Saturday, June 18, 2016

KOCHA MGHANA NDIYE ATAAMUA MAYANJA ANABAKI AU AENDE ZAKE

TETTEH
Kwa kiasi kikubwa Simba imeshamalizana na Kocha Mghana, Sellas Tetteh Teivi ili aje kukinoa kikosi hicho msimu ujao katika safari ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara. 

Sasa kali zaidi ni kwamba, kocha huyo ndiye atakayetoa ruhusa ya kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Jackson Mayanja kwamba aendelee na kazi au apigwe chini. 

Teivi amewahi kukinoa kikosi cha timu ya vijana ya Ghana na sasa akiwa na Sierra Leone amekabidhiwa hatma ya Mayanja ambaye mkataba wake wa awali unamtambulisha kama kocha msaidizi.

MAYANJA NA KIKOSI CHA SIMBA
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema, uongozi unasubiri ujio wa kocha mpya ili atoe pendekezo lake kama ataendelea na Mayanja au atakuja na msaidizi wake kwani kila mwalimu ana falsafa zake.

Habari zinasema, sekretarieti ya Simba imeliacha suala la Mayanja kwa Teivi ila wao sasa wanaendelea na mchakato wa kumpata kocha mpya wa makipa.

“Suala la kocha msaidizi tumeliacha kwanza, unajua makocha wengi wanapenda kuja na wasaidizi wao, iwapo huyu atakuja mwenyewe, basi atafanya kazi na Mayanja lakini kama atakuja na mwenzake, haina jinsi pia tunamsikiliza.
“Lakini sisi kama kamati (ya utendaji) kila mmoja anataka Mayanja tuendelee naye kutokana na kazi kubwa aliyoifanya msimu uliopita,” kilisema chanzo hicho.

Akiwa kaimu kocha mkuu akichukua mikoba ya Muingereza Dylan Kerr, Mayanja aliiongoza Simba katika mechi 16 za ligi kuu na kushinda 11, sare moja huku akifungwa michezo minne dhidi ya Yanga, Toto African, Mwadui FC na JKT Ruvu.

Hakuna kiongozi wa Simba ambaye alikuwa tayari kulitolea ufafanuzi suala hilo na hata ofisa habari wa timu hiyo, Hajji Manara alipotafutwa alisema: “Nipo likizo hivyo sijui kinachoendelea klabuni.”

No comments:

Post a Comment

-------------------------------------------------------

-------------------------------------------------------
HABARI MPYAMPYAhttp://2.bp.blogspot.com/-mFnDPXvIysA/VOZH1z-2rpI/AAAAAAAAADs/shOR30FtkF4/s1600/anigif.gif