USHABIKI
wa michezo ni furaha, ukiuendekeza mara nyingi unavuka mipaka kutoka
katika furaha na mwisho unakuharibia mambo mengi sana ya muhimu.
Ushabiki
wa michezo na hasa soka, umewagombanisha wengi na rafiki na ndugu zao.
Umewajengea wengi uadui na wengine, umeanzisha misigano na kutoelewana
kwa wengi.
Wapo
waliopoteza kazi zao au hata kuingia katika migogoro kwa majirani au
familia zao lakini yote yanatokana na migogoro inayotokana na ushabiki
wa kupindukia.
Hakika
ushabiki haupaswi kuwa wa kupindukia na kufikia kujenga uadui au
makundi yanayoeneza chuki na kupoteza kabisa maana ya ushabiki wenyewe.
Labda
nikukumbushe Rwanda baada ya kupita katika mauaji ya kimbari mwaka 1994
waliutumia mchezo wa mpira kuwakutanisha wananchi wake, safari hii
wakijulikana kama Wanyarwanda na kwa pamoja wakafuta yale mambo ya
makabila matatu, Watutsi, Wahutu na Watwa.
Unakuta
Mtutsi na Mhutu kwa pamoja wanashabikia APR na Mtusi, Mtwa na Mhutu
wanashangilia Rayon. Kwa pamoja wanaungana na taratibu wakaanza kusahau
machungu na kuondoa visasi, watu wakasameheana na kuanza kuishi maisha
mapya.
Nchi
nyingi zimetumia njia hiyo kuhakikisha zinarejea katika mstari sahihi
kwa kuwa furaha ya michezo inayojenga ushabiki inaweza kuwa furaha na
faida badala ya hasara.
Juzi,
mashabiki wa Borussia Dortmund ya Ujerumani walifanya kitu kingine
kinachoweza kukumbukwa kwa muda mrefu hasa tunapozungumzia faida ya
ushabiki.
Mechi
ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Dortmund na AS Monaco ya Ufaransa
ilitarajiwa kuchezwa Jumanne mjini Dortmund, Ujerumani. Lakini wakati
basi la wachezaji wa wenyeji likiwa njiani, lilishambuliwa na milipuko
mitatu, hivyo kusababisha mechi kusogezwa mbele.
Hatua
hiyo ilivuruga ratiba ya mashabiki wa AS Monaco ambao walijua
wangeondoka usiku baada ya mechi na wengine alfajiri kurejea Ufaransa.
Lakini sasa walilazimika kusubiri hadi Jumatano kwa kuwa mechi
ilisogezwa ili waondoke Alhamisi. Gharama ikaongezeka kwao na bajeti
ikavurugika.
Iliwezekana
wangeanza kurejea Jumatano bila kuona mechi kwa kuwa hawakuwa na
ujanja. Lakini mashabiki wa Dortmund walitaka wenzao waone mechi yao na
walichofanya ni kuzungumza, wakajiunganisha na kuanza kuwaalika.
Karibu
kila familia yenye mashabiki wa Dortmund ilialika mashabiki kadhaa wa
Monaco ambao bajeti yao ilikuwa imevurugika, wakala nao, wakanywa nao na
hata wengine wakalala katika majumba yao.
Juzi
Jumatano, mechi ikachezwa na wenyeji wakalala kwa mabao 3-2. Wana deni
watakapokwenda Monaco, Ufaransa kuhakikisha wanawashinda wenyeji wao ili
wasonge mbele. Lakini mashabiki wao wanaingia kwenye rekodi ya kuwa
moja ya mashabiki wa aina yake.
Mashabiki
wa Dortmund wameonyesha ushabiki ni zaidi ya furaha kwa timu, badala
yake ndani yake kunaweza kuwa na urafiki, undugu na kuthamini au kujali
furaha ya mwingine.
Vipi
wewe shabiki wa Simba, unampiga yule wa Yanga bila kosa kwa kuwa tu
amevaa nguo za njano kwenye jukwaa la upande wa Simba? Ukimuelekeza na
kumueleza si sehemu sahihi kwake, tatizo ni nini?
Ukiingia
uwanjani wewe shabiki wa Yanga, ukashangilia kwa juhudi na kufurahi na
wenzako bila kumtukana matusi ya nguoni yule wa Simba, hasara yako ni
ipi?
Mashabiki
wengi hasa wa soka hapa nchini wanataka kuonyesha mchezo wa soka si wa
kiungwana, ni mchezo wa kibabe, mchezo wa wahuni au watu wasio na
mpangilio. Jambo ambalo si kweli hata kidogo, badala yake ni nguvu ya
wapuuzi wachache wenye nguvu inayowapa ruhusa kuonyesha upuuzi wao mbele
ya wengine.
Unaweza
kufurahia au kusherehekea bila kuumiza wengine, bila kuwabugudhi au
kuwadhalilisha. Somo la mashabiki wa Dortmund, linatoa funzo kwa
mashabiki wengi wa soka duniani lakini wale wa Yanga na Simba, hili ni
lenu na ndio mnahusika hasa, jifunzeni.