Friday, November 18, 2016

Jicho la 3: Baada ya kuwasaini, Lwandamina, Hans van der Pluijm, Yanga itatisha…

george-lwandamina

SIJUI uwezo wa kocha mpya wa Yanga SC, Mzambia, George Lwandamina lakini naamini kitendo cha uongozi wa timu hiyo kumng’ang’ania na kumshawishi mkufunzi raia wa Holland, Hans van der Pluijm kubaki klabuni hapo ni hatua kubwa ya kuendelea kusonga mbele kimpira kwa mabingwa hao mara mbili mfululizo wa ligi kuu Tanzania Bara.
Hans mshindi mara mbili wa VPL na kocha aliyeipa Yanga taji la FA Cup msimu uliopita, ikiwemo rekodi ya kuifikisha timu hiyo katika hatua ya makundi ya michuano ya Caf Confederation Cup 2016 kwa mara ya kwanza amekubali ‘kiroho safi’ kubadilishiwa majukumu, kutoka mkufunzi mkuu wa timu hadi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi ndani ya kikosi cha mabingwa hao mara 26 wa kihistoria.
Nilishaandika sana kuhusu, Hans, uwezo wake wa kufundisha na kupata matokeo, ukarimu wake na namna alivyo na sifa za kiongozi bora.
Yanga ‘imelamba dume’ kwa mara nyingine na ushirikiano wa Hans kama Mkurugenzi wa ufundi na Lwandamina kama kocha mkuu ni sawa na ‘kunoa makali’ ya kisu kilichokuwa na makali. Yanga ‘watatisha.’
Ndani ya uwanja Yanga watakuwa bora zaidi ya vile ambavyo ingekuwa endapo Mholland huyo angeondoka kabisa katika kikosi hicho.
Wakati mwenyekiti wa klabu, Yusuph Manji akiendelea kuboresha safu ya utawala kwa kumuajiri, Mfaransa kama Mtendaji mkuu wa klabu bila shaka atakuwa ametambua thamani ya uongozi na mchango wa Hans katika maendeleo ya klabu.
Watu hawa wanne, makamu mwenyekiti, Clement Sanga na wajumbe wa kamati ya utendaji wakishikamana Yanga itapaa.
Wanachopaswa kufanya kwa sasa benchi la ufundi kwa kushirikiana na Hans ni kufanya maboresho kikosini hasa wakilenga timu ambayo watakuwa nayo katika michuano ya Caf Champions League 2017.
Lwandamina aliisaidia Zesco United kufika nusu fainali katika michuano ya mabingwa Afrika mwaka huu na Hans aliiongoza Yanga katika michezo 14 ya Champions league na Confederation hivyo wote watakuwa wakifahamu nini cha kufanya ili kuwa na timu bora zaidi katika michuano ya 2017 ambayo ukifika hatua ya timu 16 bora moja kwa moja timu itakuwa imefuzu kwa hatua ya makundi.
Yanga itakuwa na michezo 11 katika uwanja wa Uhuru katika game za mzunguko wa pili, hii ni faida kubwa kwao japokuwa watalazimika kupambana haswa ili kupata matokeo yatakayowasaidia kuhifadhi taji la VPL kwa mara ya 3 mfululizo.
Jambo la muhimu kwao hivi sasa ni kufanya tathmini ni aina gani ya wachezaji ambao wanapaswa kupunguzwa na kuongezwa ili kuendana na malengo wanayokusudia. Yanga inapaswa kumsaini kiungo wa kati mwenye uwezo wa juu zaidi ya waliopo sasa (hasa yule wa ulinzi).
Yanga inapaswa kusaini mlinzi wa kushoto wa kusaidiana na kina Mwinyi Hajji na Oscar Joshua ambao wakati mwingine majeraha yao yamekuwa yakiathiri kiwango cha ufanisi wa timu.
Yanga inapaswa kuwaongezea mikataba wachezaji wao wa kulipwa kama Vicent Bossou, Thaban Kamusoko, Donald Ngoma, Amis Tambwe na Haruna Niyonzima ambao kwa hakika nawatazama kama nguzo yao muhimu ndani ya uwanja.

No comments:

Post a Comment

-------------------------------------------------------

-------------------------------------------------------
HABARI MPYAMPYAhttp://2.bp.blogspot.com/-mFnDPXvIysA/VOZH1z-2rpI/AAAAAAAAADs/shOR30FtkF4/s1600/anigif.gif