Friday, April 21, 2017

TFF imemfungulia mashtaka Haji Manara leo April 21, 2017


April 19, 2017 uongozi wa Simba kupitia kwa afisa habari wake Haji Manara uliotoa msimamo wao kuhusu masuala mbalimbali yanayoihusu klabu ya Simba dhidi ya TFF ikiwemo suala la pointi tatu (zinazogombewa na Simba pamoja na Kagera Sugar) ambalo linachukua taswira mpya kila kukicha.
Manara wakati akizungumza na waandishi wa habari, alizungumzia Simba kudhulumiwa na TFF kwenye baadhi ya mambo waliyofikisha kwenye vyombo vya sheria vya shirikisho hilo, aliituhumu TFF kuipendelea Yanga lakini pia akaituhumu TFF kuendeshwa kwa ukabila pamoja na mambo mengine.
Leo April 21, 2017 zikiwa zimepita siku mbili tangu Manara azungumze na vyombo vya habari, TFF imetangaza kufungua mashtaka ya kinidhamu dhidi ya Manara.
Kupitia ukurasa wa Instagram (tanfootball) ukurasa rasmi wa shirikisho la soka Tanzania, kuna habari inayosomeka kama ifuatavyo…
>>>Kwa mujibu wa Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kila mwanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania analazimika kuheshimu na kufuata kanuni za maadili za shirikisho kama zilivyoainishwa kwenye kanuni zake mbali mbali.
Wanafamilia wa mpira wa miguu ni pamoja na wachezaji, makocha, waamuzi, viongozi wa mpira wa ngazi zote na waajiriwa wa taasisi ambazo ni wanachama wa TFF wa ngazi mbalimbali.
Ili kutunza heshima ya mpira wa miguu Tanzania, wanafamilia wa mchezo huo katika kutimiza masharti ya kanuni za maadili za TFF, hawana budi kuheshimu na kufuata taratibu zote hizo ndani na nje ya uwanja.
Taswira njema ya shirikisho inajenga imani ya wadau wakiwamo serikali, mashirika mbalimbali ya umma na binafsi, vyombo vya habari, vyama vya mpira vya kimataifa, NGO’s na watu binafsi kwa taasisi (TFF). Kinyume chake ni kulibomoa shirikisho.
Dhima ya uongozi wa TFF ni pamoja na kulinda na kutunza heshima hii. Hivyo vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uvunjaji wa maadili havitavumiliwa, na vikitokea hatua zitachukuliwa.
Na kwa muktadha huu Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania, limemfungulia mashtaka ya kinidhamu Msemaji wa Simba Bw. Hajji Manara kwenye Kamati ya Nidhamu. Leo hii Aprili 21, 2017 atapewa mashtaka yake na kujulishwa lini na wapi yatasikilizwa.
TFF inaendelea kutoa rai kwa wadau wa mpira kuwa pamoja ni kwamba ni haki yao kushauri, kupendekeza, kukosoa lakini yote haya yafanyike kwa staha ili kutunza heshima ya mpira wetu.

No comments:

Post a Comment

-------------------------------------------------------

-------------------------------------------------------
HABARI MPYAMPYAhttp://2.bp.blogspot.com/-mFnDPXvIysA/VOZH1z-2rpI/AAAAAAAAADs/shOR30FtkF4/s1600/anigif.gif