Thursday, November 17, 2016

Man United vs Arsenal


man-united-vs-arsenal
Mapambano katika vita sikuzote ni kuhakikisha tusitegemee katika kuamini kuwa, adui hata kuja upande wetu lakini tumsome na kujifunza kumpokea pale anapowasili.
Usiwaze kuwa hatokushambulia kwanza lakini unahakikisha kuwa unakuwa kwenye nafasi ambayo inakufanya kuwa salama dhidi yake huku unajipanga kumdhuru inavyotakiwa, hii ndiyo namna ambayo akili ya ushindi inavyotakiwa kuwa siku zote, hivyo ndivyo ambavyo Simba humuwinda Nyati siku zote na kila mla nyama hushika kisu kwa namna hiyo.
Hakuna asiyekuwa na tamaa na mchezo kati ya Manchester United dhidi ya Arsenal, hakuna jicho ambalo mboni yake haitofurahi kushuhudia uso mkavu wa Mourinho dhidi ya taswira ya huruma ya Arsenal Wenger zikitazamana katika nyasi ambazo ni wazi zitaumia kwa dakika 90 na zile za nyongeza ambazo muuaji wake ni Andre Marriner.
Kila roho itakuwa na hatima yake, kila majigambo yatapata mbabe wake na hakuna namna nyingine zaidi ya kuamini kuwa kila hasira itabidi ikinzane na furaha nyingine japo jambo zuri ambalo linaufanya huu mchezo kuwa wa kuvutia pengine ukaweza kuuita Pizza ni chuki iliyopo baina ya makocha hawa wawili. Hawakubaliani, hawafuatiliani, na wala hawahitajiani katika pembe ya kila mmoja, wote wanaamini ni Faru ingawa mwingine anayeitwa Mourinho pembe yake imemdhuru zaidi Wenger.
Silaha hazishushwi na mageuzi yanayoweza kufanyika siku hii, Manchester United bado hawana muunganiko kikosini mwao huku Arsenal wakiwa katika Kitonga na gari yao yani wanateremka tu.
Ozil macho yake yamekuwa makubwa zaidi na sasa anaziona nyavu kwa ufasaha kuliko alivyokuwa akiona miili ya wenzie ili awapigie pazi za mwisho, lakini pia Sanchez yupo katika kiwango chake cha Bugatti kiwango ghali kabisa katika maisha yake ya soka kwa sasa amekomaa, anawahusisha wengine mchezoni na anafanya kila anayemzunguka aonekane Daudi anayeweka kumuangusha Goliati yeyote anayekuja mbele yake.
Hii ndiyo silaha yao kwa sasa yani ubora wa watu hawa wawili ndio unaamua matokeo ya Arsenal kwa kiasi kikubwa huku kisimani wakiachiwa Granit Xhaka na Francis Coquelin wafate maji.
Mourinho siku zote kuhusu Wenger katika mechi za kimashindano amekuwa ni nyumba ya Kobe, kila jiwe lilipokuja upande wa kichwa chake halikumpata kwasababu ilikuwa rahisi kwake kurejesha kichwa ndani huku akiwa na sumu ya koboko. Kila alipong’ata Wenger alimuua na hakuna namna ambayo Wenger angeweza kufanya lakini hakuna wakati mzuri ambao pengine Wenger alikuwa akiuombea kama huu, ule wakati ambao adui hana mikono huku akitakiwa kukumaliza kwa bunduki.
Manchester United kwa sasa ‘maji kujaa’ lakini nyakati nyingi inakuwa ‘maji kupwa’, Mourinho hajapata muunganiko ambao ulizoeleka hapo kabla kwenye vilabu vingine alivyopita, pamoja na kuwa kuna nyakati wachezaji kama Pogba wanakuwa na nyongeza ya kile ambacho wengi wanategemea kukiona kutoka kwao bado Mourinho taa za gari lake zimezima au mwanga wake umefifia na hata lile kurunzi alilolinunua ili wakati amezidiwa limulike halijaweza kuwa fiti huku pia likionekana kutoingia kwenye mfumo linaitwa Henrikh Mkhitaryan.
Huu pia unaweza kuwa wakati mbaya zaidi kwa Arsenal Wenger kwasababu kwa namna Manchester United walivyokutana na ugumu katika mechi kubwa, silaha ya Mourinho inaweza kuwa kujihami na kuwazuia Arsenal ambao wanatiririka wasiweze kucheza kwa uhuru.
Mourinho ni ngumu kwake kuweka kichwa mahali ambapo nyumba ya Wenger inaweza kukua hivyo kutaka kufanya pambano liwe refu na wakati ambao vijana wa Arsenal wanakuwa wameishiwa nguvu au kuondoka kwa wingi ili wakashambulie aweze kutumia mwanya huo kuwaumiza.
Mamba kamwe hang’oki meno kwasababu uhai wake hutegemea hapo, hivyo akiwa mpole haina maana kuwa unatakiwa kuweka kiganja kwenye mdomo wake, hii ndiyo inatakiwa kuwa akili ya Wenger wakati huu.
Pamoja na kuwa Mourinho anaweza kuwa kwenye wakati mgumu bado anabaki kuwa moja ya makocha wa kiwango cha Dunia na uzoefu wake unaweza kuwaumiza Arsenal wakati wowote kama hawatokuwa makini na nafasi wanazozitengeneza na kama Mustafi na Koscielny hawatakuwa makini muda wote jambo ambalo halijawa tabia yao msimu huu.
Hakuna asiyetamani pilau siku za siku kuu, sembuse hili ambalo kachumbari katengeneza muhindi? Pilipili yake kila mmoja itamfaa utamu wake kila mmoja ataufurahia na wapo ambao wanatamani hata mwiko uwe wao waamue pishi litavyotoka hao wanaitwa Manchester City, Liverpool na Chelsea. Adui mwombee njaa lakini hawa wanawaombea arosto ili hata dawa watakazo zihitaji ziendelee kuwalevya.
Unapotamani kuua kwa upanga, kumbuka shoka anaweza kuwanayo jirani, umakini tu ndio utaamua mchezo huu ingawa hakuna siri sufuria lipo kwa Mourinho na mwiko anao Wenger mwenyewe wakati huu, ujanja wake tu namna ya kuivisha, kisipoiva shauri yake.

No comments:

Post a Comment

-------------------------------------------------------

-------------------------------------------------------
HABARI MPYAMPYAhttp://2.bp.blogspot.com/-mFnDPXvIysA/VOZH1z-2rpI/AAAAAAAAADs/shOR30FtkF4/s1600/anigif.gif