Thursday, June 30, 2016

KAMA ZALI MWANANGU, URENO NA RONALDO WATINGA NUSU FAINALI EURO KWA KUICHAPA POLAND KWA PENATI 5-3


Unaweza kusema kama zali mwanangu, maana Ureno iliyokuwa inaonekana itaishia hatua ya makundi ya Kombe la Euro, leo imetinga nusu fainali.

Ureno inayoongozwa na nahodha wake Cristiano Ronaldo imetinga nusu fainali kwa kuibandua Poland kwa mikwaju 5-3 ya penalti.

Changamoto ya mikwaju ya penalti ilipewa nafasi baada ya sare ya bao 1-1 katika dakika 90 na baadaye 120.

Poland starting XI: 
Fabianski, Piszczek, Glik, Pazdan, Jedrzejczyk, Blaszczykowski, Krychowiak, Maczynski (Jodlowiec), Grosicki (Kapustka), Milik, Lewandowski

Portugal starting XI:
Rui Patricio, Cedric, Pepe, Fonte, Eliseu, William Carvalho (Danilo), Joao Mario (Quaresma), Renato Sanches, Adrien Silva (Moutinho), Nani, Ronaldo









Tuesday, June 28, 2016

Sunday, June 26, 2016

ALEXIS SANCHEZ MWANASOKA BORA WA COPA AMERICA



Mshambuliaji nyota wa Arsenal, Alexis Sanchez ametangazwa kuwa mwanasoka bora wa michuano ya Copa America.


Sanchez ambaye ameiwezesha timu yake ya taifa ya Chile kubeba kombe hilo kwa mara nyingine tena, amewapiku nyota wengine wengi wakiwemo Lionel Messi, Angel Di Maria na wengine wengi.

MAGURI ASAINI OMAN MIAKA MITATU, SASA NI MCHEZAJI WA DHOFAR SC


Aliyekuwa mshambuliaji nyota wa Stand United, Elias Maguri amesaini mkataba wa miaka mitatu wa kuitumikia Dhofar SC ya nchini Oman.
Maguri ambaye alionyesha kiwango cha juu msimu uliopita kabla hajaanza kutoelewana na uongozi wa benchi la ufundi la timu hiyo, alisaini mkataba huo jana.
Klabu hiyo ndiyo wawakilishi wa Oman katika michuano ya Bara la Asia, hivyo hii itampa Maguri nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa zaidi.

Awali alikuwa akiwindwa na timu kadhaa ikiwemo Simba ya jijini Dar es Salaam lakini alishindwa kujiunga nazo na kutimkia nchini Oman.
Kabla ya kwenda kwenye timu hiyo, Maguri ambaye alitoka Simba kabla ya kujiunga na Stand aliwahi kufanya majaribio kwenye timu ya TP Mazembe na kusema kuwa amefanikiwa kufuzu, ingawa klabu yake ilimgomea  kwa kuwa hakufuata utaratibu wakati wa kwenda kwenye majaribio hayo.

Msimu uliopita mshambuliaji wa huyo wa Taifa Stars, aliifungia timu yake mabao 15 na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Amissi Tambwe (21), na Donald Ngoma (17).

SIMBA YAMUWEKEA OMOG NAFASI YA KUFANYA USAJILI




Pamoja na kuendelea na usajili, klabu ya Simba imeweka nafasi kwa ajili ya kocha wake mpya ambaye kwa asilimia 95 atakuwa Joseph Omog.

Omog raia wa Cameroon aliyewahi kuipa ubingwa Azam FC, amekubaliana na Simba kila kitu na inaonekana ndiye atakuwa kocha mpya wa Simba kwa kuwa kocha Mghana, Tetteh anaonekana kutokuwa tayari kujiunga na Msimbazi.

“Unajua kocha anapokuja, lazima naye atakuwa na mawazo yake kuhusiana na suala la usajili.

“Pamoja na kufanya usajili, lakini kocha naye atawekewa nafasi kwa wachezaji wa kigeni pamoja na wale wa ndani,” kilieleza chanzo.

“Hii maana yake pamoja na usajili huo ambao ulifanywa na kamati ya ufundi na usajili, mwalimu naye anakuwa na nafasi ya kusajili pia.”


Simba inatarajia kuanza mazoezi rasmi kesho au keshokutwa kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya.

SERENGETI BOYS YAANZA VIZURI KUWANIA AFRIKA, YAITWANGA SHELISHELI MABAO 3-0




 Timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys imeanza vema katika kuwania nafasi ya kushiriki michuano ya Afrika ya vijana chini ya miaka 17 baada ya kuitwanga Shelisheli kwa mabao 3-0.

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Segengeti Boys ingeweza kupata mabao mengi zaidi kama washambuliaji wake wangekuwa makini.

Hata hivyo, walipoteza nafasi nyingi sana na baadaye walionekana kuridhika na ushindi huo.



ATUPELE WA 'KIJANI' AICHA NDANDA FC, ATUA KATIKA KIKOSI CHA WANAJESHI



Mshambuliaji Atupele Green amejiunga na JKT Ruvu kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu.

Green ambaye alikuwa anakipiga Ndanda FC msimu uliopita, msimu ujao ataonekana akiwa na JKT iliyorejea Ligi Kuu Bara.

Tayari kila kitu kimekwenda safi baada ya Green au wa Kijani kumalizana na timu hiyo ya jeshi.




TFF YATOA ONYO, YASEMA YANGA ITAONDOLEWA MASHINDANONI NA CAF


RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI NA RAIS WA CAF, ISSA HAYATOU WAKIWA PAMOJA
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limepokea taarifa juu ya mpango na kauli za baadhi ya viongozi wa Young Africans SC kushawishi mashabiki wao kufanya vurugu dhidi ya warushaji matangazo ya televisheni ya moja kwa moja wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho la Afrika ngazi ya Makundi kati ya Young Africans ya Tanzania na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) utakaofanyika Juni 28, 2016 saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Dar es Salaam.
TFF ikiwa msimamizi mkuu wa mpira wa miguu Tanzania, inawajibika na mara moja inachukua nafasi hii kuwatahadharisha baadhi ya viongozi wa Young Africans, wanachama na mashabiki wao kutofanya hivyo kwani itakuwa ni kinyume na  kanuni za mashindano na mikataba ya udhamini katika hatua hii.
Ikumbukwe kwamba CAF inamiliki asilimia mia moja ya haki za habari na masoko katika ngazi hii ya makundi na jaribio lolote la kukwamisha matangazo ya biashara au utengenezaji na urushaji wa matangazo ya televisheni au ukwamishaji wa shughuli zingine kama hizo kwa CAF au wakala aliyeteuliwa na CAF kutaigharimu klabu mwenyeji si kwa kutozwa faini tu lakini pia uwezekano wa kuondolewa mashindanoni.
Pia TFF inatoa tahadhari hiyo ikiwamo ile ya utamaduni wa kukaa uwanjani ili kuepusha aina yoyote ya vurugu kwenye michezo yake hususani hii ya hatua ya makundi. TFF inafahamu kuwa tayari viongozi wa Young Africans walikwisha kusoma nyaraka na taarifa mbalimbali kuhusu kanuni na masuala ya udhamini kwa timu zinazofuzu hatua ya Nane Bora.Wapenzi wa Yanga wanaombwa kufika kwa wingi na kuishangilia kwa nguvu  timu yao ikiwa ni njia ya kuitia hamasa.Hata hivyo shamrashamra hizo zifanyike kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu za Mpira wa Miguu na sheria za nchi.
Vitendo vya kuashiria vurugu na kufanya vurugu vikithibitishwa katika taarifa ya Mwamuzi, Janny Sikazwe wa Zambia; Kamishna wa mchezo, Celestin Ntangungira wa Rwanda na Mratibu Mkuu Maalumu kutoka Msumbiji, Sidio Jose Mugadza, hatua zake zitachukuliwa dhidi yake ikiwamo KUONDOLEWA KWENYE MASHINDANO. Vilevile vitendo vya kutishia amani,kudhuru mwili au kuharibu mali vitachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za kijinai.
Katika mchezo huo wa kimataifa Na. 107, Mwamuzi Sikazwe atasaidiwa na Jarson Emiliano dos Santos kutoka Angola atayekuwa kwenye mstari wa kulia (line 1) na Berhe O’Michael wa Eritrea atayekuwa upande wa kushoto (line 2) huku Wellington Kaoma wa Zambia akiwa ni mwamuzi wa akiba.
Wakati huohuo, kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini kinatarajia kukaa siku ya Jumamosi tarehe 2 Julai 2016. Taarifa zaidi itatolewa karibuni.

Saturday, June 25, 2016

KATIBU MPYA WA SIMBA AMEAHIDI MAMBO MAKUU MAWILI KWA MASHABIKI



img_9676.jpg
Patrick Kahemele amesaini mkata wa miaka miwili kuitumikia Simba kama Katibu Mkuu wa klabu hiyo baada ya mabingwa hao wa zamani kukaa kwa muda mfefu bila kuwa na mtendaji mkuu wa shughuli za klabu yao.
Kahemele ameahidi mambo makuu mawili katika uongozi wake wa miaka miwili ndani ya Simba. Jambo la kubwa na kwanza ni kuifanya Simba ijitegemee na kuacha kutegemea mifuko ya watu wachache lakini huu ukiwa ni mpango wa muda mrefu. Jambo la pili ni kuisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara ilioukosa kwa misimu minne sasa.
“Simba ni timu kubwa, imekuwa na hamu ya mafanikio ndani ya uwanja na nje ya uwanja. Tukizungumza nje ya uwanja, klabu inahitaji kujitegemea na naamini wana Simba wana mawazo mengi, kikubwa ni kukaa na kushirikiana tuweke mawazo yetu pamoja na kuona ni jinsi gani tunaweza tukaikwamua klabu ya Simba kutoka kutegemea mifuko ya watu wachache hadi kuwa klabu inayojitegemea na kusimama yenyewe,” amesema Kahemele ambaye ataanza majukumu yake ya kazi Julai 1 mwaka huu.
“Hiyo ni mipango ya muda mrefu katika kipindi cha miaka miwili ningependa nifanikishe hilo ambalo hata nikiondoka mimi pamoja na viongozi wenzangu tunakuwa tumefanya kitiu flani. Lakini la msingi kabisa ni kuhakikisha msimu ujao lazima ubingwa uende Msimbazi kwasababu Simba ni timu ambayo imezoea kushinda vikombe lakini kazi hiyo inaanzia kwenye usajili, lazima tuwe na timu nzuri, benchi la ufundi zuri, timu ipate kambi na huduma nzuri na vyote hivyo vikiwekwa pamoja hakuna linaloshindikana.”
Anatoa neno kuhusu mashabiki wa ‘mnyama’
“Mashabiki wa Simba ni wastaarabu sana, sijawahi kuona mashabiki wa Simba wakitia presha, mashabiki wa Simba wakikupa shida ujue umewakosea lakini kama hujawakosea hawana shida kabisa.”

KESSY ATACHEZA DHIDI YA MAZEMBE? TFF IMETOA UFAFANUZI


Kessy-Algeria
Shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia msemaji wake, Alfred Lucas limesema kuwa, linashughulikia sakata la uhamisho wa mchezaji Hassan Kessy Ramadhani kutoka Simba kwenda Yanga ili aweze kucheza kwenye mchezo wa kimataifa kati ya Yanga dhidi ya TP Mazembe unaotarajiwa kuchezwa siku ya Jumanne June 28 kwenye uwanja wa taifa.
“Tayari Yanga wameshaandika barua imekuja TFF wakiomba suala la Kessy liweze kumalizwa haraka ili waweze kumtumia kwenye mchezo wao wa Jumanne dhidi ya TP Mazembe,”amesema Alfred Lucas afisa habari wa shirikisho la soka Tanzania.
“Niwahakikishie mashabiki wa Yanga kwamba TFF weekend yote hii kwa maana ya leo Jumamosi na Jumapili tutalifanyia kazi hilo na tayari mawasiliano yameshafanyika ili Yanga waanze kumtumia mchezaji huyu mara baada ya mkataba wake kuisha.”
“Lakini kama kuna kikwazo chochote tunajaribu kufikiria ili Yanaga wawe huru kusiwe na dosari yeyote kwenye michuano hii halafu sababu ikawa ni kuwakosa wachezaji wake wote iliyowasajili kwa ajili ya michuano hiyo.”
“Naamini kwa uungwana waliokuwa nao Simba kama kuna kikwazo watakiondoa ili mchezaji huyo aendelee kipaji chake na maisha mengine yaendelee.”
Kessy hakuruhusiwa kucheza kwenye mchezo wa kimataifa kati ya Yanga dhidi ya MO Bejaia kwasababu kibali chake kutoka Simba kwenda Yanga kilikuwa hakijathibishwa.

PAUL SCHOLES ASAINI MKATABA KUCHEZA SOKA INDIA


Scholes

Mchezaji wa zamani wa Manchester United na England Paul Scholes amesaini mkataba wa miaka mitatu kucheza kwenye ligi ya Premier Futsal nchini India. Mchezaji huyu wa Man United amatajwa kuwa mmoja wa nyota watakaocheza ligi hiyo pamoja na Deco.
Huu utakuwa msimu wa kwanza wa ligi hii mpya ambayo itahusisha kuchezwa kwa aina ya mchezo wa mpira wenye sheria tofauti .
Mchezo huu unachezwa na wachezaji watano pekee kwa kila timu pia utumia mpira mdogo zaidi, unaodunda zaidi na unachezwa ndani na si uwanjani kama ilivyozoeleka.
“Futsal ni mchezo unaofurahisha, na umetoa mchango mkubwa sana katika kukuza vipaji vya wachezaji wakubwa zaidi kuwahi kutokea,” alisema Scholes.
“Premier Futsal ni njia nzuri sana ya kutambulisha mchezo wa mpira India, na nasubiri kwa hamu sana kupata nafasi ya kuwasilimia mashabiki wote nchini India ambao najua ni kati ya mashabiki bora zaidi duniani.”
Mchezaji wa zamani wa Barcelona Deco na wachezaji mbalimbali wengine wa mchezo wa Futsal wameshasaini mkataba kucheza ligi hii na waandaji wa ligi hii wameahidi kwamba majina mengine makubwa lukuki yatajiunga na ligi hii hivi punde.
“Tangu tuzindue ligi yetu tulisema kwamba tunatia jitihada kuleta vipaji mbalimbali nchini India na kama inavyonekana kweli tunatimiza ahadi yetu.”
Scholes 41, alifanikiwa kushinda ubingwa wa Ligi mara 11 na klabu ya Manchester United pamoja na ligi ya mabingwa 2 akiwa klabu ya Manchester United kabla ya kustaafu mwaka 2013.
Raisi wa Ligi hii ni Luis Figo mchezaji wa zamani wa Real Madrid na Barcelona.

OSCAR JOSHUA ARUDISHA MATUMAINI, AANZA KUJIFUA UTURUKI




Yanga itakuwa dimbani Jumanne ijayo kuwavaa TP Mazembe katika mechi ya Kundi A ya Kombe la Shirikisho Afrika linaloandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) dhidi ya TP Mazembe, hofu kubwa ya timu hiyo ni beki ya kushoto.

Wachezaji wawili wanaocheza nafasi hiyo, Haji Mwinyi na Oscar Joshua wote wapo katika hatari ya kuikosa mechi hiyo, hivyo Yanga ipo katika wakati mgumu wa nani acheze nafasi hiyo.

Mwinyi yeye ana kadi nyekundu aliyoonyeshwa katika mchezo uliopita wa michuano hiyo dhidi ya MO Bejaia ya Algeria wakati Joshua ana maumivu ya nyama za paja, pia aliyapata katika mchezo huo.

Habari njema kwa Yanga ni kwamba, Joshua tayari ameanza mazoezi mepesi kambini huko mjini Antalya, Uturuki ambako timu hiyo imejichimbia kujiandaa na mechi dhidi ya TP Mazembe.

Kutoka Uturuki, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema: “Joshua anaendelea vizuri na tayari ameanza mazoezi mepesi kwa ajili ya kujiandaa na mechi na Mazembe.

“Bado sijajua hatma yake kama atacheza au hatocheza mechi na Mazembe, hivyo kila kitu kitajulikana ikiwa imebaki siku moja kabla ya mchezo wao baada ya daktari wetu Edward Bavo kutoa ripoti yake.”

Joshua alipata majeraha hayo usiku wa Jumapili iliyopita dakika ya 32 katika mchezo dhidi ya MO Bejaia mjini Bejaia, Algeria ambapo ilibidi atolewe na nafasi yake kuchukuliwa na Mwinyi. Katika mchezo huo, Yanga ilifungwa bao 1-0.

JEMBE LIMEREJEA UWANJANI, NI JUMA ABDUL, APIGA DAKIKA ZA FULL GAME MAZOEZINI


JUMA ABDUL
Yanga huenda ikashusha pumzi kidogo katika nafasi ya beki ya kulia kwani Juma Abdul ameanza mazoezi ya nguvu na jana Ijumaa asubuhi alicheza dakika 90 uwanjani.

Abdul aliumia kifundo cha mguu katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA dhidi ya Azam FC hivi karibuni ambapo Yanga ilishinda mabao 3-1, siku alipoumia nafasi yake ilichukuliwa na Mbuyu Twite.

Alitibiwa na kupata nafuu lakini akajitonesha katika mchezo wa Taifa Stars na Misri wa kufuzu Kombe la Afrika 2017 na tangu hapo hakuonekana uwanjani, ambapo alikuwa akiuguza jeraha hilo.

Baada ya kufanya mazoezi ya ufukweni kwa wiki nzima, jana Abdul alifanya mazoezi ya uwanjani kwenye Uwanja wa Garden uliopo Vijana, Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo alitumia dakika 90.

SALEHJEMBE ilimshuhudia Abdul akianza na zoezi la kukimbia akizunguka uwanja mara 20 kabla ya kucheza uwanjani.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Abdul alisema: “Nipo fiti kabisa na ninaweza kucheza mechi na TP Mazembe, wiki nzima nilikuwa na programu ya mazoezi ya stamina katika Ufukwe wa Coco.

“Leo (jana) ndiyo nimeanza kucheza uwanjani na nimetoka freshi kabisa na sina shaka hata nikipewa mechi ya Mazembe.”

Wakati wenzake wakiwa kambini Antalya, Uturuki, beki huyo alikuwa chini ya uangalizi wa Daktari Haroun Ally.

Yanga itacheza na TP Mazembe, Jumanne ijayo mchezo wa Kundi A wa Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 

SIMBA YAANZA TENA HARAKATI ZA KUMSAJILI MAVUGO, ATATUA NCHINI SOOOOON...



Wakati wowote kuanzia sasa Simba itamleta nchini straika Laudit Mavugo baada ya kumaliza mkataba wake kuitumikia Vital’O ya Burundi baada ya awali dili hilo kushindikana.

Tangu mwaka jana, Simba ilikuwa ikimuwania Mavugo raia wa Burundi kila kipindi cha usajili kinapofika lakini mambo huaribika na ikabidi isubiri hadi straika huyo alipomaliza mkataba wake.

Mmoja wa mabosi wa Kamati ya Usajili ya Simba ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema Mavugo atatua wakati wowote kuanzia sasa na tayari alisaini mkataba wa miaka miwili tangu msimu uliopita.

Alisema mkataba huo uliigharimu Simba Sh milioni 36, lakini awali walibanwa na mambo ya mkataba wa straika huyo na timu yake hivyo kungoja hadi amalize mkataba.

“Mavugo atawasili nchini wakati wowote kuanzia sasa kwa kuwa ni mchezaji wetu na alisaini mkataba wa miaka miwili ya kuitumikia Simba na fedha zilizotumika kwenye usajili wake ni Sh milioni 36.

“Kwa sasa mkataba wake umekwisha kule katika timu yake aliyokuwa akiichezea, hivyo yupo huru na ni uhakika atatua kuja kuichezea Simba msimu ujao,” alisema bosi huyo. 

Mavugo ana uwezo mkubwa wa kuzifumania nyavu na Simba inaamini atakuwa mkombozi wao msimu ujao na kuzima ngebe za wapinzani wao.

SOURCE: CHAMPIONI

Friday, June 24, 2016

BAADA YA MKATABA WA BIN SLUM, MBEYA CITY YAANZA KUONYESHA JEURI YA FEDHA, YAIBOMOA PRISONS


Siku moja tu baada ya kuingia mkataba mpya na kampuni maarufu ya kuuza matairi nchini ya Bin Slum Tyres, klabu uya Mbeya City imeanza kuonyesha jeuri ya fedha.
Mbeya City imeingia mkataba na kiungo mshambuliaji kutoka Prisons ya Mbeya pia, mohammed Mkopi.

Mkopi amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea Mbeya City ambayo imesaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh milioni 300 kupitia bidhaa za betri za magari za RB kutoka kwa Bin Slum.

Awali, Mbeya City ilitaka kumchukua Didier Kavumbagu kutoka Azam FC, lakini raia huyo wa Burundi aliamua kwenda nchini Vietnam ambako ameanza maisha mapya ya soka.

TFF YASEMA YANGA ILIJICHANGANYA YENYE, YATUPA DONGO KUWA SEKRETARIETI YA JANGWANI INA MAPUNGUFU, YATISHIA KUTOA ADHABU




Kumekuwa na taarifa za upotoshaji kuhusu uratibu na ushiriki wa klabu za Tanzania katika mashindano ya kimataifa hususani ushiriki wa Young Africans SC katika mashindano ya Kombe la Shirikisho kwa msimu wa 2015/2016.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limekuwa likitoa kila aina ya msaasa uliowezekana kuisaidia klabu za Young Africans na Azam ambazo ziliwakilisha nchi katika mashindanmo ya kimataifa. Kwa upande wa Young Africans awali walishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na upande wa Azam ilishiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Mtakumbuka, Azam FC ilitolewa na Esperance ya Tunisia katika michuano hiyo na kwa upande wa Young Africans iliposhindwa kufuzu kwa hatua ya Nane Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikashushwa na kucheza na Esperanca Sagrada ya Angola na kuitoa hivyo kufuzu kwa hatua ya Nane Bora ya Kombe la Shirikisho au kwa lugha nyingine, hatua ya Makundi. TFF ikaendelea kuisaidia Young Africans kuhakikisha inashiriki vema katika mashindano hayo.
Sasa, Aprili 21, 2016 Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilitoa waraka kwa timu zilizokuwa zinacheza kuwania kuingia hatua ya Makundi (Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho) kupeleka majina ya maofisa watakaohudhuria warsha ya namna ya kuratibu mechi hizo kuelekea fainali. Kadhalika walitakiwa kupeleka vivuli (photocopies) vya hati zao za kusafiria.
Maofisa walihitajika ni meneja wa timu, daktari wa timu na ofisa habari wa timu. Taarifa hiyo ilikuja kabla ya Young Africans kucheza na Esperanca ya Angola. TFF iliwaataarifu Young Africans kwa kuwataka kutuma nyaraka hizo kati ya Aprili 26 na Aprili 28, 2016.
Lengo la warsha ilikuwa ni kujadili maswala ya uratibu, ufundi, udhamini na kanuni za mashindano. CAF ilijitolea kugharamia usafiri, malazi na gharama zote kwa watu watatu kutoka Young Africans SC.
Taarifa hizi na hata ukumbusho (reminders) zilipelekwa kwa baruapepe, simu na hata kuonana ana kwa ana kwa Katibu Mkuu wa Young Africans, Ofisa Habari na Viongozi wengine wa klabu.
Maofisa wa TFF kwa nyakati tofauti tofauti waliwasihi Young Africans na pia kuwakumbusha kutuma majina CAF na vivuli vya hati hati ya kusafiria, lakini kwa sababu wanazoweza kuzielezea wenyewe kwa nini hawakupeleka majina.
Mei 22, 2016 ikiwa ni siku mbili kabla ya warsha kuanza hapo Mei 24, 2016, Kaimu Katibu Mkuu wa Young Africans, Bwana Baraka Deusdedit alituma majina CAF yakiwa hayana vivuli yaani photocopies vya hati ya kusafiria.
Siku moja kabla ya washiriki kuanza kuwasili Cairo, Misri, Kaimu Katibu Mkuu wa Young Africans alituma nyaraka kama zilivyotakiwa na wakatumiwa tiketi tatu (3) na CAF. Pamoja na tiketi kuletwa Young Africans bado watu hao hawakusafiri wakidai klabu haijatoa ruhusa.
Maofisa wa TFF wamekuwa wakifanya kazi mpaka muda wa ziada wakiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Young Africans, Baraka Deusdedit ili timu iweze kushiriki vema pamoja na upungufu wa kiutawala ndani ya sekretarieti yake yanayojidhihirisha wazi.
Masuala yote yanayolalamikiwa na Ofisa Habari wa Young Africans, yaliyotolewa kwa timu zote kwenye semina ya Cairo, Misri.
TFF itaendelea kuvitembelea kusaidia klabu kujenga weledi kupitia mradi wa leseni za klabu na vilevile kuratibu ushiriki wa mashindano mbalimbali.
Hata hivyo, TFF haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa maofisa wa klabu wanaochafua jina la shirikisho ili kuficha madhaifu yao ya kiutawala (Administrative inefficiencies).

Thursday, June 23, 2016

ARGENTINA V CHILE NI FAINALI YA MARUDIO 2015

Chile
Chile imeifunga Colombia kwa bao 2-0 kwenye mchezo wa nusu fainali ya Copa America Centenario na itakutana na Argentina kwenye mchezo wa fainali kwenye uwanja wa MetLife mchezo wa fainali unaozikutanisha timu hizo baada ya mwaka mmoja.
Magoli ya mapema ya Charles Aranguiz na Jose Fuenzalida yaliipa La Roja  uongozi wa game hiyo mapema , licha ya Colombia kutengeneza nafasi za kutosha, hawakuweza kubadili matokeo hayo.
Chile na Argentina zimekuwa ni bora kwenye mashindano kwa muda mrefu na zinastahili kupambana kuwania ndoo ya Copa America kwenye mchezo wa fainali siku ya Jumapili.
Ni nafasi kwa Argentina kulipa kisasi baada ya kupoteza mchezo wa fainali ya michuano hiyo mbele ya Chile waliokuwa wenyeji wa mashindano mwaka uliopita.
Chile watakuwa na faida ya urejeo wa kiungo wao Vidal huku Diaz akitarajiwa kuwepo kwenye kikosi baada ya kuwa majeruhi huku kikosi kizima kikiwa kwenye form nzuri.
Argentina ndiyo wanapewa nafasi kubwa kwasababu ya walishaichapa Chile bao 2-1 kwenye hatua ya makundi. Argentina walicheza mchezo huo bila ya uwepo wa nyota wao Lionel Messi aliyekuwa akiuguza maumivu ya mbavu.
Wakiwa bila ya Ezequiel Lavezzi ambaye anauguza majeraha ya kiwiko, kikosi cha Tata Martino bado kina nyota wengine wengi ambao wanaweza kuziba nafasi hiyo.
Argentina watakuwa kwenye presha kubwa ukilinganisha na Chile. La Albiceleste  haijafanikiwa kutwaa taji hilo tangu ilipolinyakua kwa mara ya mwisho mwaka 1993. Baada ya kupoteza fainali mbili hivi karibuni ile ya Kombe la Dunia pamoja na Copa America, watakuwa wanataka kurekebisha makosa.
Messi bado ameendelea kukumbwa na jinamizi la kushindwa kutwaa mataji akiwa na timu yake ya taifa, Jumapili itakuwa ni nafasi yake nyingine ya kukamilisha ndoto zake za muda mrefu.

UNATAKA KUJUA NANI ANACHEZA NA YUPI 16 BORA YA EURO? RATIBA HII HAPA


TIMU ZILIZOFUZU HATUA YA 16 BORA YA EURO 2016

UBELGIJI YAITWANGA SWEDEN NA KUISUKUMIZA NJE YA EURO 201 NA ZLATAN WAKE

NAINGGOLAN AMBAYE NI MFUNGAJI WA BAO PEKEE KATIKA MECHI HIYO AKIMDHIBITI ZLATAN...

Radja Nainggolan anayewaniwa na Chelsea, ameifungia Ubelgiji bao moja tu muhimu lililoipa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sweden.

Ubelgiji imesonga mbele hatua ya 16 Bora lakini mshambuliaji nyota na nahodha wa Sweden, Zlatan Ibrahimovich na kikosi chake, wanarejea kwao Ulaya Kaskazini.

Mechi ilikuwa tamu na ya kuvutia, lakini mwisho Sweden wanafunga safari kurejea kwao baada ya kipigo hicho.a








Monday, June 20, 2016

HESHIMA KWAKE HUYU SHABIKI WA HISPANIA ASIYEONA, LAKINI YUKO UWANJANI KILA MECHI


Heshima kwake huyu shabiki wa Hispania ambaye hana uwezo wa kuona, lakini amekuwa akijitokeza uwanjani kuishangilia timu yake ya taifa.

Shabiki huyo amesafiri kutoka Hispania hadi Ufaransa kuiunga mkono Hispania katika mechi za Kombe la Euro ambayo ni mtetezi.

Kawaida amekuwa akibaki kifua wazi na kuandika maneno haya: “Sioni, lakini nasikia furaha.”

LEBRON AFANYA YAKE, AMPIGA BAO CURRY NA KUIPA CAVALIERS UBINGWA WA NBA



Nyota wa kikapu LeBron James amekamilisha ndoto yake ya kuiwezesha timu yake ya Cavaliers kubeba ubingwa wa Ligi ya Mpira wa Kikapu nchini Marekani maarufu kama NBA.

Cavaliers wamewatwanga wapinzani wao wakubwa Golden State Warriors kwa point 93-89 na kufanikiwa kushinda mchezo wa mwisho wakiwa ugenini.

Ilikuwa ni mechi ya kukata na shoka na Cavaliers walionyesha wamepania kufanya makubwa ugenini licha ya nyota Stephen Curry kuonekana kikwako kwao.

Kwa mara nyongine, James aliibuka bora katika mechi hiyo baada ya kumaliza akiwa na pointi  27 points, asisti 11 na ribaundi 11.













-------------------------------------------------------

-------------------------------------------------------
HABARI MPYAMPYAhttp://2.bp.blogspot.com/-mFnDPXvIysA/VOZH1z-2rpI/AAAAAAAAADs/shOR30FtkF4/s1600/anigif.gif