muunganiko wa timu na kushiriki katika mipango yote ya kupatikana kwa bao. Hii ni sifa kuu inayowatofautisha watu hawa. Mfungaji bora yeye anaweza kujitegemea katika kulitafuta bao na asishiriki katika upatikanaji wa mpira hadi kufika langoni mwa mpinzani.
Ni kutokana na aina hizo, tunapata aina mbalimbali za washambualiji. Kuna wale ambao huitwa washambuliaji waliokamilika ‘complete strikers’, hawa hufanya kazi zote kulingana na mfumo na hushiriki kikamilifu katika kuisaidia timu kuanzia kuitafuta mipira mpaka kupatikana kwa bao. Hapa utakutana na watu kama Luis Suarez, Messi, Sergio Aguero.

Takwimu za Ufungaji za Messi na Ronaldo msimu uliopita
Wapo wale waitwao waviziaji (poachers), hapa unakutana na kina Javier Hernandez ‘Chicharito’ Filippo Inzaghi, Ruud van Nistelrooy. Pia kuna kundi la washambuliaji wao kazi yao ni kumalizia mipira langoni (target man) hapa wamo kina Oliver Giroud, Peter Crouch, Fernando Torres, Gonzalo Higuain na wengineo. Matumizi yao uwanjani ni tofauti na kariba ya ushambuliaji wa kina Messi.
 Kuna vitu vya kumuangalia mshambuliaji bora kama straika nini majukumu yake uwanjani kama kufunga. Kulingana soka la kisasa (modern football), straika kwa sasa ni zaidi ya kufunga. Kuna wakati eneo ambalo upo unaangalia jinsi ya kuisaidia timu yako na siyo suala la kufunga mabao wewe mwenyewe, ila mchango wako kikosini kwa jumla, achilia mbali kufunga kwako.
Ndiyo maana Jose Mourinho amekuwa akilumbana na Diego Costa, siyo kusema anashindwa kufunga tu, ila anaangalia mchango wake uwanjani katika kuisaidia Chelsea hasa kipindi hiki kigumu kwao.
Majukumu ya Messi si kuwa kama straika tu ndani ya Barcelona, ila uwezo wa kutoa asisti na uwepo wake kwenye safu ya ushambuliaji husaidia sana wenzake kufunga kiurahisi.
Mathalan angalia bao linalowania tuzo ya Puskas, anatoka katikati ya uwanja, anachambua mchezaji hadi mchezaji na kutupia mpira kambani. Hayo ndiyo mahitaji ya mshambuliaji katika soka la kisasa.

Matokeo ya kura zilizompa Messi tuzo ya Ushambuliaji Bora
Hivyo, Messi amekamilika, kulinganisha na CR7 ambaye kweli anajua kufunga lakini hajakamilika kwa mantiki ya mahitaji ya soka la kisasa. Hata takwimu zinaonyesha Messi alimaliza msimu akiwa na asisti 18 dhidi ya 16 za CR7
Pia  nigusie kuhusu tuzo ya mchezaji bora wa dunia, Messi, CR7 na Neymar. Kwa mtazamo wangu, sioni kama CR7 alitakiwa kuingia safari hii, ukilinganisha na wengine walivyofanya vizuri. Ninaamini ilikuwa ni fursa kwa mmoja wa Juventus alitakiwa kuwemo katika majina haya.
Hakuna aliyekubali kuwa msimu uliopita Juve ilikuwa katika ubora wake na kweli walistahili kutoa mchezaji mmojawapo katika kinyanganyiro hiki. kati ya Paul Pogba ama Arturo Vidal mmojawapo alitakiwa kuingia.
 Mimi ni shabiki mkubwa wa Ronaldo, sidhani kama alistahili kuingia kulinganisha na wenzake walivyofanya mengi mazuri.
Niliwaangalia Neymar na Luis Suarez, siamini kama Neymar alitakiwa kuwemo mbele ya Suarez, labda pengine kwa kuwa Suarez alikuwa na adhabu kwa timu ya taifa. Suarez ana mchango mkubwa tena sana kuliko Neymar ambaye naweza kusema wanajaribu kupewa promo na makampuni makubwa kwa ajili ya kujitangaza kwa tija ya biashara nchini Brazil, lakini vinginevyo hakustahili mbele ya Mruguay huyo.
Ila kama ilikuwa sababu ya adhabu ya kinidhamu kwa Suarez, Neymar anastahili kuwemo lakini kwa mtazamo wangu, Ronaldo angetoka na kuingiza jina mojawapo kati ya Vidal ama Pogba kutokana na mafanikio makubwa waliyokuwa nayo msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment

-------------------------------------------------------

-------------------------------------------------------
HABARI MPYAMPYAhttp://2.bp.blogspot.com/-mFnDPXvIysA/VOZH1z-2rpI/AAAAAAAAADs/shOR30FtkF4/s1600/anigif.gif